Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Ibn ´Umar iko mikononi Mwake! Lau mtu mmoja atakuwa na dhahabu mfano wa mlima wa Uhud kisha akazitoa katika njia ya Allaah hatomkubalia Allaah kutoka kwake mpaka aamini Qadar.”

Kisha akatolea dalili kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake.”[1]

Ameipokea Muslim.

2- ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anhu) alisema kumwambia mwanawe:

“Ee mwanangu! Hakika hutopata ladha ya imani mpaka kwanza ujue kuwa yaliyokufika hayakuwa yakukukosa na yaliyokukosa hayakuwa yakukufika. Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Ee Mola Wangu! Niandike nini?” Akasema: “Andika makadirio ya kila kitu mpaka kitaposimama Qiyaamah.” Ee mwanangu! Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa salla) akisema: “Yule atakayekufa akiamini kinyume na hivi, basi huyo si katika mimi.”[2]

Katika upokezi wa Ahmad imekuja:

“Hakika kitu cha kwanza alichoumba Allaah (Ta´ala) ilikuwa ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Basi tokea hapo kukapangwa kila kitu kitachokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.”[3]

Ibn Wahb amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Yeyote ambaye haamini Qadar, kheri na shari yake, Allaah atamchoma kwa Moto.”

Imepokelewa katika “al-Musnad” Ahmad na tungo za Sunan kutoka kwa Ibn-ud-Daylamiy ambaye amesema:

“Nilimwendea Ka´b-ul-Ahbaar na kumwambia: “Katika nafsi yangu kuna kitu kuhusu Qadar. Tafadhali nieleze juu ya kitu pengine Allaah akakiondosha moyoni mwangu.” Akasema: “Lau utatoa dhahabu mfano wa sawa na mlima wa Uhud, basi Allaah hatozikubali kutoka kwako mpaka uamini Qadar, ujue ya kwamba yaliyokupata hayakuwa yenye kukukosa na yaliyokukosa hayakuwa yenye kukupata. Iwapo utakufa ukiwa na imani kinyume na hii utakuwa mmoja katika watu wa Motoni.” Nikamwendea ´Abdullaah bin Mas´uud, Hudhayfah bin al-Yamaan na Zayd bin Thaabit na wote wakanieleza kwa mfano wa hayo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[4]

Hadiyth ni Swahiyh kaipokea al-Haakim katika “as-Swahiyh” yake.

MAELEZO

Pale ilipokuwa kuamini Qadar ni miongoni mwa misingi ya imani ndipo mwandishi akaweka mlango huu. Kuamini Qadar ni miongoni mwa mambo yanayopelekea katika Tawhiyd na yanapinga kufuru. Mlango huu ndani yake kuna makemeo na matahadharisho makali kwa yule anayepinga na kukadhibisha Qadar.

Waislamu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa ni wenye kuamini Qadar na ni wenye kujisalimisha kwa Allaah. Mwishoni mwa zama za Maswahabah ndipo kukazuka kikundi kinachopinga Qadar na wakasema kuwa Allaah hajui yanayopitika kabla ya kutokea kwake. Wakadai kwamba kuthibitisha Qadar kunapingana na uadilifu. Ni vipi mambo yatapangwa hapo kabla kisha aadhibiwe mtenda maasi na kafiri kwa waliyoyafanya? Fikira zao zinatokamana na ujinga, upotevu na kutatizika kwao na mambo.

Ahl-ul-Haqq katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ahl-ul-Sunnah wal-Jamaa´ah waliofuata mwenendo wao waliamini na wakadhibitisha Qadar. Wanaonelea kuwa Allaah amekadiria mambo na akayaandika na kwamba hakuna kinachotokea isipokuwa kwa matakwa Yake. Kila kitu kimeshakadiriwa, kila kitu kimeshadhibitiwa na ni Mwenye kutambua kila kitu. Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Jadiliana nao juu ya elimu. Wakiithibitisha, basi wameshindwa, na wakiikanusha, wanakufuru.”

Maana yake ni kwamba wanatakiwa kuulizwa kama Allaah anayajua mambo kabla ya kutokea kwake au hayajui. Wakikubali, basi hiyo ndio Qadar. Wakipinga na wakasema kuwa Allaah hayajui yatayotokea, wanakufuru kwa sababu katika hali hii watakuwa wamemsifu Allaah kuwa na ujinga na upotevu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah ni mjuzi wa kila kitu.” (al-Anfaal 08:75)

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”[Haya yote] ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni muweza na kwamba Allaah amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi.” (at-Twalaaq 65:12)

Mwenye kumnasibishia Allaah ujinga na kwamba hayajui mambo basi kwa hakika atakuwa ametukana ishara za Allaah na amemponda kikwelikweli na kwa ajili hiyo anakuwa kafiri. Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni wengi wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameonelea kuwa Qadariyyah ni makafiri. Kwa sababu wamekadhibisha Qadar ya Allaah, wamepinga ujuzi Wake, wamezikadhibisha dalili zote hizi na wamemnasibishia Allaah ujinga. Imesihi kupitia kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake.”

