60. Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar III


Nne: Kuhusu walioenda kinyume na Qadhwaa´ na Qadar. Kuna mapote mawili yaliyoenda kinyume na Qadhwaa´ na Qadar na yote mawili yanagongana:

La kwanza: Qadariyyah. Hawa ni wale wanaopinga Qadar. Wameitwa Qadariyyah. Mtu wa kwanza kusema hayo ni ´Amr bin ´Ubayd na Waaswil bin ´Atwaa’ na akaepuka katika kikao cha Hasan al-Baswriy. Qadariyyah ambao wanapinga Qadar ni Mu´tazilah. Wamesema kuwa mja mwenyewe ndiye anaumba matendo yake na kwamba mambo hayakukadiriwa na Allaah. Wamesema kuwa matendo ya waja wao wenyewe ndio wanafanya yapatikane. Wanasema kuwa Allaah hana lolote, si utashi wala matakwa, kuhusiana nayo. Ndio maana wakaitwa “Qadariyyah”. Hii ina maana kuwa mja ndiye anayeumba matendo yake mwenyewe. Kwa hali hii mtu anakuwa amethibitisha waumbaji wawili. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndiye muumbaji na kila kisichokuwa Yeye vimeumbwa. Wao wanapinga haya na kusema kuwa Allaah yuko pamoja Naye waumbaji wengine ambao ni wale waja wanaoumba matendo yao wenyewe. Huku ni kushirikisha katika uola. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaita:

“Waabudu moto wa Ummah huu.”[1]

Kwa sababu wamethibitisha kuwepo kwa waumbaji wawili kama walivyofanya waabudu moto. Waabudu moto wamesema kuwa kuna waumbaji wawili; nuru ambayo inaumba mambo mazuri na giza mambo ya shari. Qadariyyah wakawazidi ambapo wamesema kuwa kila mmoja anaumba matendo yake mwenyewe. Hivyo wakawa ni wenye kuthibitisha waumbaji wengi pamoja na Allaah (´Azza wa Jall). Huku ni kushirikisha katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

La pili: Jabriyyah. Hawa ni wafuasi wa Jahm bin Swafwaan. Wamesema kuwa mja hana khiyari wala matakwa yoyote. Wanaona kuwa ametenzwa nguvu kwa yale anayofanya pasi na yeye kuwa na khiyari. Wanasema ni kama chombo kilicho kwenye mikono ya yule mwenye kukiendesha. Ni kama upepo angani. Ni kama maiti kwenye mikono ya muoshaji. Wanaonelea kuwa mja ametenzwa nguvu katika matendo yake. Ni kama chombo chenye kuendeshwa.

Jabriyyah wamepindukia katika kuthibitisha utashi na matakwa ya Allaah na wakati huo huo wakapinga utashi na matakwa ya mja. Mu´tazilah wao ni kinyume wamepindukia katika kuthibitisha utashi na matakwa ya mja na wakati huo huo wakapinga utashi wa Allaah (´Azza wa Jall). Kila pote limoja katika hayo mawili yamekosea katika kitu kimoja:

Qadariyyah wamepindukia katika kuthibitisha utashi na matakwa ya mja mpaka wakafikia kusema kuwa amejitosheleza na Allaah na anaumba kila anachotaka.

