60. Radd juu ya utata wa tano: kuna tofauti kati ya mwenye kuliomba sanamu na Mtume au mja mwema

Akisema: “Simshirikishi Allaah na chengine chochote, kamwe, lakini kuwaelekea watu wema sio shirki”. Mwambie: “Ukiwa kweli unakubali ya kwamba Allaah ameharamisha shirki na kwamba ni jambo kubwa kuliko zinaa na unakubali ya kwamba Allaah hatoisamehe, ni jambo gani sasa ambalo Allaah kaharamisha na kusema kwamba hatolisamehe?” Kwa hakika hajui. Mwambie: “Vipi utajitakasa nafsi yako na shirki na wewe huijui? Au vipi Allaah atakuharamishia wewe hili na kutaja ya kwamba hatolisamehe, wakati wewe huliulizii na wala hulijui? Wafikiria ya kwamba Allaah atatuharamishia na wala asitubainishie?” Akisema: “Shirki ni kuabudu masanamu, na sisi hatuabudu masanamu” Mwambie: “Na nini maana ya kuabudu masanamu? Unafikiria ya kwamba walikuwa wakiamini kuwa miti ile na mawe yale yanaumba na yanaruzuku na yanaendesha mambo kwa yule anayeviomba? Hili linakadhibishwa na Qur-aan!”

Akisema: “Ni yule mwenye kuuelekea mti, jiwe au pango lililojengwa kwenye kaburi n.k, anakiomba, kukichinjia na kusema: “Kinatukurubisha kwa Allaah na Allaah anatulinda [na madhara] kwa baraka zake na anatupa kwa baraka zake” Mwambie: “Umesema kweli. Na hichi ndio kitendo chenu kwenye makaburi na majengo yaliyo kwenye makaburi na mengineyo.”

Hili amelikubali ya kwamba kitendo chao hichi ni kuabudu masanamu na ndio jambo lililokuwa linatakikana. Mtu anaweza kumwambia pia: “Kuhusu maneno yako, kwamba shirki ni kuabudu (tu) masanamu, je unamaanisha ya kwamba shirki ni hili tu, na kwamba kuwategemea watu wema na kuwaomba hayaingii katika hiyo [shirki]?” Anaraddiwa[1] na yale aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake kuhusu kukufuru kwa yule ambaye kamtegemea Malaika, ´Iysa na watu wema. Lazima akukubalie ya kwamba mwenye kumshirikisha katika ´Ibaadah ya Allaah miongoni kwa watu wema, ndio shirki iliyotajwa katika Qur-aan, na ndilo lililokuwa linatakikana.

Siri ya mambo ni kwamba akisema: “Mimi simshirikishi Allaah”. Mwambie: “Nieleze, ni nini kumshirikisha Allaah?” Akisema: “Ni kuabudu masanamu” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kuabudu masanamu?” Akisema: “Mimi siabudu isipokuwa Allaah pekee” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kumuabudu Allaah pekee?” Akikueleza kama ilivyoeleza Qur-aan, ndio kinachotakikana. Na ikiwa hajui, vipi atadai kitu na yeye hakijui?

Na akikubainishia kinyume na maana yake, mbainishie Aayah zilizo za wazi za maana ya kumshirikisha Allaah na kuabudu masanamu na kwamba ndio yale yale wayafanyayo leo, na kwamba kumuabudu Allaah pekee hali ya kuwa hana mshirika, ndio yale wanayotupinga kwayo na kutupigia kelele, kama walivyokuwa wakipiga kelele ndugu zao pale waliposeama:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya miungu wote kuwa ni mungu mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno.” (Swaad 38 : 05)

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) anabainisha kuwa shirki haikukomeka na kuyaabudu masanamu peke yake. Kwa kuwa washirikina wa kale kuna waliokuwa wakiwaabudu Malaika ambao ndio viumbe wema kabisa:

بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ وَمَن يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلَـٰهٌ مِّن دُونِهِ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ

“Bali [hao Malaika] ni waja waliokirimiwa; hawamtangulii kwa neno nao kwa amri Yake wanaitekeleza. Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawamuombei uombezi isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia – nao kutokana na kumkhofu ni wenye kutahadhari. Yeyote yule miongoni mwao atakayesema: “Mimi ni mungu mwabudiwa badala Yake”, basi huyo Tutamlipa [Moto wa] Jahannam. Hivyo ndivyo Tunavyowalipa madhalimu.” (21:26-29)

Kuna ambao walikuwa wakiwaabudu watu wema. Amesema (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza, na wanataraji Rahmah Yake na wanakhofu Adhabu Yake.” (17:57)

Imesemekana imeteremka juu ya wale wanaomuabudu mja aitwaye ´Uzayr na Mtume al-Masiyh.

Imesemekana vilevile kuwa imeteremka juu ya wale watu waliokuwa wakiabudu majini ambapo wale majini wakasilimu na wale watu waliokuwa wakiyaabudu hawakujua kuwa majini hayo yamesilimu.

Kinacholengwa ni kwamba Allaah ametaja kuwa washirikina wa mwanzo kuna miongoni mwao waliokuwa wakiabudu masanamu, miti na mawe. Kuna wengine walikuwa wakiwaabudu Mitume na waja wema. Hata hivyo akawasawazisha katika hukumu na akawahukumu wote kufuru na shirki. Wewe mtu wa utata! Ni vipi utataka kutofautisha kati ya mwenye kuabudu sanamu na mja mwema? Je, unataka kutenganisha kati ya vitu ambavyo Allaah amevijumuisha? Huku ni kupingana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivi ndivyo inavyoraddiwa shubuha hii. Kwa vile imebaini kwamba hapana tofauti kati ya shirki ya wale wa kale na shirki ya watu hawa ambao wanaodai Uislamu ilihali wanaabudu makaburi, mawalii na waja wema kwa kuwa eti hawakujua kuwa wayafanyayo ni shirki. Hii ndio natija ya kujahili ´Aqiydah ya Tawhiyd sahihi na kutokujua shirki inayopingana nayo. Asiyeitambua shari hutumbukia ndani yake ilihali si mwenye kujua. Kuanzia hapa inapata kuwa wazi ule udharurah wa kutilia ´Aqiydah sahihi umuhimu mkubwa na yale yanayopingana nayo.

[1] Anajibiwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 90
  • Imechapishwa: 24/01/2017