58. Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar


Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar ndani yake kuna mambo mengi:

Mosi: Ni kuhusu maana ya Qadhwaa´ na Qadar. Qadar ni Allaah (Jalla wa ´Alaa) kuyakadiria, kuyataka na kuyaumba mambo katika wakati wake. Hii ndio maana ya Qadar. Mara nyingi kunaposemwa Qadhwaa´ na Qadar hakuna tofauti kati yake. Hata hivyo Qadhwaa´ imeenea zaidi kuliko Qadar. Kwa sababu wakati mwingine Qadhwaa´ inakuja ikiwa na maana ya Qadar. Wakati mwingine inakuja ikiwa na maana ya kwamba Allaah amevikadiria vitu na kuvipanga. Vilevile wakati mwingine inakuja ikiwa na maana ya kuwahukumu watu kati ya yale waliyotofautiana:

إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ

Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Qiyaamah katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana nayo.” (45:17)

Kwa hivyo Qadhwaa´ imeeneza zaidi kuliko Qadar.

Pili: Kuhusu kuamini Qadhwaa´ na Qadar. Kuamini Qadhwaa´ na Qadar ni wajibu na ni faradhi juu ya muumini. Kwa kuwa ni nguzo miongoni mwa nguzo za imani sita. Jengine ni kwa sababu ni kuamini uwezo wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa ajili hii ndio maana amesema:

“Qadar ni uwezo wa Allaah. Mwenye kuipinga basi amepinga uwezo wa Allaah (Jalla wa ´Alaa).”[1]

Katika baadhi ya ibara vilevile imekuja:

“Qadar ni siri ya Allaah kwa viumbe Wake.”[2]

Haijuzu kutafiti Qadhwaa´ na Qadar mtu akavuka zile dalili zilizokuja katika Qur-aan na Sunnah na akajikakamua. Haya hatimae yanapelekea katika upotevu na kuchanganyikiwa. Kwa sababu ni siri ya Allaah kwa waja Wake. Pindi utapojikakama na kufanya utafiti hutofikia natija yoyote. Kwa kuwa utakuwa ni mwenye kutafiti jambo ambalo Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameliwaficha viumbe Wake. Inatosha kwako kuamini peke yake. Hakuna yeyote aliyejikakama akafikia natija yoyote. Bali kinyume chake alifikia katika kuchanganyikiwa. Kwa ajili hiyo inatosheleza kwako kutembea kwa mujibu wa dalili zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah juu ya kuthibitisha Qadar na kuiamini. Haya yanakutosheleza.

[1] Ibn Battwah katika “al-Ibaanah” (02/231) na “al-Minhaaj as-Sunnah an-Nabawiyyah” (03/254)

[2] al-Laalakaa´iy katika “I´tiqaad Ahl-is-Sunnah” (1122) (03/1122) na Abu Na´iym katika “al-Hilyah” (06/181)