[7] Idadi ya Rak´ah ni kumi na moja. Tunaona kuwa mtu asizidishe juu ya hizo. Badala yake mtu anatakiwa kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuzidisha juu ya hizo mpaka alipofariki. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa kuhusu swalah yake katika Ramadhaan ambapo akasema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi, si katika Ramadhaan wala nyingine, juu ya Rak´ah kumi na moja. Alikuwa akiswali nne, usiulize juu ya uzuri wake na urefu wake. Kisha akiswali tena nne, usiulize juu ya uzuri wake na urefu wake. Halafu akiswali tatu.”[1]

[8] Hata hivyo inafaa kwa mtu kupunguza idadi yake, hata kama mtu ataswali Rak´ah moja ya Witr peke yake. Dalili ni kitendo na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu kitendo chake, ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Rak´ah ngapi za Witr. Ndipo akajibu:

“Alikuwa akiswali Witr kwa nne[2] na tatu, sita na tatu, kumi na kumi na moja na hakuwa anaswali Witr chini ya saba wala zaidi ya kumi na tatu.”[3]

Ama kuhusu maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), amesema:

“Witr ni yenye kudumu. Yule anayetaka aswali Witr kwa tano, anayetaka aswali Witr kwa tatu na anayetaka aswali Witr kwa moja.”[4]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Imetajwa katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 20-21, na “Swahiyh Abiy Daawuud” (1212).

[2] Katika hizo kunaingia Rak´ah mbili za Sunnah baada ya ´Ishaa na Rak´ah mbili fupi ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akianza swalah ya usiku kwazo. Haya ni maoni ya Haafidhw. Tazama “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 19-20.

[3] Ameipokea Abu Daawuud, Ahmad na wengineo. Hadiyth ina mlolongo wa wapokezi mzuri ambao unazingatiwa kuwa Swahiyh na al-´Iraaqiy. Imetajwa katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 98-99, na “Swahiyh Abiy Daawuud” (1233).

 [4] Ameipokea at-Twahaawiy, al-Haakim na wengineo. Hadiyth ina mlolongo wa wapokezi Swahiyh kama walivyosema maimamu wengi. Ina Hadiyth nyingine mfano wake ilio na nyongeza ambayo ni munkari , kama nilivyobainisha katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 99-100

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 07/05/2019