59. Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar II


Tatu: Kuhusu ngazi za kuamini Qadhwaa´ na Qadar. Kuamini Qadhwaa´ na Qadar ndani yake mna ngazi nne:

Ngazi ya kwanza: Kuamini kuwa Allaah aliyajua yaliyopo na yatayokuwepo kutokana na elimu Yake ya milele ambayo anasifika nayo daima na milele. Hakuna kitu, kilichopo na kitachokuwepo, isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) anakijua. Amesema (Ta´ala):

وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

“Halianguki jani lolote ila Hulijua, na wala punje katika viza vya ardhi, na wala kilichorutubika na wala  kikavu isipokuwa [kimedhibitiwa] katika Kitabu kinachobainisha” (06:59)

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا

“Je, huoni kwamba Allaah anajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watu watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala wa watu watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala wa chini kuliko ya hivyo na wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao [kiujuzi] popote watakapokuwa.” (58:07)

Hakika Yeye anayajua yale mazungumzo na minong´ono inayokuwa kati ya watu. Vilevile Yeye (Subhaanah):

لَا جَرَمَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ

“Hapana shaka kwamba Allaah anajua wanayoyafanya siri na wanayayoyadhihirisha.” (16:23)

وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

“Allaah anayajua yaliyomo vifuani.” (03:154)

وَيَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

“Anajua yale yaliyomo katika mbingu na yale yaliyomo katika ardhi.” (03:29)

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَخْفَىٰ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ

“Hakika Allaah hakifichiki Kwake chochote katika ardhi wala katika mbingu.” (03:05)

Elimu ya Allaah imekusanya yaliyokuwepo, yatayokuwepo na yasiyokuwepo lau yangelikuwepo vipi yangalikuwa. Hivyo elimu ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) imekusanya na imekizunguka kila kitu. Inahusiana na yaliyokuwepo hapo kale, yaliyopo hivi sasa na yatayokuwepo huko mbeleni.

Ngazi ya pili: Uamini na kuitakidi kuwa Allaah ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa kila kitu. Ubao uliohifadhiwa ni kitu kilichoumbwa. Hakuna anayejua namna ilivyo na ukubwa wake isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa).  Ubao huo uko huko Kwake (Jalla wa ´Alaa). Tunauamini na vilevile tunaamini kuhusu uandikwaji huu. Imekuja katika Hadiyth:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ni kalamu kisha Akaiambia: “Andika!” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatayokuwepo hadi Qiyaamah kisimame.””[1]

Hivyo ikawa imeandika yatayokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.

Vilevile imekuja katika Hadiyth ya kwamba:

“Allaah aliandika makadirio ya viumbe miaka elfu khamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[2]

´Arshi na kalamu ni kipi kilichotangulia kuwepo? Kuna kundi lililosema kuwa ´Arshi ndio ilitangulia kabla ya kalamu. Kundi lingine likasema kuwa kalamu ndio ilitangulia kabla ya ´Arshi. Kundi lingine likapambanua. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Watu wametofautiana juu ya kalamu ambayo

imeandika Qadhwaa´ kutoka kwa Allaah

Je, ilikuwa kabla ya ´Arshi au baada yake?

kuna maoni mawili kwa Abu ´Alaa al-Hamadhaaniy

Maoni sahihi ni kuwa ´Arshi ndio ilikuwa kabla yake [kalamu]

kwa kuwa kipindi cha maandiko ilikuwa iko na nguzo

Uandishi ulitokea sambamba ilipopatikana kalamu. Pindi Allaah alipoiumba ndipo akaiambia:

“Andika.”

Kwa mtazamo wa kupatikana, ´Arshi ndio ilitangulia kuwepo. Haya ndio maoni sahihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah alikadiria makadirio ya viumbe miaka elfu khamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”

Aliyakadiria kabla ya uandishi kisha ndio akayaandika. Uandishi ulitokea baada ya kupatikana kwa kalamu. Kupatikana kwa kalamu kulikuja nyuma baada ya ´Arshi. ´Arshi ndio ilitangulia. Ni lazima kuyatambua mambo haya kwa sababu yanaingia katika ngazi ya uandishi. Inahusiana na uandishi wa jumla ulioenea ambapo kuliandikwa kila kitu.

