Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

…Vitabu Vyake…

MAELEZO

Vitabu ni wingi wa “kitabu”. Makusudio ya vitabu hivi ni vile ambavyo Allaah ameviteremsha kwa Mitume Yake kama rehema na uongofu kwa viumbe. Lengo yavyo ni ili waweze kufikia furaha duniani na Aakhirah.

Kuamini vitabu kunakusanya mambo manne:

1- Kuamini kwamba ni kweli vimeteremka kutoka kwa Allaah.

2- Kuamini vile vitabu ambavyo tumevijua majina yake. Mfano wa hivyo ni Qur-aan ambacho kimeteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Tawraat ambayo imeteremshwa kwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Injiyl ambayo imeteremshwa kwa ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na az-Zabuur ambayo imeteremshwa kwa Daawuud (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama vile tusivovijua majina yake, tunatakiwa kuviamini kwa njia ya jumla.

3- Kuamini yale maelezo sahihi, kama maelezo ya Qur-aan, na yale maelezo ambayo hayakubadilishwa wala kupotoshwa katika vile vitabu vilivyotangulia.

4- Kutendea kazi zile hukumu ambazo hazikufutwa na kuridhia na kujisalimisha nazo pasi na kujali ikiwa tumefahamu hekima yake au hatukuifahamu. Vitabu vyote vilivyotangulia vimefutwa kwa Qur-aan Tukufu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ

“Tumekuteremshia Kitabu kwa haki kinachosadikisha yale yaliyokuja katika Vitabu vilivyokuwa kabla yake na chenye kuvidhibiti.” (al-Maaidah 05 : 48)

Bi maana ni chenye kuvihukumu. Kujengea juu ya haya haijuzu kutenda kazi kwa mujibu wa hukumu za hivyo vitabu vilivyotangulia ikiwa sio sahihi au kukubaliwa na Qur-aan.

Kuamini vitabu kunazalisha matunda ikiwa ni pamoja na:

1- Ujuzi juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) amewatilia umuhimu waja Wake, kwa vile kila watu amewateremshia kitabu wanaongozwa kwacho.

2- Ujuzi juu ya hekima ya Allaah (Ta´ala) katika Shari´ah Yake, kwa kule kuwawekea Shari´ah kila watu kulingana na yale yanayoendana na hali zao. Allaah (Ta´ala) amesema:

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila Ummah katika nyinyi Tumeujaalia Shari’ah na mfumo wake. (al-Maaidah 05 : 48)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 01/06/2020