62. Allaah hamuhitajii yeyote kabisa


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna yeyote awezaye kujitosheleza Naye.

MAELEZO

Hakuna yeyote awezaye kujitosheleza na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala) kuwaambia watu wote wakiwemo wafalme, wakuu na matajiri:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

“Enyi watu!  Nyinyi wote ni mafakiri kwa Allaah na Allaah ndiye Mkwasi,  Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[1]

Kila mtu ni mwenye kumuhitajia Allaah, hakuna yeyote ajitoshelezaye kutokamana na Allaah. Ni mafukara na wenye kumuhitajia Allaah pasi na kujali ni kiasi gani cha mali anamiliki. Ni nani anayemlindia mali yake? Ni nani ambaye anampa uzima mwili wake? Ni nani anayemfunza namna ya kuchuma mali hiyo? Ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Nyinyi ni wenye kumuhitajia Allaah kwa kila njia na Allaah pekee ndiye ambaye ni mkwasi kwa viumbe Wake. Allaah ni Tajiri Mwenye kujitosheleza, Ambaye sifa zote njema zinamrejelea Yeye kutokana na matendo Yake, makadirio na kila kitu. Kila anachokifanya ni chenye kusifiwa, kwa sababu anakiweka kila kitu mahali pake stahiki. Endapo Allaah asingeumba isipokuwa ukafiri peke yake basi hakuna yeyote ambaye angeliingia Peponi. Allaah ameumba Pepo na Moto, ukafiri na imani. Baadhi wataingia Motoni na wengine wataingia Peponi. Wale ambao watafanya matendo mema wataingia Peponi na wale watakaokufuru na maovu wataingia Motoni. Allaah hawalinganishi baina ya hao wawili. Amesema (Ta´ala):

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[2]

[1] 35:15

[2] 45:21

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 49
  • Imechapishwa: 05/08/2021