Jabriyyah wamepindukia katika kuthibitisha utashi na matakwa ya Allaah mpaka hilo likawapelekea kupinga utashi na matakwa ya mja.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wamekaa kati na kati. Wamesema kuwa kila kitu kinakuwa kwa Qadhwaa´ na Qadar ya Allaah kukiwemo matendo ya waja. Yameumbwa na Allaah na wakati huo huo ni matendo ya waja walioyafanya kwa khiyari na kupenda kwao wenyewe. Waja wana utashi na khiyari ya kufanya jambo lakini hata hivyo hayakujitosheleza na Allaah, kama wanavyosema Qadariyyah, na hawakutenzwa nguvu, kama wanavyosema Jabriyyah. Bali wanafanya mambo kwa khiyari na utashi wao msafi. Kwa ajili hiyo ndio maana wanalipwa thawabu kwa kutenda kheri na wanaadhibiwa kwa kutenda shari. Si kwa jengine ni kwa sababu wamefanya kwa khiyari na kwa kupenda kwao wenyewe. Lau wangelikuwa wametenzwa nguvu hawaadhibiwi. Ni vipi wataadhibiwa kwa mambo ambayo hawana kwayo khiyari wala utashi? Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah (Jalla wa ´Alaa) hamchukulii mwendawazimu ambaye hana khiyari. Kadhalika hamchukulii ambaye katenzwa nguvu kwa sababu hana khiyari. Vilevile hamchukulii mwenye kulala ambaye hana kufikiria na wala hana akili. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kalamu imesimamishwa kutoka kwa watu watatu; mdogo mpaka abaleghe, mwendawazimu mpaka apate akili na mwenye kulala mpaka aamke.”[2]

Kwa nini? Kwa sababu watu hawa hawana utashi na matakwa. Kwa hiyo hawachukuliwi kwa muda ule ambao fahamu zao zimepotea na matakwa. Kuhusu yule ambaye ana utashi, matakwa na khiyari analipwa kwa kutenda jema na anaadhibiwa kwa kutenda maasi. Kwa sababu ametenda kwa khiyari na matakwa yake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ

 “Hakika wale walioamini na wakatenda mema.” (02:277)

Ameyanasibisha matendo kwao. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا

“Hakika wale waliokufuru.” (02:06)

Ameunasibisha ukafiri kwao kwa sababu ni kitendo walichokifanya kwa kutaka kwao. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ

“Na yule atakayemwasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto.” (72:23)

Ameyanasibisha maasi kwao kwa sababu ni kitendo chao.

Kwa mtazamo wa kitendo ni cha mja. Kwa mtazamo wa Qadar kimekadiriwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa hivyo inakuwa ni makadirio ya Allaah na wakati huo huo ni kitendo cha mja. Huku ndio kuoanisha baina ya maandiko. Dalili ya hilo maneno Yake (Ta´ala):

لِمَن شَاء مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاؤُونَ إِلَّا أَن يَشَاء اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule miongoni mwenu anayetaka anyooke. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:28-29)

Maneno Yake:

لِمَن شَاء مِنكُمْ

“Kwa yule miongoni mwenu anayetaka anyooke.”

Hapa wanaraddiwa Jabriyyah ambao wanapinga mja kuwa na utashi. Ni dalili inayofahamisha kuwa mja ananyooka kwa kupenda kwake. Kisha akasema:

وَمَا تَشَاؤُونَ إِلَّا أَن يَشَاء اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”

Hapa wanaraddiwa Qadariyyah ambao wanasema matakwa ya waja yamejitosheleza na kwamba mja anatenda kivyake. Aayah hii inaraddi mapote yote mawili na sambamba na hilo inathibitisha madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Mema na maasi yote mawili ni kitendo cha mja na wakati huo huo ni Qadhwaa´ na Qadar ya Allaah. Allaah amewakadiria navyo na wao wameyafanya kwa kupenda na kutaka kwao. Kwa ajili hiyo mtu mwenye akili anaweza kufanya, anaweza kuacha, anaweza kuamka na kuswali, anaweza kutoa swadaqah na anaweza kupigana Jihaad katika njia ya Allaah. Kadhalika anaweza kuacha swalah, anaweza kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu na anaweza kuacha kupigana Jihaad katika njia ya Allaah. Anaweza akayaacha yote haya kwa kupenda na kutaka kwake. Anaweza kufanya kama ambavyo vilevile anaweza kuacha. Anaenda kuzini, kunywa pombe na kula ribaa kwa khiyari yake mwenyewe. Anaweza kuacha kula ribaa, kuzini na mambo mengine ya haramu. Anafanya yote haya kwa khiyari na kupenda kwake mwenyewe. Hakuna asiyejua haya.

[1] Abu Daawuud (3691), at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” (03/65) na wengineo

[2] Ibn Maajah (2045), Ibn Hibbaan (143)  na wengineo