1 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika katika ufasaha kuna uchawi.”

2 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefananisha ufasaha na uchawi. Kwa sababu mchawi anavuta moyo wa mtazamaji kwa kutumia uchawi wake na mfasaha anavuta moyo wa msikilizaji kwa kutumia ufasaha na upangiliaji wa maneno yake.

3 – Ibn Shubrumah amesema:

“Sijaona sifa nzuri kwa mtu kama uzuri wa ufasaha na sijaona sifa nzuri kwa mwanamke kama unene. Wakati mtu anapozungumza kwa ufasaha basi ni kama amevaa hariri nyeusi. Wakati mtu anapozungumza akakosea basi ni kama amevaa mavazi yaliyoraruka. Ukitaka kumuona mdogo mtumzima na kumuona mkubwa mdogo basi jifunze sarufi.”

4 – Ufasaha ni shuka bora ya juu anayovaa mtu na shuka bora ya chini anayovaa mwenye busara. Adabu ni rafiki ugenini, inayokuliwaza wakati wa upweke, pambo katika mikusanyiko ya watu, ziada ya busara na ni dalili ya muruwa. Ambaye alifaidika adabu kipindi cha utotoni mwake basi atafaidika nayo kipindi cha ukubwani mwake. Anayepanda mti mdogo wa mtende basi punde kidogo atakula tende zake tosa. Wenye busara hawawaoni kulingana watu wawili; mfasaha na ambaye si mfasaha.

5 – Saalim bin Qutaybah amesema:

“Nilikuwa kwa Ibn Hubayrah wakati yalipokuja mazungumzo ya kuhusu lugha ya kiarabu. Akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba hawalingani watu wawili; nasaba yao ni moja na muruwa wao ni mmoja, mmoja wao anazungumza kwa makosa na mwingine hazungumzi kwa makosa. Lakini mbora wao duniani na Aakhirah ni yule asiyezungumza kwa makosa.” Nikasema: “Allaah akutengeneze kiongozi! Naelewa kwamba huyu ni mbora duniani kutokana na ufasaha na kiarabu chake, lakini ni kipi kilichomfanya Aakhirah pia kuwa mbora?” Akajibu: “Anaisoma Qur-aan kama ilivyoteremshwa. Mtu ambaye anatamka kwa makosa kunampelekea kuingiza ndani ya Qur-aan mambo yasiyotakikana na kutoa nje mambo yanayotakikana.” Ndipo nikasema: “Kiongozi amesema kweli.”

6 – Ni lazima kwa mwenye adabu kuusafisha moyo wake kwa adabu kama ambavo moto unasafishwa kwa kuni. Ambaye hausafishi moyo wake basi utachafuka mpaka utakuwa mweusi.

7 – ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy amesema:

“Sijawahi kujutia kitu kama kutosoma kiarabu.”

8 – al-Asma´iy amesema:

“Jifunzeni sarufi! Hakika wana wa israaiyl walikufuru kwa neno moja. Allaah alisema: “Ee ´Iysaa! Hakika mimi nimekuumba (walladtuk)!” Wao wakasoma: “Ee ´Iysaa! Hakika mimi nimekuzaa (waladtuk)!” Matokeo yake wakakufuru.

9 – Watu walio na haja kubwa ya kulazimiana na adabu na ufasaha ni wanazuoni kwa sababu ya kusoma kwao Hadiyth kwa wingi na kuingia ndani ya aina mbalimbali ya elimu.

10 – al-Asma´iy amesema:

“Kikubwa ninachochelea kwa mwanafunzi, ni kwamba asipofahamu sarufi basi anaweza kuingia ndani ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kunisemea uongo kwa makusudi basi ajiandalie makazi yake Motoni.”

11 – Shu´bah amesema:

“Mfano wa anayesoma Hadiyth bila kujua sarufi ni kama mfano wa mnyama aliye na begi tupu la chakula shingoni mwake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 219-223
  • Imechapishwa: 26/08/2021