Alikuwa akisujudu juu ya ardhi mara nyingi[1].

Ilikuwa inatokea wakati mwingine Maswahabah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaoswali pamoja naye kipindi cha joto kali na hivyo hawawezi kuweka paji za uso ardhini, hutandaza nguo zao na wakasujudia juu yake[2].

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ardhi yote imefanywa kwangu mimi na Ummah wangu kuwa mahala pa kuswali na safi. Popote pale ambapo mwanamume kutoka katika Ummah wangu wakati wa swalah utamwingilia, hapo hapo ndipo ipo sehemu yake ya kuswalia na twahara yake. Waliokuwa kabla yangu walikuwa wakilichukulia hilo kubwa na walikuwa hawaswali kwengine isipokuwa tu kwenye makanisa na masinagogi yao.”[3]

Wakati mwingine ilikuwa inaweza kutokea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifanya Sujuud kwenye udongo na maji. Ilimtokea asubuhi ya tarehe 21 Ramadhaan. Kulinyesha mvua usiku huo na paa la msikiti (lililokuwa la majani ya mitende) liliezuka. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasujudu kwenye maji na udongo. Abu Sa´iyd al-Khudriy amesema:

“Nikaona namna ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na athari ya maji na udongo kwenye paji lake la uso na kwenye pua yake.”[4]

Aliswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenye Khumrah[5][6].

Mara nyingine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali kwenye jamvi/zulia[7].

Wakati mwingine ilitokea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaswali kwenye kinguo chake alichokiweka mbele[8].

[1] Hili ni kwa sababu Msikiti wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa haukufunikwa kwa majamvi na vyenginevyo, kama zitavyothibitisha Hadiyth nyingi kukiwemo inayofuata na ya Abu Sa´iyd itakayofuatia.

[2] Muslim na Abu ´Awaanah.

[3] Ahmad, as-Sarraaj na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[4] al-Bukhaariy na Muslim.

[5] Khumrah ni kipande cha kitambaa kilichofanywa kwa ajili tu ya kuweka uso katika Sujuud. Kimetengenezwa kwa jamvi, nguo na miti mingine. Khumrah sio kubwa zaidi ya hivyo.” Tazama “an-Nihaayah”.

[6] al-Bukhaariy na Muslim.

[7] Muslim na Abu ´Awaanah.

[8] al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth inathibitisha ya kwamba inafaa kukalia nguo zake. Inathibitisha vilevile kuwa imeharamishwa kukalia hariri. Imethibitishwa katika al-Bukhaariy na Muslim ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameharamisha kukalia nguo ya hariri. Bali kumesimuliwa waziwazi ya kwamba ni haramu kukalia hariri. Hivyo basi usidanganyike na wale wakubwa wanaojuzisha hilo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 130-131
  • Imechapishwa: 07/08/2017