Hayo yamefahamishwa pia na Qur-aan. Allaah (Subhaanah) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (al-Hadiyd 57:22)

Kwa ajili hii ndio maana Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Ibn ´Umar iko mikononi Mwake! Lau mtu mmoja atakuwa na dhahabu mfano wa mlima wa Uhud kisha akazitoa katika njia ya Allaah hatomkubalia Allaah kutoka kwake mpaka aamini Qadar.”

Vivyo hivyo yamesemwa na Zayd bin Thaabit, Ubayy bin Ka´b, ´Abdullaah bin Mas´uud na wengineo. Hivyo pia ndivo wanavosema Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni wajibu kwa kila muislamu kuamini Qadar.

Kuamini Qadar kumekusanya mambo mane:

1- Allaah anakijua kila kitu.

2- Akakiandika.

3- Amekiumba kila kitu na amekadiria kila kitu.

4- Anachotaka Allaah huwa na asichotaka Allaah hakiwi.

Mwenye kuamini mambo haya mane basi anaamini Qadar. Mwenye kukadhibisha moja katika mambo hayo amekadhibisha kitu katika Qadar.

2- ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anhu) alisema kumwambia mwanawe:

“Ee mwanangu! Hakika hutopata ladha ya imani mpaka kwanza ujue kuwa yaliyokufika hayakuwa yakukukosa na yaliyokukosa hayakuwa yakukufika. Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Ee Mola Wangu! Niandike nini?” Akasema: “Andika makadirio ya kila kitu mpaka kitaposimama Qiyaamah.” Ee mwanangu! Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa salla) akisema: “Yule atakayekufa akiamini kinyume na hivi, basi huyo si katika mimi.”

Bi maana hutohisi utulivu, raha na utamu wa imani isipokuwa mpaka uamini kwamba yaliyokufika hayakuwa yakukukosa na yaliyokukosa hayakuwa yakukufika. Huku ndio kuamini Qadar. Akiamini namna hii basi moyo wake utakunjuka na atafanyia kazi Shari´ah ya Allaah. Mtu kama huyu afanye yale anayotakiwa kufanya na huku moyo wake umetulizana kwa sababu anatambua hakuna kitachomfika isipokuwa kile alichomwandikia Allaah. Tafsiri hii ya baadhi ya mambo ya Qadar imekusanya Qadar nzima.

Kadhalika walisema Maswahabah kumwambia ´Abdullaah bin Fayruuz ad-Daylamiy ambaye ni Taabiy´ anayetambulika. Alipowauliza walimwambia kwamba Allaah hakubali chochote kutoka kwake mpaka aamini Qadar. Vinginevyo matendo yake ni yenye kuporomoka. Ni dalili inayoonyesha kuwa walimaanisha kwamba anakufuru kwa hilo. Kwa sababu Allaah amesema:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha basi pasi na shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.” (al-An´aam 06:88)

Ambaye matendo yake na swadaqah zake hazikubaliwi ni kafiri ambaye imani yake haijahakikika. Mwenye kukanusha Qadar basi amepinga moja ya nguzo za imani na kwa hivyo matendo yake yote yanaporomoka. Muslim amepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Awf kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa salla) amesema:

“Allaah amekadiria makadirio ya viumbe kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka khamsini na wakati huo ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[5]

Kila kitu kimeshakadiriwa na kupangwa kwa mujibu wa ujuzi na uandishi wa Allaah. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Muumbaji mwenye kuyaendesha mambo kwa mujibu wa makadirio Yake. Hii ndio haki na ndio mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Yule mwenye kuyaamini haya ndiye kapatia na yule mwenye kwenda kinyume na haya amepondoka kutoka katika haki.

[1] Muslim (8).

[2] Abu Daawuud (4700). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (111).

[3] Ahmad (22757) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (2017).

[4] Abu Daawuud (4699), Ibn Maajah (77), Ahmad (21629) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (4940). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (62).

[5] Muslim (2653).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 165-167
  • Imechapishwa: 14/11/2018