59. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) ”Wakamdhania Allaah pasi na haki, dhana ya kipindi cha kikafiri”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يَظُنُّونَ بِاللّهِ غَيْرَ الْحَقِّ ظَنَّ الْجَاهِلِيَّةِ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ الأَمْرِ مِن شَيْءٍ قُلْ إِنَّ الأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّهِ

”Wakamdhania Allaah pasi na haki, dhana ya kipindi cha kikafiri, wanasema [kujiuliza wenyewe]: “Je, tuna amri yoyote sisi katika jambo hili?”  Sema: “Hakika amri yote ni ya Allaah.” (Aal ´Imraan 03:154)

2-

الظَّانِّينَ بِاللَّهِ ظَنَّ السَّوْءِ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ

”… wanaomdhania Allaah dhana ovu. Utawafikia mgeuko mbaya … ” (al-Fath 48:06)

3- Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu Aayah ya kwanza:

“Imefasiri dhana hii kwamba Yeye (Subhaanah) hatomnusuru Mtume wake na kwamba amri yake itaangamizwa. Imefasiriwa pia ya kwamba yaliyomsibu haikuwa kwa Qadar ya Allaah na kwa hekima Yake. Imefasiriwa vilevile kwa kupinga hekima, kupinga Qadar na kukanusha kutimia kwa amri ya Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba itazishinda dini zengine zote.

Hizi ndio dhana mbaya walizokuwa wakidhania wanafiki na washirikina katika Suurah “al-Fath”. Hizi zimekuwa ni dhana mbaya kwa sababu ni kumdhania kinyume na yale yanayomstahikia Yeye (Subhaanah). Bali hayalingani na hekima Yake, sifa Zake na ahadi Yake ya kweli. Yeyote mwenye kudhania ya kwamba ataifanya batili kuitokomeza haki kwa hali ya kuendelea, akapinga yaliyotokea ni kwa mipango na makadirio Yake, akapinga kwamba ameyakadiria kwa hekima Yake kubwa inayostahiki kuhimidiwa na kufikiria ya kwamba hayo hutendeka kwa matakwa ya kiholela – mwenye kudhania hivi basi ana dhana za wale waliokufuru. Basi adhabu kali itawapata wale waliokufuru ya Moto. Watu wengi ni wenye kumfikiria Allaah dhana mbaya kwa yanayowasibu na kwa anayowafanyia wengine. Hakuna anayesalimika na hayo isipokuwa yule aliyemjua Allaah kwa majina Yake na sifa Zake na akajua yale yanayopelekewa na hekima Yake na sifa Zake. Hebu yule mwenye akili mwenye kuitakia kheri nafsi yake atilie umuhimu juu ya jambo hili, atubie kwa Allaah na amuombe msamaha kwa kumdhania Mola wake dhana mbaya. Lau ungempeleleza mtu kama basi ungemuona namna anavyojikakama juu ya Qadar na kuilaumu na jinsi alivyo na mitazamo mbalimbali juu ya mambo yalivyotakiwa kuwa badala yake. Inapokuja katika dhana hii baadhi wana kiwango kidogo na wengine kikubwa. Ichunguze nafsi yako mwenyewe; je, wewe umesalimika?

Ikiwa umesalimika kwayo, basi utakuwa umesalimika kwa jambo kubwa

vinginevyo mimi siwezi kukuthibitishia kwamba ni mwenye kuokoka

MAELEZO

Ibn-ul-Qayyim amesema kuhusiana na Aayah ya kwanza:

“Malengo ya mlango huu ni kwamba watu wengi si wenye kujisalimisha juu ya hekima na makadirio ya Allaah. Hawajisalimishi juu ya mawaidha ya Allaah (Subhaanah) kwa waja kuhusiana na makosa yao. Hawawaidhiki na kuzindukana. Bali wanamdhania Allaah vibaya na wanafanya hivo kwa njia nyingi:

1- Wako ambao wanafikiria kuwa yale yanayotokea ambayo hawayapendi yanatokea pasi na hekima na makadirio ya Allaah.

2- Wengine wanadhania kwamba yanatokea tu kwa matakwa na sio kwa hekima.

3- Wapo wengine wanaodhania kuwa Allaah ni mwenye kuwadhulumu viumbe na wakahoji ni kwa nini wametendewa hivi na vile.

Watu wengi ni wenye kufikiria hivi. Ndio maana Allaah (´Azza wa Jall) amesema kuhusu wanafiki:

وَطَائِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِاللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ

“Na kundi likawashughulisha nafsi zao wakamdhania Allaah pasi na haki.” (Aal ´Imraan 03:154)

Haya yalitokea katika vita vya Uhud wakati waislamu waliposhindwa. Wengi walijeruhiwa na sabini wakauawa. Hapo ndipo wanafiki waliongea, wakamdhania Allaah kinyume na haki na wakasema:

 هَل لَّنَا مِنَ الأَمْرِ مِن شَيْءٍ

“Je, tuna amri yoyote sisi katika jambo hili?”

