59. Hivi ndivyo walivyofahamu Salaf – mwisho wa “Kitaab-us-Swifaat”


59- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: al-´Abbaas bin Muhammad ad-Duuriy ametuhadithia: Nimemsikia Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam akisema juu ya Hadiyth kuhusu kuonekana, Kursiy, Mola wetu kucheka juu ya kukata tamaa kwa waja Wake, Mola wetu alikuweko wapi kabla ya kuumba mbingu, kwamba Moto hautojaa mpaka Mola wako (´Azza wa Jall) atapoweka unyayo Wake juu yake ambapo utasema: “Tosha, tosha” na mfano wa Hadiyth kama hizo:

“Hadiyth hizi ni Swahiyh. Wapokezi waaminifu wamezinukuu baadhi kutoka kwa wengine mpaka zikatufikia. Hakika sisi tunaonelea kuwa ni haki na hatuzitilii shaka. Lakini endapo mtu atatuuliza ni vipi anaweka unyayo Wake na ni vipi anacheka, tutamwambia kwamba hazifasiriwi na wala hatukumsikia yeyote akizifasiri.”[1]

60- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: al-´Abbaas bin Muhammad ad-Duuriy ametuhadithia: Nimemsikia Yahyaa bin Ma´iyn akisema: Nimeshuhudia Zakariyyaa bin ´Adiy akimuuliza Wakiy´:

“Ee Abu Sufyaan! Kunasemwa nini kuhusu Hadiyth hizi, kama vile Kursiy na nyenginezo mfano wake?” Wakiy´ akasema: “Tulikutana na Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid, Sufyaan na Mis´ar wakihadithia Hadiyth hizi na wala hawafasiri kitu.”

61- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq as-Swaaghaaniy ametuhadithia: Muhammad bin Sulaymaan – Luwayn – amesema:

“Kulisemwa kuambiwa Ibn ´Uyaynah: “Kunasemwa nini juu ya Hadiyth hizi kuhusu kuonekana ambazo unahadithia?” Akasema: “Hadiyth hizi ni za kweli. Tumezisikia kutoka kwa watu tunaowaamini na kuwaridhia.”

62- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: al-Hasan bin al-Fadhwl bin as-Samh ametuhadithia: Nimemsikia Ahmad bin Abiy Shurayh akisema: Nimemsikia Wakiy´ akitueleza kuhusu Hadiyth ya kuonekana, au nyingine, na akasema:

“Mtakayemuona anapinga Hadiyth hizi, basi mzingatieni kuwa ni katika Jahmiyyah.”

63- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: ´Iysaa bin Ishaaq bin Muusaa al-Answaariy Abul-´Abbaas ametuhadithia: Nimemsikia baba yangu akisema: Nimemsikia Suyaan akisema:

“Kila kitu ambacho Allaah amejisifu Mwenyewe katika Qur-aan tafsiri yake ni kule kukisoma kwake pasi na kukifanyia namna wala kukifananisha.”

64- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Ishaaq bin Ya´quub al-´Attwaar ametuhadithia: Nimemsikia Ahmad bin ad-Dawraqiy akisema: Nimemsikia Wakiy´ akisema:

“Tunajisalimisha Hadiyth hizi kama zilivyokuja. Hatusemi “Kwa nini?” au “Vipi?”

65- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Abul-´Abbaas Ishaaq bin Ya´quub ametuhadithia: Nimemsikia Ahmad bin ad-Dawraqiy akisema: Ahmad bin Nasr amenihadithia: Nimemsikia Sufyaan bin ´Uyaynah akisema nyumbani kwake baada ya ´Ishaa’, baada ya kumuuliza kwa kumng´ang´ania akasema:

“Niache nipumue.” Nikasema: “Ee Muhammad! Mimi nataka kukuuliza kitu.” Akasema: “Hapana usiulize.” Nikasema: “Ni lazima nikuulize. Nisipokuuliza wewe, ni nani nitamuuliza?” Akasema: “Sawa uliza.” Nikasema: “Vipi kuhusu Hadiyth kutoka kwa ´Ubaydah, kutoka kwa ´Abdullaah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah (´Azza wa Jall) atazibeba mbingu kwenye kidole, ardhi kwenye kidole… “

“Nyoyo za wanaadamu ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall)… “

“Allaah (´Azza wa Jall) anashangaa na anacheka.”?

