61. Maandiko yanatakiwa kukubaliwa hata kama hayafahamiki


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye alama tatu ni mnafiki.”[1]

Hapa ni kwa lengo la kukemea. Tunazipokea kama zilivyokuja na wala hatuzifasiri.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”[2]

“Pindi waislamu wawili watapokutana na silaha zao yule muuaji na yule muuliwaji Motoni.”[3]

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”[4]

“Yule mwenye kumwambia nduguye “ee kafiri”, basi imemgusa mmoja wao.”[5]

“Ni kumkufuru Allaah mtu kuikana nasabu yake hata kama imefichikana.”[6]

Hizi na Hadiyth mfano wake ambazo ni Swahiyh na zimehifadhiwa tunajisalimisha nazo ijapokuwa hatuzielewi. Hatuzizungumzii, hatujadiliani nazo na wala hatuzifasiri kwa njia inayopingana na uinje wake. Hatuzirudishi isipokuwa kwa kitu kilicho na haki zaidi ya kukipokea.”

MAELEZO

Alipotaja ya kwamba unafiki ni kuonyesha Uislamu na kuficha ukafiri ndipo akataja Hadiyth zinazotaja alama za wanafiki. Hapa Imaam Ahmad amefanya tofauti kati ya unafiki sampuli mbili. Amesema:

“Yule mwenye alama tatu ni mnafiki.”

Hapa ni kwa lengo la kukemea. Tunazipokea kama zilivyokuja na wala hatuzifasiri.”

Bi maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamaanishi kuwa ni wanafiki wa kitiikadi ambao wanaficha kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake na siku ya Mwisho. Huu ni unafiki aina nyingine uliotajwa kwa lengo la kukaripia. Kwa msemo mwingine yule mwenye unafiki huyu ana unafiki moja wapo miongoni mwa unafiki walionao wanafiki. Wanachuoni wanaita unafiki sampuli hii ya kwamba ni unafiki wa kimatendo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye alama tatu ni mnafiki; anapozungumza anasema uongo, anapoahidi anavunja ahadi na anapoaminiwa anakhini.”[7]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… pindi anapogombana anaapiza, anapoahidi anasaliti.”

Hizi ni alama za unafiki wa kimatendo. Anaweza kuwa na unafiki wa kimatendo. Hata hivyo ni wajibu kutahadhari na mtu ambaye anapoahidi anavunja ahadi, anapoapa anasema uongo, anapoaminiwa anafanya khiyana na anapogombana anaapiza. Ni wajibu kwetu kumjengea dhana mbaya na kutahadhari naye, kwa sababu ana alama zenye nguvu kabisa miongoni mwa alama za wanafiki. Hatuna uhakika juu ya hilo, lakini tunatakiwa kuwa makini.

Tunataja Hadiyth hizi pasi na kukata moja kwa moja kuwa wale walio na sifa hizi ni makafiri. Tunachukua msimamo wa kusimama katika suala hili. Hili linazipa Hadiyth mshtuko. Baadhi ya Salaf  wamesema kuwa hawazifasiri Hadiyth mfano wa hizi. Salaf wengine wakazifasiri kwa ajili ya kuwaraddi Khawaarij. Kwani Khawaarij wanaonelea kuwa yule ambaye yuko na moja katika alama hizi ni mnafiki mia kwa mia. Kwa ajili hiyo wakawakufurisha watu. Sisi hatufanyi hivo.

Ima tunazitaja kwa lengo la kukhofisha na kuogofya. Tukiingia katika mjadala kuhusu matendo haya tunazifasiri kuwa ni unafiki wa kimatendo na kufuru ndogo. Kwani kuna kufuru kubwa na kufuru ndogo. Kuna unafiki mkubwa na unafiki mdogo. Kuna shirki kubwa na shirki ndogo. Moja ya sababu inaweza kuwa pale tunapojadiliana na Khawaarij waliopindukia. Hapa tunalazimika kupambanua na kusema kuwa alama hii ni kufuru ndogo. Tukiwaona wasiokuwa na elimu wanatumbukia katika maasi haya tunawatajia Hadiyth kwa njia ya kutopambanua kwa ajili ya kuwakhofisha.

Udhahiri ni kwamba haya ndio madhehebu ya Ahmad (Rahimahu Allaah). Dalili ya hili ni yale yaliyopokelewa. Anaenda kinyume na Khawaarij na ni mmoja katika wanaowapiga vita kwa ukali kabisa.  Wanatumia Hadiyth kama hizi kwa sababu ya kuwakufurisha watenda madhambi makubwa. Ahl-us-Sunnah hawawakufurishi wenye kutenda madhambi makubwa. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”

Khawaarij wanatumia dalili Hadiyth hii wakati wa kukufurisha. Ahl-us-Sunnah wanapinga na kusema kuwa sio dalili kabisa ya hilo. Kwani Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yatapigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni kati yao kwa uadilifu na tendeni haki. Kwani hakika Allaah anawapenda wanaotenda haki. Hakika waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”[8]

Amewathibitishia imani na udugu wao wa kiimani pamoja na kuwa wamepigana. Lakini huyu anayempiga vita muislamu kwa kuamini kuwa ni halali ni kafiri. Na ikiwa anaonelea kuwa ni haramu kumuua muislamu lakini akafanya hivo kwa sababu ya matamanio, sababu, chuki au kitu kingine, basi kitendo hicho ni haramu na yule mhalifu sio kafiri. Katika hali hii kufuru yake ni ndogo na ni kufuru ya kimatendo isiyomtoa mtu katika Uislamu. Kwa ajili hiyo Abu ´Ubayd, Ibn Taymiyyah na maimamu wengine wamezifasiri Hadiyth hizi ambazo zimeshikiliwa na Khawaarij kwa ajili ya kuwakufurisha waislamu watendao madhambi kama vile uzinifu, unywaji pombe, mauaji, mapigano na mfano wa hayo. Ahl-us-Sunnah wanazifasiri Hadiyth hizi kwa njia tuliyoitaja.

