17- Abu Daawuud amepokea kupitia kwa ´Awf bin Maalik ambaye amesema:

“Tulikuwa wasaba, wanane au kumi kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akasema: “Je, hamumpi kiapo cha usikivu na utiifu [bay´ah] Mtume wa Allaah?” Na tulikuwa karibuni tumetoka kumpa kiapo cha usikivu na utiifu na kusema: “Tumekupa kiapo cha usikivu na utiifu.” Akasema vivyo hivyo mara tatu. Tukanyoosha mikono yetu na kutoa kiapo cha usikivu na utiivu. Mtu mmoja akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tumekupa kiapo cha usikivu na utiifu, tumekupa kiapo cha usikivu na utiifu kwa chepi?” Akasema: “Kumuabudu Allaah na kutomshirikisha Yeye na chochote, kuswali vipindi vitano na kusikiliza na kutii.” Kisha akasema kimya kimya: “Na kutowaomba watu kitu.”Kuna watu fimbo ilikuwa inaweza kuwaponyoka na hawamuombi yeyote awape nayo.”[1]

18- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema:

Kumuahidi kwao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kiapo cha usikivu na utiifu kutomuomba yeyote chochote ni tabia njema. Hivyo mtu anakuwa ni mwenye kuepuka huduma za watu kuwa katika dhamira yake. Hadiyth inafunza pia mtu awe ni mwenye subira wakati wa haja na kuwatowategemea watu. Pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaamrisha hilo wakashikamana bara bara na kila nyanja na kila hali hata hali isiyoweza kuingia akilini. Walifanya hivo kwa lengo la kuzuia njia na Allaah ndiye Anajua zaidi.

19- Imepokelewa jinsi Abu Hamzah al-Khuraasaaniy – ambaye alikuwa ni mmoja katika wafanya ´ibaadah wakubwa – alifikiwa na khabari ya kundi la Maswahabah lililompa kiapo cha usikivu na utiifu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kutomuomba yeyote chochote. Akasema: “Ee Mola! Watu hawa wamempa kiapo cha usikivu na utiifu Mtume Wako kwa sababu wamemuona. Ninakuahidi Wewe kuwa sintomuomba yeyote chochote.” Akatoka Shaam na kwenda kuhiji. Usiku mmoja wakati alipokuwa anatembea akatengana na marafiki zake. Akawakimbilia. Pindi alipokuwa anawaendea akatumbukia kwenye kisima kando ya barabara. Alipokuwa chini akasema: “Hebu niite mtu anisaidie.” Kisha akajiambia mwenyewe: “Yule ambaye nimemuahidi ananiona na kunisikia. Ninaapa kwa Allaah sintosema herufi hata moja kumwambia mtu.” Hakukupita muda mrefu kundi la watu likapita kwenye kisima kile na kusema: “Kisima hiki kinatakiwa kuzibwa tena.” Wakakiweka vibao na kukiziba na udongo. Wakati Abu Hamzah alipoona hilo akasema: “Huku ndio kuangamia.” Alipotaka tu kuwaomba msaada akasema: “Ninaapa kwa Allaah sintotoka nje.” Kisha akajiambia mwenyewe: “Wewe siumemuahidi Yule mwenye kukuona?” Akanyamaza na kumtegemea Allaah. Akarudi kushegama na kuanza kufikiri. Ghafla udongo ukaanza kumwangukia na vibao vinatolewa. Akasikia sauti ya mwenye kusema: “Nipe mkono wako.” Akasema: “Nikampa mkono wangu. Mara moja nikajikuta kando. Nikatoka kwenye kisima na sikumwona yeyote. Ndipo nikasikia mwenye kuita: “Vipi umeona matunda ya kutegemea?”[2]

20- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wametofautiana juu ya kunyamaza kwa mtu huyu wakati alipokuwa katika hali ngumu hii kisimani:

1- Kuna wenye kusema kuwa mtu huyu alimpa ahadi Allaah. Hivyo ni wajibu kutimiza ahadi kwa njia kamilifu. Fanyeni kama alivofanya mtu huyu na hivyo mtakuja kuongozwa – Allaah akitaka.

2- Wengine wanasema kunyamaza kwake katika hali kama hii kunamdhuru, na hilo halijuzu. Lau angelielewa maana ya kutegemea basi angelitambua kuwa kutaka msaada katika hali kama hiyo haipingani na kutegemea. Kama jinsi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukosa kutegemea wakati alipotoka Makkah kwa kujificha, akataka msaada wa uelekezwaji na akajificha pangoni mpaka hali ilipotulia. Utegemeaji wenye kusifiwa haufikiwi kwa makatazo. Kunyamaza kwa mtu huyu katika hali kama hii kumekatazwa.

Allaah amemruzuku mwanaadamu vitu vyenye kumlinda na madhara na kumletea manufaa. Yule mwenye kuacha kuvitumia kwa kumtegemea Allaah basi hajui ni nini maana ya kutegemea. Isitoshe anatupilia mbali hekima ya Allaah (Ta´ala). Kwa sababu kutegemea maana yake ni kuufungamanisha moyo na Allaah. Kutegemea haina maana ya kupuuzia sababu. Lau mtu atapigwa na njaa na akaacha kuomba mpaka akafa anaingia Motoni, kama alivosema Sufyaan ath-Thawriy na wengine. Kwa sababu Allaah amekuelekeza namna ya kujisalimisha. Ukiyapuuzia hiyo ina maana kwamba umejisababishia kujiua mwenyewe.

Maneno ya Abu Hamzah “Nikasikia sauti ikisema: “Nipe mkono wako.” inaweza kuwa ni kwa bahati mbaya na inaweza kuwa vilevile ni kutokana na upole wa Allaah kwa mja Wake mjinga. Haipingwi ya kwamba Allaah (Ta´ala) alikuwa ni mpole kwake. Kinachokataliwa ni kitendo chake ambapo anajisababishia kujiua mwenyewe. Allaah amemuazima uhai ambao amemuamrisha kuuhifadhi.

[1] Muslim (1043), Abu Daawuud (1642), an-Nasaa’iy (1/228) na Ibn Maajah (2867).

[2] Tazama “Taarikh Baghdaad” (01/391).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 18/03/2017