6. Muozeshe msichana wako kwa mwanaume anayemcha Allaah

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amembainishia mwanaume kipi anachotakiwa kuzingatia. Je, amembainishia mwanamke ni kipi anachotakiwa kuzingatia? Ndio. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewazungumzisha walezi kuchagua mwanaume mwenye dini na tabia nzuri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapokujieni mwanaume ambaye mmeridhia dini na tabia yake, basi muozesheni. Msipofanya hivo, kutakuwa fitina katika ardhi na usifadi mkubwa.”[1]

Ninaapa kwa Mola wa Ka´bah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kweli pale aliposema:

“Msipofanya hivo, kutakuwa fitina katika ardhi na usifadi mkubwa.”

Endapo mwanaume hatomuozesha mtu wa dini na tabia njema ni lazima kutokee fitina. Hivyo atamuozesha kwa mwanaume asiyekuwa na dini wala tabia njema. Atamfanya nini? Huenda akamuadhibu. Huenda akamlazimisha kufanya mambo Aliyoharamisha Allaah. Baada ya kuwa baba amemlinda msichana wake na mambo ya haramu anamsalimisha kwa mwanaume anayemtumbukiza katika mambo ambayo Allaah Amemharamishia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msipofanya hivo, kutakuwa fitina katika ardhi na usifadi mkubwa.”

Yanapatikana haya pale ambapo hamuozeshi kwa mwanaume mwenye dini na tabia njema. Ni lazima kutokee fitina na uharibifu mkubwa. Kuna mtu alimwambia al-Hasan bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Kuna wanaume wengi wamemchumbia msichana wangu. Nimuozeshe yupi?” Akamwambia: “Muozeshe kwa yule anayemcha Allaah. Akimpenda atamkirimu na akimchukia hatomdhulumu.”[2]

Hivyo atakuwa pamoja naye katika kheri katika hali zote. Allaah Akimtia kwenye moyo kumpenda atamkirimu na kumheshimu. Akimchukia na kutokuwa na mapenzi kwake ndani ya moyo wake hatomfedhehesha, hatomrudisha kwa familia yake na wala hatomdhulumu. Atataamiliana naye kiuadilifu.

[1] at-Tirmidhiy (1084), Ibn Maajah (1967) na wengine. Nzuri kwa mujibu wa Shaykh al-Albaaniy. Tazama ”as-Swahiyhah” (1022) na ”al-Irwaa’” (1868).

[2] Ibn Abiyd-Dunyaa katika ”al-´Ayaal” (1/173).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 23/03/2017