Wakati Allaah (Ta´ala) alipotaka kuwarehemu na kuwatukuza waja kwa kumtuma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa walimwengu Akamfanya akawa ni kutafuta upweke. Hivyo akawa ni mwenye kuabudu kwenye pango la Hiraa´. Hivyo ndivyo wafanya ´ibaadah walivyokuwa wakifanya katika zama hizo, kama alivyotaja Abu Twaalib katika shairi lake linaloitwa “al-Laamiyyah”.

Haki ikamshangaza pindi alipokuwa Hiraa´. Ilikuwa katika Ramadhaan. Alikuwa na miaka arubaini. Akashangazwa na Malaika aliyemjia na kumwambia: “Soma.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Sijui kusoma.” Malaika akamtikisa mpaka akapata shida. Akamwacha na kumwambia tena: “Soma.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Mimi sijui kusoma.” Alifanya hivo mara tatu. Kisha akasema:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ

“Soma kwa Jina la Mola wako Aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kutokana na pande la damu linaloning’inia. Soma na Mola wako ni Mkarimu kabisa. Ambaye Aliyefunza kwa kalamu. Amemfunza mwanaadamu yale asiyoyajua.” (96:01-05)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akarudi nyumbani akitetemeka. Akamweleza Khadiydah (Radhiya Allaahu ´anhaa) yaliyopitika na kusema:

“Ninakhofia akili yangu.” Akamtuliza na kumwambia: “Bishara njema! Ninaapa kwa Allaah ya kwamba hatokufedhehesha. Kwani hakika wewe unaunga kizazi, unasema kweli, unamwangalia dhaifu na ni mwenye kusimama nyuma ya haki.”

Akamtajia sifa nzuri ambazo ilikuwa ni katika tabia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuonesha kuwa anamwamini, kumtuliza na kumsaidia katika haki. Yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumwamini. Allaah amuwie radhi na akumtukuze.

Kisha kukapita muda ambao Allaah alitaka upite pasi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuona kitu. Wahyi ukakatika ambapo akataka kujitupa chini kutoka kwenye mlima. Kilichomfanya hivo ilikuwa ni hamu na ladha aliyoipata kwa Wahyi wa Allaah. Imesemekana vilevile ya kwamba Wahyi ulikatika kwa muda wa miaka miwili au zaidi. Baada ya hapo akateremshiwa Malaika. Alikuwa amekaa kwenye kiti kati ya mbingu na ardhi. Akamtuliza na kumweleza kuwa yeye ni Mtume wa Allaah wa kweli. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona Malaika asikia woga na akaenda kwa Khadiyjah na kumwambia: “Nifunike! Nigubike!” Ndipo Allaah akamteremshia:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

”Ee uliyejigubika, simama na uonye! Na Mola wako mtukuze. Na nguo zako zitwaharishe.” (74:01-04)

Kipindi cha kwanza ilikuwa ni kipindi cha utume na kupokea Wahyi. Halafu Allaah katika Aayah hii akamuamrisha kuwaonya watu wake na awalinganie katika dini ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachukua jukumu kikamilifu na akamtii Allaah kwa njia kamilifu kabisa. Akawalingania katika dini ya Allaah (Subhaanah) wazee na wadogo, aliye huru na mtumwa, wanaume na wanawake, weusi na wekundu. Waja wa Allaah kutoka kila kabila wakamuitikia. Wa kwanza wao alikuwa ni Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Alikuwa akiitwa ´Abdullaah bin ´Uthmaan at-Taymiy. Akampa nusura katika dini ya Allaah. Akalingania pamoja naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa elimu na baswiyrah. Miongoni mwa ambao walisilimu kuingia katika Uislamu kupitia kwa Abu Bakr ilikuwa ni ´Uthmaan bin ´Affaan, Twalhah na Sa´d bin Abiy Waqqaas.

Kuhusu ´Aliy, alikuwa bado ni mdogo wakati alipoingia katika Uislamu. Yasemekana alikuwa na miaka nane. Imesemekana pia kuwa alikuwa na zaidi ya hivyo. Imesemekena pia ya kwamba aliingia katika Uislamu kabla ya Abu Bakr. Imesemekana vilevile ya kwamba sivyo. Kwa hali yoyote ile kuingia kwake katika Uislamu hakukuwa kama alivyoingia Abu Bakr kwa sababu alikuwa akiishi pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimchukua kutoka kwa ami yake ili kumsaidia. Kadhalika akasilimu Khadiyjah na Zayd bin al-Haarithah.

Padiri Waraqah bin Nawfal pia akaingia katika Uislamu. Akasadikisha Wahyi ambao umekuja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akatamani angelikuwa kijana. Ilipitika mwanzoni wakati kulipoteremka Wahyi. at-Tirmidhiy amepokea kuwa alimuota Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba alikuwa katika muonekano mzuri[1]. Hadiyth nyingine inasema:

“Nimemuona padiri akiwa kwenye nguo nyeupe.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Khadiyjah alienda na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamueleza aliyoyaona kwa Jibriyl (´alayhis-Salaam). Ndipo Waraqah bin Nawfal akasema:

“Hii ni Naamuus aliyokuja nayo Muusa bin ´Imraan.”

Wale ambao Allaah amezifungua nyoyo zao kwa Uislamu wakaingia katika Uislamu kutokana na nuru, baswiyrah na uwazi. Ikapelekea washirikina wa Makkah wakawatia kwenye matatizo na mateso. Allaah akamhifadhi na kumlinda Mtume Wake kupitia kwa ami yake Abu Twaalib. Abu Twaalib alikuwa ni mtu sharifu na mwenye kutiiwa kati yao. Walikuwa hawathubutu kumsibu kwa kitu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wanajua ni kiasi gani anavyompenda. Kwa hekima Yake Allaah akamwacha akafa katika dini ya watu wake kwa sababu ilikuwa na maslahi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa analingania katika dini ya Allaah usiku na mchana, kwa siri na kwa dhahiri. Hakuna aliekuwa akiweza kumzuia na hilo na kwa ajili ya Allaah hakuna anajali lawama za wenye kulaumu.

[1] at-Tirmidhiy (2288). Dhaifu kwa mujibu al-Albaaniy.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 18-22
  • Imechapishwa: 18/03/2017