Tarawiyh ni swalah ya usiku inayoswaliwa kwa mkusanyiko, Jamaa´ah katika Ramadhaan. Wakati wake unaanza baada ya ´Ishaa mpaka alfajiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishaji´isha kusimama usiku katika Ramadhaan na kusema:

“Yule mwenye kusimama kuswali nyusiku za Ramadhaan kwa imani na matarajio basi atasamehewa madhambi yaliyotangulia.”[1]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali pamoja na watu nyusiku mbili za mwanzo na kwamba kulikuja watu wengi katika kila swalah. Usiku wa tatu au wa nne akaacha kwenda msikitini. Asubuhi ilipofika akasema:

“Niliona nini mlichofanya jana usiku. Hakuna kilichonizuia mimi kuwajia isipokuwa nilikhofia isije ikafaradhishwa kwenu.”[2]

Ilikuwa ni katika Ramadhaan.

Sunnah ni kuswali Rakaa kumi na moja. Kila baada ya Rakaa mbili kutolewe Tasliym. Wakati ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alipoulizwa kuhusu swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anazidisha katika Ramadhaan wala nje ya Ramadhaan Rakaa kumi na moja.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika “al-Muwattwa´”  kumepokelewa kutoka kwa Muhammad bin Yuusuf (ambaye alikuwa ni mwaminifu na thabiti), kutoka kwa Swahabah as-Saaib  bin Yaziyd ya kwamba ´Umar bin al-Khattwaab alimwamrisha ´Ubayy bin Ka´b na Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anhum) kuwaswalisha watu Rakaa kumi na moja[4].

Pamoja na hivyo hakuna neno kukiswaliwa zaidi ya Rakaa kumi na moja. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya swalah ya usiku akasema:

“Swalah ya usiku ni mbili mbili. Mmoja wenu akichelea kuingiliwa na asubuhi aswali Rakaa moja ambayo ni Witr ya yale aliyoswali.”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hata hivyo bora na ukamilifu zaidi ni kuswali ile idadi iliyotajwa katika Sunnah, kuswali kwa utaratibu na kurefusha bila ya kuwatia watu uzito.

Uvukaji mipaka wa leo wa kudokoa swalah unaofanywa na baadhi ya watu ni jambo linaloenda kinyume na Shari´ah. Isitoshe swalah sio sahihi ikiwa itapelekea kubatilisha mambo ya wajibu ya swalah au nguzo. Ni maimamu wachache wenye kufanya utaratibu katika Tarawiyh. Hili ni kosa. Imamu haswali peke yake, anawaswalisha wengine pia. Yeye ni kama mtawala ambaye anatakiwa kuangalia maslahi ya watu. Wanachuoni wamesema kuwa imechukizwa kwa imamu kuswali mbio mbio kiasi cha kwamba maimamu hawawahi kufanya yale ya wajibu.

Watu wanatakiwa kudhibiti Tarawiyh na wasiikose kwa kutoka kwenye msikiti huu na kwenda kwenye mwingine. Yule mwenye kuswali pamoja na imamu mpaka akamaliza naye basi anaandikiwa kama ameswali usiku mzima hata kama ataenda na kujilalia baada ya hapo.

Ikiwa hakukhofiwi fitina yoyote ni sawa pia kwa wanawake kuswali Tarawiyh msikitini. Kwa sharti wawe wametoka hali ya kuwa wamevaa mavazi ya kujiheshimu na wasijitie manukato.

[1] al-Bukhaariy (2009).

[2] al-Bukhaariy (2012) na Muslim (761).

[3] al-Bukhaariy (1138) na Muslim (764).

[4] Maalik (1/110).

[5] al-Bukhaariy (990) na Muslim (749).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 05/06/2017