59. Allaah ndiye mwenye kuongoza na kupotosha

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Anampotosha Amtakaye na anamtosa kwa uadilifu Wake, anamwongoza Amtakaye na anamuwafikisha kwa fadhilah Zake.

MAELEZO

Anampotosha amtakaye kwa uadilifu Wake na anamwongoza amtakaye kwa fadhilah Zake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anamwongoza amtakaye kwa utukufu Wake:

ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ

“Hiyo ni fadhila ya Allaah humpa amtakaye.”[1]

Shari Allaah (Jalla wa ´Alaa) anafanya impate yule ambaye anaona kuwa inamstahiki. Ni uadilifu kutoka Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni Mwenye kusifiwa kwa hali zote mbili; ni Mwenye kusifiwa juu ya fadhilah Zake na ni Mwenye kusifiwa juu ya uadilifu Wake. Anampotosha amtakaye kwa uadilifu Wake, lakini mja mwenyewe ndiye ambaye amejisababishia upotofu. Asipokubali haki, akaipuuza haki, akaipinga haki, kama vilivyo vitendo vya makafiri kwa Mitume, basi Allaah anamlipa kwa kumpotosha. Namna hii ndivo Allaah anawaadhibu kutokana na matendo na ukengeukaji wao:

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ ۚ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ

“Pindi walipopotoka, basi Allaah akazipotosha nyoyo zao. Na Allaah haongoi watu mafasiki.”[2]

Hawaongoi kutokana na kuasi kwao. Hawaongoi makafiri kutokana na ukafiri wao. Hawaongoi madhalimu kutokana na dhuluma yao. Mambo yamefungamana na sababu zake:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa na akamcha Allaah na akasadikisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[3]

Ambaye anaipenda haki, anaikubali haki na anajibidisha na haki, basi Allaah anamwongoza:

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ

“Na wale walioongoka, basi Anawazidishia uongofu na anawapa taqwa yao.”[4]

Kuhusu yule ambaye anaipa mgongo haki, anaikufuru na kuifanyia ukaidi, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anamtosa. Namna hii ndivo anaadhibiwa. Allaah hawapotoshi waumini na wala hawaongoi wapotofu wasiokubali. Anakiweka kila kitu mahali pake stahiki; anaweka uongofu mahali pake stahiki na anaweka upotofu mahali pake stahiki – yote haya ni uadilifu, fadhilah na hekima.

[1] 62:4

[2] 61:5

[3] 92:5-10

[4] 47:17

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 04/08/2021