59. Mwenye kumtukana swahabah ni mzushi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kumtukana mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamchukia kwa sababu ya kitu alichofanya au akayataja mabaya yake ni mtu wa Bid´ah mpaka awatakie rehema wote na asiwe na kinyongo na yeyote katika wao.”

MAELEZO

Huu ni msingi moja wapo wa Ahl-us-Sunnah. Haijuzu kumtukana yeyote katika Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala hata kuyataja mabaya yao, kama kweli yatakuwepo. Wale wanaofanya hivo kwa masikitiko makubwa wanaichukulia dini wepesi, Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Aqiydah ya Kiislamu. Mtu anawatweza Mitume na Maswahabah, anakufurisha, anawatuhumu wengine unafiki, anaukufurisha Ummah na wakati huohuo anazingatiwa kuwa bwana wa mabwana na kiongozi wa viongozi. Kwa mujibu wa kina nani? Kwa wale wanaotaka kuunyanyua Ummah na kuurudishia utukufu wake? Watu hawa sio wenye kuaminiwa juu ya dini ya Allaah. Wanatakiwa kutiwa kwenye mkumbo mmoja na Raafidhwah kwa sababu wanatetea madhehebu yao, kufuru, uzandiki na vitabu vilivyobeba jarima hizi. Wamejenga mapenzi na chuki yao juu yake. Watu hawa sio wenye kuaminiwa juu ya dini ya Allaah. Hawana uaminifu, hawana thamani yoyote. Wanatakiwa kutiwa kwenye mkumbo mmoja na Raafidhwah na mapote mengine ya upotevu na wapigwe vita kwa njia kali sana. Watu hawa ni mahaini na ni wafanya ghushi. Wamewafanya kupotea watoto wa Ummah kwa talbisi, hila na vitimbi.

Hii ni dini ya Allaah. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni vipi mnaweza kusema kuwa nyinyi ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ilihali mko mbali na wao? Kila kunapopitika jambo nyinyi mnakuwa pamoja na Ahl-ul-Bid´ah. Kila tunaposhika njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tunakuoneni nyinyi mnashika njia nyingine. Mnatetea  na kuwalinda Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal. Wamebuni vidhibiti na mifumo na wameipindua dunia chini na juu kwa sababu ya kuwatetea Ahl-ul-Bid´ah. Ni vipi watu hawa watakuwa Ahl-us-Sunnah? Wanatakiwa kutiwa katika mkumbo mmoja na wapotevu, Ahl-ul-Bid´ah na Raafidhwah. Hata kama watasema kuwa wako dhidi ya Raafidhwah hatuwaamini. Tusihisi kuwa na amani kuwaacha watoto wetu kuwa pamoja nao. Hii leo watoto wetu wanaenda masomoni na katika vyuo vikuu ambapo wako Ahl-ul-Bid´ah wanaowalea. Wanawalea juu ya ufisadi huu, upotevu, matamanio na kuwatawanyisha vijana wa Ummah kutoka katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Inasikitisha kuona vijana wanajisalimisha nao. Wanawapa uaminifu wa upofu hawa wadanganyifu wanaocheza na akili ya vijana.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kumtukana mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamchukia kwa sababu ya kitu alichofanya… “

Hata kama itathibiti kuwa swahabah huyu alikosea usitaje na wala usimponde. Badala yake unatakiwa kusema kwamba alikuwa Mujtahid. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Yaliyopitika kati ya Maswahabah walikuwa ni Mujtahiduun. Mengi wanayonasibishiwa nayo ni uongo. Mengi wanayonasibishiwa nayo yamepotoshwa, yamegeuzwa, yamebadilishwa, yamezidishwa na kuongezwa juu yake, kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah). Makosa yao yaliyothibiti ni kama tone kwenye bahari. Wakifanya kosa basi mtu anatakiwa kutambua kuwa tende moja wanayotoa inashinda swadaqah ilio sawa na ukubwa wa mlima wa Uhud. Wewe ukitoa thawabu nyingi zilizo sawa na ukubwa wa Uhud na swahabah akatoa shayiri ilio gramu 300, basi shayiri hii ni bora mbele ya Allaah kuliko dhahabu ilio sawa na Uhud na milima ya ulimwengu mzima. Ukikusanya milima yote hii basi haitoshinda swadaqah ya swahabah ilio gramu 300.

Ina maana kwamba ni wajibu kuwaheshimu, kuwakadiria na kutambua nafasi walio nayo mbele ya Allaah. Ikiwa wale wakubwa waliokuja baada ya Maswahabah wakitoa swadaqah na swahabah akatoa gramu 300, basi swadaqah ya swahabah ina uzito zaidi mbele ya Allaah. Tusemeje kuhusu swadaqah yako wewe? Wale wanaowatukana Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakuwaadhimisha na wala hawakuelewa nafasi walio nayo. Wamewachukulia wepesi. Wale wanaowatetea na kuwasapoti watu mfano wa hawa hawakutambua nafasi wala hadhi walio nayo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Vinginevyo ni vipi watawatetea wale  wanaowatukana Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Vitabu vinavyowatukana Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vinachapishwa, vinasambazwa, kuenezwa na kutetewa. Halafu wanasema kuwa ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba Ahl-us-Sunnah hawana lolote kuhusiana na watu hawa!

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 435-437
  • Imechapishwa: 28/12/2017