Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Unafiki ni ukafiri na maana yake ni kumkufuru Allaah, kumuabudu mwengine asiyekuwa Yeye na wakati huohuo mtu akaonyesha Uislamu waziwazi. Hivyo ndivyo walivyofanya wanafiki wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

MAELEZO

Unafiki ni kuonyesha Uislamu na kuficha ukafiri, ni mamoja mtu akamuabudu mwengine asiyekuwa Allaah au asifanye hivo. Huenda zandiki kama vile mkomunisti akawa hamuabudu si Allaah wala mwengine. Yule anayeonyesha Uislamu na kuficha ukafiri ni mnafiki. Ni mamoja anamuabudu mwengine asiyekuwa Allaah au hafanyi hivo. Maana ya mnafiki kama tulivyosema ni yule anayeonyesha Uislamu kwa unafiki, uongo, taqiyyah na anaficha ukafiri.

Watu wengi wanasema kuwa ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ilihali ukweli wa mambo ni watu wa Bid´ah. Kwa undani kabisa yuko na Bid´ah na huku anaonyesha na kusema kuwa ni katika Ahl-us-Sunnah. Huu ni unafiki. Wanawasapoti Ahl-ul-Bid´ah na wanaonelea Bid´ah na wanasema kuwa ni Ahl-us-Sunnah. Alama ni kuwa wamesimama katika upande wa Ahl-ul-Bid´ah na wanabuni mifumo kwa lengo la kuwatetea.

Sisi tunawataka vijana wenye busara na akili wanaopenda tu kwa ajili ya Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini na khaswa khaswa Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tukiona kasoro katika mapenzi haya tunatambua kuwa kuna kasoro katika ´Aqiydah. Kasoro hii ni ya khatari na ni khasara kubwa.

Mnafiki anaonyesha Uislamu na anaficha ukafiri. Anaonyesha Uislamu waziwazi. Hivyo ndivyo walivyofanya wanafiki wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anasema kuwa baadhi ya watu wanafikiria kuwa unafiki ulikuwepo tu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha baadaye ukatoweka. Hili ni kosa. Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Unafiki hivi sasa ni mbaya zaidi kuliko katika kipindi cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Alipoulizwa sababu ya kusema hivo akasema: “Wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanafiki walikuwa wakificha unafiki wao. Ama leo wanaonyesha unafiki wao waziwazi.”

Leo unafiki umekuwa ni jambo la kawaida na khaswa katika harakati za kisiasa. Baadhi yao wamelishuhudia wenyewe. Kuna waliosema:

“Simjui mwanasiasa yeyote asiyedanganya.”

Wengine wakasema:

“Siasa ni unafiki.”

Wanasiasa wengi katika mapote ya kisiasa wana unafiki wa kimatendo. Moja katika alama ya unafiki huu ni kusimama upande wa Ahl-ul-Bid´ah na kutunga mifumo ya khatari kwa ajili ya kupambana na kuwasaga Ahl-us-Sunnah. Kama mfano wa mfumo wa haki sawa (Manhaj-ul-Muwaazanah), kuzungumzia mfumo mpana unaoenea Ummah mzima na misingi mingine iliyowekwa kwa ajili ya kuwapiga vita Ahl-us-Sunnah na kuwatetea Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 437-438
  • Imechapishwa: 28/12/2017