Sufyaan akasema: “Ziko kama zilivyopokelewa. Tunazithibitisha na kuzihadithia pasi na kuzifanyia namna.”

66- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Muhammad bin Muhammad bin ´Umar bin al-Hakam Abul-Hasan bin al-´Attwaar ametuhadithia: Nimemsikia Muhammad bin Mus´ab al-´Aabid akisema:

“Mwenye kudai kwamba Huzungumzi wala Huonekani Aakhirah basi ameukufuru uso Wako na wala Hakutambui. Nashuhudia ya kwamba uko juu ya ´Arshi, juu ya mbingu saba, na sio kama wanavosema maadui Zako mazanadiki.”

67- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq as-Swaaghaaniy ametuhadithia: Muslim bin Qaadim ametuhadithia: Muusa bin Daawuud ametuhadithia: ´Abbaad bin al-´Awaam ametuhadithia:

“Shariyk bin ´Abdillaah alifika kwetu ambapo tukamwambia: “Ee Abu ´Abdillaah! Sisi tuko na watu katika Mu´tazilah ambao wanazipinga Hadiyth hizi:

“Hakika Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kila usiku hushuka katika  mbingu ya dunia.”[2]

na:

“Watu wa Peponi watamuona Mola wao.”

hivyo Shariyk akanihadithia karibu Hadiyth kumi juu ya hili. Kisha akasema: “Ama sisi tumeichukua dini yetu kutoka kwa Taabi´uun na Taabi´uun wameichukua kutoka kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao wameichukua dini yao kutoka kwa yupi?”

68- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Abu ´Abdillaah bin Rawh bin Abiy Sa´d ametuhadithia: Nimemsikia Abu Rubaabah ´Uqbah bin Qubaysah bin ´Uqbah:

“Siku moja tulimwendea Abu Nu´aym. Akashuka kwenye ngazi zilizokuwa nyumbani kwake. Akakaa katikati yetu na alikuwa anaonekana kama mwenye hasira.  Akasema: ”Sufyaan bin Sa´iyd bin Masruuq ath-Thawriy ametuhadithia, Zuhayr bin Mu´aawiyah bin Hudayj bin Rahiyl al-Ju´fiy ametuhadithia, Hasan bin Swaalih bin Hayy ametuhadithia na Shariyk bin ´Abdillaah an-Nakha-iy ametuhadithia:

“Hawa wana wa Muhaajiruun wanaeleza kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ataonekana Aakhirah mpaka alipokuja mwana wa myahudi Sabbaagh na akadai kwamba hatoonekana – yaani Bishr bin al-Marriysiy.”

69- Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Ahmad bin Sa´d Abu Ibraahiym az-Zuhriy ametuhadithia: al-Haytham bin al-Khaarijah ametuhadithia: al-Waliyd bin Muslim ametuhadithia:

“Nilimuuliza al-Awzaa´iy, Maalik bin Anas na Sufyaan ath-Thawriy juu ya Hadiyth hizi zinazozungumzia kuonekana na nyenginezo. Wakasema: “Zipitishe pasi na kuzifanyia namna.”

70- Ibn Makhlad ametuhadithia: Abu Ibraahiym az-Zuhriy ametuhadithia: Yahyaa bin Ayyuub ametuhadithia: ´Abdullaah bin Wahb ametuhadithia, kutoka kwa Maalik bin Anas, kutoka kwa az-Zuhriy aliyesema:

“Jisalimisheni juu ya Sunnah na wala msipingane nazo.”

MWISHO

[1] Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Taymiyyah katika ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (5/51).

[2] al-Bukhaariy (1145) na Muslim (758).

  • Mhusika: Imaam ´Aliy bin ´Umar ad-Daaraqutwniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-us-Swifaat, uk. 114-124
  • Imechapishwa: 13/04/2018