61. Hakupitiki chochote isipokuwa kwa utashi wa Allaah

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Ametakasika Allaah kutokamana na kuweko ndani ya ufalme Wake yale asiyoyataka.

MAELEZO

Ametakasika Allaah kutokamana na kuweko ndani ya ufalme Wake yale asiyoyataka. Hakupitiki ndani ya ufalme Wake isipokuwa yale aliyoyataka. Hilo limekusanya kizuri na kibaya, ukafiri na imani, uongofu na upotofu. Anakiweka kila kitu mahali pake stahiki.

Haya ni tofauti na ´Aqiydah ya Qadariyyah. Wao wanaona kuwa Allaah hakutaka ukafiri wala shari. Kuonelea kwamba ndani ya ufalme Wake kunapitika yale asiyoyataka kunajulisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) si muweza. Hapana, kheri na shari vyote viko mikononi mwa Allaah. Kufuru na imani vyote vinatokamana na makadirio ya Allaah (´Azza wa Jall). Hakuyaumba pasi na malengo wala dhumuni.

Kwa mfano Allaah ameumba sumu. Sumu ni yenye kudhuru na kuua. Lakini ikitumiwa ipasavyo inaweza kunufaisha au kudhuru. Allaah anaweza kufanya ikampata yule anayetaka kumuadhibu na hivyo ikamdhuru. Anaweza kufanya impate yule ambaye anataka kumponya na hivyo akaponya. Allaah ndiye ambaye ameumba sumu hii. Ingawa ni yenye kuua lakini ndani yake kuna hekima.

Ameumba njaa na shibe kutokana na hekima. Kwa ajili ya majaribio na mtihani. Ameumba maradhi na uzima. Ameumba vinyume viwili, lakini kila kimoja kinawekwa mahali pake stahiki. Endapo Allaah asingeliumba isipokuwa kheri tupu basi kila mtu angeliingia Peponi. Lakini anachotaka Allaah (Jalla wa ´Alaa) ni kwamba asiwepo yeyote ambaye ataingia Peponi isipokuwa kutokana na matendo yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“ingieni Peponi kwa yale mliyokuwa mkitenda.”[1]

Hakuna ambaye ataingia Peponi isipokuwa kwa matendo yake na hakuna ambaye ataingia Motoni isipokuwa kwa matendo yake.

[1] 16:32

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 05/08/2021