Je, tulikuwa na mamlaka juu ya jambo hili? Wakasema vilevile:

لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا

“Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeuawa hapa.” (Aal ´Imraan 03:154)

Bi maana sisi tumetenzwa nguvu na hatuna la kusema. Muhammad ndiye katuleta katika jambo hili mpaka yakatokea yaliyotokea.

Haya yote ni kwa sababu ya ujinga wao, upotevu wao, uchache wa maono yao na upofu wa nyoyo zao. Ndio maana wakamdhania Allaah vibaya. Hawakufikiria kuwa yaliyotokea yalitokea kwa hekima kubwa. Hawakufikiria kuwa Allaah atamnusuru Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakafikiria kuwa itatokomea misheni ya Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakadhania kuwa yaliyokea hayakutokea isipokuwa kwa utashi peke yake. Dhana zao mbaya hizi zikawa zimekusanya kati ya kumdhania Allaah vibaya kwamba hatomnusuru Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mawalii wake pamoja vilevile na kwamba hafanyi hivo kwa hekima isipokuwa ni kwa utashi peke yake. Yote haya ni batili. Kwa ajili hii ndio maana akabainisha (Subhaanah) katika Kitabu Chake kitukufu hekima na siri ya yale anayoyapanga, anayoyafanya na kuyaweka katika Shari´ah na kwamba anawajaribu waja Wake kwa kuwapa vipindi vya tabu na vya raha ili kusafisha ule uchafu uliyomo katika nyoyo za waumini na kuwatokomeza makafiri. Waumini wanapaswa kutubia kwa Allaah, wamuombe msamaha, wajiandae kukutana Naye (Subhaanah) na kutekeleza haki Zake. Amesema (Ta´ala):

أَوَلَمَّا أَصَابَتْكُم مُّصِيبَةٌ قَدْ أَصَبْتُم مِّثْلَيْهَا قُلْتُمْ أَنَّىٰ هَـٰذَا ۖ قُلْ هُوَ مِنْ عِندِ أَنفُسِكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَمَا أَصَابَكُمْ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ فَبِإِذْنِ اللَّـهِ وَلِيَعْلَمَ الْمُؤْمِنِينَ  وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ نَافَقُوا

“Ulipokusibuni msiba, ingawa mliwasibu [maadui wenu] mara mbili yake, mlisema: “Umetoka wapi huu?” Sema: “Huo ni kutoka kwenu wenyewe.” Hakika Allaah juu ya kila jambo ni muweza. Na yale yaliyokusibuni siku yalipokutana makundi mawili, basi [yalitokea] ni kwa idhini ya Allaah na ili adhihirishe waumini, na ili adhihirishe wale waliofanya unafiki.” (Aal ´Imraan 03:165-167)

Allaah (Subhaanah) anawajaribu watu hawa kwa sababu ya hekima kubwa. Waumini wanapewa mitihani ili zisafishwe imani zao, madhambi yao yasamehewe na ili wajiandae kwa ajili ya kukutana na Mola wao. Makafiri wanafutiliwa mbali na wanafiki wanafedheheshwa na aibu zao na batili zao zinafichuliwa. Nyoyo za wanafiki zimeharibika. Ni wenye kumdhania Allaah vibaya na ndio maana Allaah akawanusuru waumini kama alivyowaahidi:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ

“Enyi mloamini! Mkisaidia kuinusuru dini ya Allaah, basi Atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.” (Muhammad 47:07)

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yule mwenye kuinusuru dini Yake – hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Asiyeshindika – ambao Tukiwamakinisha katika ardhi… “(al-Hajj 22:40-41)

Ahadi hii inaweza kupatikana kwa njia ya kushindwa ambapo waumini wakafa wakiwa mashahidi na wengine wakauawa kwa hekima zilizotajwa.”

Iwapo watu wangekuwa ni wenye kushinda siku zote na hawapatwi na kitu katika majaribio, huenda wangeingiwa na mtihani wa kujiona na kuwa na kiburi kwa Allaah na kutokutambua mapungufu na kasoro zao. Huenda vilevile wangefikiria kuwa mafanikio yao yanatokamana na mamlaka yao, nguvu zao na matendo yao. Wanapofikwa na jambo lenye kuchukiza wanakuwa ni wenye kunyenyekea na kurejea kwa Allaah. Ni wajibu kwa muislamu kuipeleleza nafsi yake ili aweze kusalimika kutokamana na mtihani huu. Endapo mtu ataipeleleza nafsi yake basi ataona namna alivyo na mapungufu na kasoro nyingi na vipingamizi juu ya Qadar na jinsi anavyojiona nafsi yake na matendo yake. Isipokuwa yule aliyekingwa na Allaah.

Ni wajibu kwa muumini kuamini mipango na makadirio ya Allaah, kwamba Yeye ana hekima kubwa katika yale yote anayofanya na kwamba amekwishatangulia kupanga kila kitu. Anatakiwa kutambua kuwa yanatokamana na hekima ya Allaah na sababu zake kuu kwamba Amewasahilishia waumini kwa yale yaliyo bora kwao, akawanyanyua daraja zao na ili wapate kurejea Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 162-164
  • Imechapishwa: 08/11/2018