Madhehebu tofauti ya Suufiyyuun waliopetuka mipaka yanaweza kugawanywa mafungu matatu:

1- Wafuasi wa madhehebu ya taaluma za falsafa. Wametilia nguvu nyingi fikira za falsafa kuliko kuipa nyongo dunia. Wanacholenga kwa neno “taaluma” ni kwamba moyo unaangaza kwa nuru ambayo inaenea kwenye mioyo na ambayo inakuwa natija ya malezi ya kinafsi, mazoezi ya kiroho na kuuadhibu mwili ili kuisafisha roho. Hii ni sifa ambayo huenda Suufiyyuun wote wanashirikiana nayo, isipokuwa wafuasi wa fungu hili wamesimama katika mpaka huu na kwa ajili hiyo hawakutumbukia ndani ya kile walichotumbukia wengine kilicho na maana ya kwamba Allaah Yuko katika kila kitu au kila kitu ni Allaah. Lakini hata hivyo madhehebu haya yanakwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu na ni kitu kimechukuliwa kutoka katika dini potevu kama Ubudha na nyenginezo.

2- Wale ambao wanaamini kwamba Allaah amechanganyika kimwili na viumbe – Allaah ametakasika kutokamana na hilo. Hili ni jambo ambalo limelinganiwa na baadhi ya Suufiyyuun waliopindukia kama kwa mfano wa al-Husayn bin Mansuur al-Hallaaj, ambaye matokeo yake wanachuoni walifutu kuwa ni kafiri. Wakaamrisha auawe na akasulubiwa katika mwaka wa 309 baada ya Hijrah. Maneno yafuatayo yananasibishwa kwake:

“Ametakasika Allaah ambaye Amedhihirisha umbile Lake la kibinaadamu

Na kuficha uwazi Wake wa kiungu

Kisha Akajidhihirisha kwa viumbe Wake waziwazi katika sura ya kula na kunywa.”[1]

Vilevile amesema:

“Mimi ndiye mwenye kupenda na Mwenye kupendwa ndio mimi. Sisi ni roho mbili zilizo kwenye kiwiliwili kimoja. Unaponiona mimi, basi umemuona Yeye, na unapomuona Yeye, basi umetuona sote wawili.”

al-Hallaaj alikuwa ni mwenye kuamini kuwa Allaah Anajidhihirisha kwa sura ya viumbe Wake, kwamba uungu una pande mbili na kwamba Allaah ana asili ya kiungu na ya kimtu. Anaona kuwa uungu umekita ndani ya kiwiliwili cha mwanadamu na hivyo roho ya mtu ndio uungu wa kikweli wa Allaah na mwili wake ndio ile sura yake ya kimtu.

Licha ya kwamba aliuawa kwa sababu ya ukafiri wake mbaya – baadhi ya Suufiyyuun wakajitenga naye mbali – kunajitokeza watu ambao wanamzingatia alikuwa ni Suufiy na kuonelea kuwa ´Aqiydah yake ilikuwa sahihi na kuyaandika maneno yake. al-Khatwiyb al-Baghdaadiy amepokea kwamba baadhi ya watu hao alikuwa ´Abul-´Abbaas bin ´Atwaa´ al-Baghdaadiy, Muhammad bin Khaliyf ash-Shirrraaziy na Ibraahiym an-Naswaabaadhiy[2].

3- Fikira ya tatu ni imani ya kuamini kwamba kila kitu kilichopo ni kitu kimoja katika uhakika wake na kila kitu tunachokiona ni kipengele katika Dhati ya Allaah. Kiongozi wa madhehebu haya alikuwa Ibn ´Arabiy al-Haatimiy at-Twaaiy ambaye alikufa mwaka wa 638 baada ya Hijrah na akazikwa Dameski. Anasema kuhusu madhehebu haya katika kitabu chake “al-Futuuhaat al-Makkiyyah”:

“Mja ndiye Mola na Mola ndiye mja. Laiti ningejua ni nani katika yao ambaye inamuwajibikia kufanya ´ibaadah. Itakuwa ni haki lau nitasema kuwa ni mja, lakini lau nitasema ni Mola, vipi itamuwajibikia Yeye kufnaya ´ibaadah?”[3]

Vilevile amesema katika “al-Futuuhaat”:

“Wale waliomwabudu ndama hajamwabudu mwengine isipokuwa Allaah.”[4]

Suufiyyuun Ibn ´Arabiy huyu wanamwita kwa majina mbalimbali ikiwemo “al-´Aarif billaah” (mjuzi zaidi wa kumjua Allaah), “al-Qutwb al-Akbar” (nguzo kubwa), “al-Misk al-Adhwfar” (miski yenye kuenea) na “al-Kibriyt al-Ahmar” (kiberiti chekundu), pamoja na ´Aqiydah yake ya Wahdat-ul-Wujuud na mambo mengine makubwa ya khatari. Amemsifu Fir´awn na kusema kwamba amekufa akiwa muumini. Amemkosoa Haaruun (´alayhis-Salaam) kwa kuwakataza kwake wale watu walioabudia ndama kwa kitendo hicho akiwa ni mwenye kwenda kinyume waziwazi na dalili ya Qur-aan. Anaona kuwa wakristo wamekufuru kwa sababu tu wamesema ya kwamba ´Iysaa ni mungu. Lau wangelisema ya kwamba vitu vyengine vyote ni miungu, basi wasingelikuwa makafiri.

Pamoja na upotevu mwingi wa Ibn ´Arabiy na wanachuoni kumkufurisha bado ni mwenye kuendelea kutakaswa na Suufiyyah na watu wengine ambao hawapambanui kati ya haki na batili na wenye kupuuza kuikubali haki pamoja na kuwa kwake wazi kama jua. Bado vitabu vyake vilivyosheheni ukafiri, kama “al-Futuuhaat al-Makkiyyah” na “al-Fuswusw al-Hukm”, ni vyenye kuenezwa. Isitoshe ana kitabu cha tafsiri ya Qur-aan kinachoitwa “Tafsiyr-ul-Baatwini”. Kwa sababu yeye anaona kuwa kila Aayah ina maana ya nje na maana ya ndani iliyojificha. Uinje wake unatendewa kazi na wale watu wa kawaida na undani wake unatendewa kazi na wale watu maalum[5].

Katika kundi hili alijitokeza Ibn Baashiysh ambaye amesema:

“Ee Allaah! Nipe afya katika bwawa za Tawhiyd na unizamishe katika dhati ya Umoja wa bahari hiyo. Nisukume ndani ya hali ya Umoja huo kiasi cha kwamba nisiweze kuona, kusikia wala kuhisi ila kwayo.”

[1] at-Twawaasiyn, uk. 130, ambacho ni cha Wakiyl.

[2] Taarikh Baghdaad (08/112).

[3] al-Futuuhaat al-Makiyyah ya Dr. Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy katika kitabu chake “al-Hadiyyah al-Haadiyah”, uk. 43.

[4] Yamenukuliwa kama maneno ya Ibn ´Arabiy na Ibn Taymiyyah katika “al-Fataawaa”, mjeledi wa 11, yameandikwa katika kitabu “al-Futuuhaat.

[5] Tazama utangulizi wa tafsiri yake iliyotajwa. Chapa ya Beirut.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 23/12/2019