Pengine mtu akauliza Allaah si anamuamrisha Malaika ambaye amewakilishwa kuandika riziki, muda wa kueshi na kama atakuwa mla khasara au mwenye furaha wale watoto walio tumboni mwa mama zao, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika umbo la kila mmoja wenu linakusanywa pamoja katika tumbo la mama yake kwa muda wa siku arobaini, kisha inakuwa mbegu kwa muda kama huo, kisha inakuwa kama tone la damu kwa muda kama huo, halafu anatumiwa Malaika ambaye humpulizia roho na huamrishwa mambo mane: kuandika riziki yake, muda wake wa kueshi, matendo yake na kama atakuwa mla khasara au mwenye furaha.”[3]

Jibu ni kuwa huu ni upambanuzi wa yale yaliyoandikwa hapo kabla. Haya yamechukuliwa kutoka katika yale yaliyotangulia kuandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa.

Vilevile imekuja ya kwamba usiku wenye cheo Allaah hukadiria yatayopitika katika mwaka katika uhai, kufa, vita na mengineyo. Yote haya yanapitika katika usiku wenye cheo. Kwa ajili hii ndio maana ukaitwa kuwa ni usiku wenye cheo kwa kuwa ndani yake kunakadiriwa yatayopitika katika mwaka:

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

“Humo hubainishwa kila jambo la hikmah.” (44:04)

Jibu ni kama lililotangulia ya kwamba uandishi huu unaopitika katika usiku wenye cheo umechukuliwa kutoka katika ule uandishi ulioenea katika Ubao uliohifadhiwa. Kwa hivyo hakuna mgongano kati ya dalili. Dalili ya daraja hizi mbili – ambayo ni elimu na uandishi – ni maneno Yake (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujauumba.” (57:22)

Bi maana kuumba. Ni dalili yenye kuonesha kuwa misiba yote inayopitika imeandikwa katika Ubao uliohifadhiwa.

Ngazi ya tatu: Utashi na matakwa. Kila chenye kupitika basi Allaah amekitaka. Hakupitiki kitu katika ufalme Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) Asichokitaka. Amesema (Ta´ala):

فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ

“Mwingi wa kufanya Atakalo.” (85:16)

إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ

“Hakika Allaah anafanya atakavyo.” (22:18)

وَمَا تَشَاؤُونَ إِلَّا أَن يَشَاء اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu wote.”  (81:29)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Na lau Allaah angelitaka wasingelipigana, lakini Allaah anafanya alitakalo.” (02:253)

Kila chenye kupitika basi Allaah amekitaka baada ya kukijua na kukiandika kwenye Ubao uliohifadhiwa.

Ngazi ya nne: Kuumba. Amesema (Ta´ala):

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

“Allaah ndiye muumbaji wa kila kitu – Naye juu ya kila kitu ni mtegemewa.” (39:62)

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Na hali Allaah amekuumbeni na yale mnayoyatenda.” (37:96)

مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

“… kabla hatujauumba.” (57:22)

Bi maana kabla ya Sisi kuumba. Aayah hizi zimetolea dalili kuthibitisha ngazi ya uandishi, uumbaji na utashi. Hizi ndio ngazi nne ambazo ni wajibu kuziamini:

Ya kwanza: Elimu.

Ya pili: Kuyaandika katika Ubao uliohifadhiwa.

Ya tatu: Kulitaka jambo pale linapotokea.

Ya nne: Kukiumba kitu.

Hizi ndio ngazi za Qadhwaa´ na Qadar. Ambaye anapinga moja wapo hawi mwenye kuamini Qadhwaa´ na Qadar.

[1] Abu Daawuud (4700), at-Tirmidhiy (2155) na (3319), Ahmad (05/317) na wengieno

[2] Muslim (16) na (2653)

[3] al-Bukhaariy (3208), (3332) na Muslim (01) na (2643)