1 – Ni wajibu kwa mwenye busara kuwa na muruwa ili awe na sifa nzuri kadri na anavoweza na kuepuka sifa mbaya kadri na anavoweza.

2 – Sijapatapo kumuona mtu aliyekula hasara pakubwa na mpumbavu na mjinga mkubwa kama yule ambaye anajifakharisha kwa sifa nzuri za mababu zao watukufu ingawa wao wenyewe hawanazo.

3 – al-Hasan al-Baswriy amesema:

“Hakuna dini pasi na muruwa.”

4 – Baadhi wamesema kuwa muruwa ni kule kuwapa chakula ndugu zake baba, kurekebisha mali yake na kukaa kwenye mlango wa nyumba yake.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kuwa na inswafu kwa yule aliye chini yako, kumtukuza yule aliye juu yako na kumzawadia zawadi sawa na kile yeye alichokupa.

Baadhi ya wengine wakasema muruwa ni kuikubali haki na kuwaangalia wageni.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kuzungumza ukweli, kusubiri juu ya maudhi ya jirani, kuwatendea wema wenzako na kutowaudhi watu na majirani.

Wako wengine ambao wamesema kuwa muruwa ni kutokuwa na tabia mbaya.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kule kutoa na kuwa na tabia njema.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kule kujizuia na kufanya kazi; kujizuia na yale yote aliyoharamisha Allaah na akafanyia kazi yale aliyohalalisha Allaah.

Wengine wakasema muruwa ni kule mtu kushukuru pale anapopewa, kusubiri pale anapopewa mtihani, kusamehe ilihali mtu yuko na uwezo na kutimiza ahadi wakati mtu anapoahidi.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kule kuwa mpole juu ya mambo na mwerevu.

Baadhi ya wengine wakasema kuwa muruwa ni mtu kujiepusha na yale yote yenye kutia mashaka, kwa sababu mtu akiwa mwenye kutiliwa mashaka basi hawi mtukufu, kutengeneza mali yake, kwa sababu fakiri hana muruwa, na kuihudumia familia yake, kwa sababu yule ambaye familia yake inawahitajia wengine hawi mtukufu.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni usafi na kunukia harufu nzuri.

Baadhi ya wengine wakasema kuwa muruwa ni ule ufaswaha na kusamehe.

Wengine wakasema kuwa muruwa ni kule kuchunga maagano na kuheshimu mikataba.

Baadhi ya wengine wakasema kuwa muruwa ni kule kutania na kutabasamu.

5 – Wametofautiana juu ya muruwa, lakini maana ya yote waliyoyasema ni yenye kukaribiana.

6 – Muruwa kwa vile ninavoona mimi ni kuyaepuka yale yote anayoyachukia Allaah na waislamu na kufanya yale yote ambayo Allaah anayapenda na waislamu.

7 – Ibn Siyriyn amesema:

“Mambo matatu sio katika muruwa; kula masokoni, kujitia manukato kwa muuzaji manukato na kujitazama kwenye kio cha anayefanya chuku.”

8 – ash-Sha´biy amesema:

“Sio katika muruwa kujitazama kwenye kio cha anayefanya chuku.”

9 – Abu Qilaabah amesema:

“Sio katika muruwa mtu kuchuma faida kutoka katika mali ya rafiki yake.”

10 – Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan amesema:

“Ugonjwa wa muruwa ni kuwa na marafiki wabaya.”

11 – Shariyk amesema:

“Udhalilishaji wa dunia unapatikana katika mambo matano: kuingia katika bafu za nje kabla ya alfajiri bila kuwa na ndoo, kuvuka mahali pa watembeaji kwa miguu bila ya kipande, kuhudhuria kikao cha elimu bila ya daftari, mtukufu kumuhitajia mtu wa chini yake na mtu kumuhitajia mwanamke wake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 229-234
  • Imechapishwa: 29/08/2021