Miongoni mwa haki ya mume juu ya mke wake ni kwamba asimamie kuchunga nyumba yake na wala asitoke isipokuwa kwa idhini yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mwanamke ni mchungi kwenye nyumba ya mume wake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Miongoni mwa haki ya mume juu ya mke ni yeye kusimamia kazi za nyumbani na wala asimlazimishe mume kuleta mfanyakazi ambaye atamtia uzito na kumsababishia khatari juu ya nafsi yake na watoto wake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Maneno Yake:

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah ameamrisha wajihifadhi.”[1]

inapelekea uwajibu wa kumtii kabisa mume wake katika kumhudumia, kusafiri pamoja naye, kujimakinisha kwake na mengineyo. Hivo ndivo ilivyofahamisha Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Hadyi an-Nabawiy”:

“Wale waliosema kuwa huduma ni lazima [kwa mwanamke juu ya mume] wametumia hoja kwamba huo ndio utimilifu wa wema kwa wale waliozungumzishwa na Allaah (Subhaanah). Ama mke kustarehe na huku mume yeye ndiye akamhudumia, kufagia, kusaga vyakula, kutengeneza vitonge vya mkate, kufua, kutandika na kusimamia kazi za nyumbani ni katika maovu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Nao wake wana haki kama ambayo [ya waume zao] iliyo juu yao kwa mujibu wa wema.”[3]

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ

“Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake.”[4]

Mwanamke asipomhudumia, bali yeye mume ndiye anamhudumia, ina maana yeye mke ndiye anamsimamia.” Mpaka aliposema: “Allaah amewajibisha mume kumpa matumizi mke wake, mavazi na makazi katika mkabala wa kustarehe naye, kumhudumia na yale ambayo yamezoeleka kiada kwa wanandoa. Jengine isitoshe mikataba hii isiyofungamana inateremshwa katika desturi. Desturi inasema mwanamke kuhudumia na kusimamia manufaa ya ndani ya nyumba.” Akasema tena: “Si sahihi kutofautisha kati ya mwanamke mtukufu, mwanamke duni, mwanamke fakiri na mwanamke tajiri. Huyu ndiye mwanamke mtukufu zaidi ulimwenguni ambaye alikuwa akimhudumia mume wake. Siku moja alimwendea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimshtakia huduma lakini hakumtia mashaka [ya kwamba sio lazima n.k.].”[5]

[1] 04:34

[2] (32/260-261).

[3] 02:228

[4] 04:34

[5] (05/188-189).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 107-108
  • Imechapishwa: 16/09/2022