Vilevile inahusiana na Hadiyth:

“Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pindi anapokunywa pombe hali ya kuwa ni muumini, hapori mwenye kupora pindi anapopora, jambo linalofanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[9]

Mtu kama huyu anatakiwa ima aadhibiwe kwa kupigwa mawe au atandikwe bakora. Lau angelikuwa kafiri basi angeliguswa na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[10]

Mtu kama huyu anatakiwa kuuawa. Kwanza anatakiwa kuambiwa atubie. Ima atubie na la sivyo anauawa hali ya kuwa ni mwenye kuritadi na si hali ya kuwa ni mtenda dhambi.

Mwizi anatakiwa kukatwa mkono hali ya kuwa ni adhabu yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ ۗوَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke wakateni mikono yao – ni malipo kwa yale waliyoyachuma; [Shari´ah hii] ni makemeo makali kutoka kwa Allaah. Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[11]

Lau mwizi angelikuwa amekufuru basi angeuawa na si kukatwa mkono peke yake.

Shari´ah yote kwa ukamilifu wake inatakiwa kuchukuliwa. Dalili zinatakiwa kuoanishwa. Lakini wale ambao nyoyoni mwao mna upotevu hufuata yale  maandiko yasiyokuwa wazi kwa ajili ya kutafuta fitina na kutafuta kuyapindisha maana yake. Ahl-us-Sunnah wanafuata yale maandiko yaliyo wazi na wanayarudisha yale maandiko yasiyokuwa wazi  kwa yale yaliyo wazi. Wanachukua haya maandiko yasiyokuwa wazi, wanayarudisha kwa yale maandiko yaliyo wazi na kuyaoanisha. Hawayagonganishi haya kwa haya, kama wanavyofanya Khawaarij, Murji-ah, Mu´tazilah na Ahl-ul-Bid´ah wengine. Ahl-ul-Bid´ah hushikilia andiko lililo na utata na kuanza kulijengea juu yake Bid´ah. Baada ya hapo wanawakufurisha waislamu na mengineyo. Kuhusu wale ambao wamebobea katika elimu wanazioanisha dalili ili waweze kuzitendea kazi zote. Ndio maana tunasema kuwa inahusiana na kufuru ndogo katika maandiko haya. Wakati fulani tuna haki ya kusema tu kuwa ni kufuru, lakini tunaamini kuwa ni kufuru ndogo. Mfano wa kufuru kubwa ni kumkadhibisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumtukana Allaah au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kukanusha kitu kinachojulikana fika katika Uislamu, kupinga moja ya nguzo za Uislamu kama vile swalah, swawm na zakaah, kuwakana Malaika, Pepo au Moto na mfano wa hayo. Haya ni kufuru kubwa inayomtoa mtu katika Uislamu. Vivyo hivyo kufanya mzaha juu ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuifanya haki si lolote si chochote au kuifanyia kiburi. Yote haya ni kufuru zinazomtoa mtu katika Uislamu na kuhusu watenda madhambi waliotajwa katika Hadiyth zilizotangulia ni kufuru ndogo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kumwambia nduguye “ee kafiri”, basi imemgusa mmoja wao.”

Hii ni kufuru ndogo. Isipokuwa ikiwa anaonelea kuwa dini ya muislamu huyu ni kufuru ambapo akawa amemkufurisha. Katika hali hii mtu huyu ni kafiri. Dhambi yake ni kufuru ya kikweli. Ama ikiwa amemkufurisha kwa hasira kwa sababu tu ya mambo yenye tofauti au kwa sababu nyingine, sio kufuru kubwa. Bali ni kufuru ndogo. Unaweza siku zote kumtia sawa ndugu yako pasi na kumkufurisha.

Imaam Ahmad amesema:

“Hizi na Hadiyth mfano wake ambazo ni Swahiyh na zimehifadhiwa tunajisalimisha nazo ijapokuwa hatuzielewi.”

Haya ameyasema Ahmad kwa sababu ya unyenyekevu. Kuna uwezekano anawakusudia wale watu wa kawaida wasiozielewa; wanatakiwa kujisalimisha nazo kwa hali yoyote. Ama kuhusu wanachuoni waliobobea katika elimu kama Ahmad (Rahimahu Allaah), wanazifasiri kwa mujibu wa madhehebu ya Ahl-us-Sunnah. Aliwapiga vita Khawaarij walioshikilia maandiko haya na akawapiga vita Murji-ah walioshikilia maandiko yanayohusiana na ahadi. Alipambana na mapote yote, jambo ambalo linathibitisha kuwa alikuwa ni kiongozi katika Sunnah. Vilevile (Rahimahu Allaah) anajua maana ya Hadiyth hizi.

[1] al-Bukhaariy (33) na Muslim (59).

[2] al-Bukhaariy (121) na Muslim (65).

[3] al-Bukhaariy (31) na Muslim (2888).

[4] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[5] al-Bukhaariy (6104) na Muslim (60).

[6] Ahmad (2/215). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (4485).

[7] al-Bukhaariy (33) na Muslim (59).

[8] 49:09-10

[9] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[10] al-Bukhaariy (3017).

[11] 05:38

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 438-442
  • Imechapishwa: 01/01/2018