Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kumpiga mawe mzinifu aliyeoa/kuolewa au aliwahi kuoa/kuolewa ni haki endapo atakiri mwenyewe au kukawepo ushahidi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe na wale viongozi waongofu pia walipiga mawe.”

MAELEZO

Hivi ndivyo anavyoadhibiwa mwenye kuzini; anapigwa mawe mpaka anakufa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpiga mawe mwanamke kutoka katika kabila la Ghaamidiy, Maa´iz, mwanamke kutoka katika kabila la Juhaniy na mayahudi wawili waliozini. Hukumu hii imethibiti katika Tawraat, Injiyl na Qur-aan. Moja katika hukumu za kale ambayo ilikubaliwa na Shari´ah ya Kiislamu ni kupiga mawe. Kupiga mawe ni jambo limewekwa katika Shari´ah katika Tawraat, Injiyl na Qur-aan. Kuliteremshwa Aayah ambapo tamko lake likafutwa na hukumu yake ikabaki. Hayo yameelezwa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) wakati aliposema:

“Hakika Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa haki na akamteremshia Kitabu. Miongoni mwa mambo aliyomteremshia ilikuwa ni pamoja vilevile na Aayah ya kupiga mawe. Tuliisoma, tukaihifadhi na kuifahamu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe na sisi tukapiga mawe baada yake. Nachelea asije kutokea mtu akasema: “Naapa kwa Allaah! Hatupati Aayah ya kupiga mawe katika Qur-aan” na akapotea kwa sababu ya kuacha faradhi miongoni mwa faradhi za Allaah iliyoteremshwa katika Qur-aan. Kupigwa mawe katika Qur-aan ni haki na wanatekelezewa wanaume na wanawake ambao wameoa/kuolewa au waliwahi kuoa/kuolewa baada ya kuthibitishwa ushahidi, ujauzito au mtu mwenyewe akakubali.”[1]

Ushahidi unatakiwa kuwa wa watu wane. Endapo watatu tu ndio watatoa ushahidi, wanaadhibiwa kwa tuhuma. Ni lazima watimie wane. Ni lazima vilevile waone kabisa kuwa dhakari ya mwanaume iko ndani ya uke wa mwanamke. Ushahidi wao haukubaliwi endapo hawatimii watu wane ambao kweli wameona jimaa. Masharti haya ni kwa sababu ya kulinda uhai na heshima:

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ

“Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Midhali hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.”[2]

Mtu kukubali mwenyewe ni ushahidi mwingine. Maa´iz na mwanamke kutoka katika kabila la Ghaamidiy wote wawili walikubali wenyewe.

Ujauzito wa mwanamke ni ushahidi mwingine. Ushahidi wake ni ushahidi bora kabisa.

Tunachotaka kusema ni kuwa adhabu ya kupigwa mawe haitekelezwi kabla ya  kupatikana ushahidi wa watu wane, mwanaume au mwanamke akubali mwenyewe au mimba. Hii ndio adhabu ya mzinifu ambaye ameoa/kuolewa au aliwahi kuoa/kuolewa. Kwa msemo mwingine mtu alimuoa mwanamke kwa kufunga ndoa sahihi na akamwingilia kipindi cha ndoa hii. Masharti haya ni lazima yapatikane ili adhabu iweze kutekelezwa:

1- Mtu anatakiwa kuwa na akili na asiwe ni mwendawazimu.

2- Mtu anatakiwa awe amebaleghe na si mtoto.

3- Mtu anatakiwa awe huru na asiwe mtumwa. Akiwa mtumwa au kijakazi, ni mamoja wawe wameshaingia katika ndoa au bado, adhabu yao ni nusu ya adhabu ya aliye huru, nayo ni bakora khamsini. Kwa sababu kupigwa mawe hakuwezi kufanywa nusu na kwa sababu vilevile adhabu ya walio huru na ambao bado hawajaingia katika ndoa ni kama Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alivyosema:

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamme mpigeni kila mmoja katika wawili hao bakora mia na wala isiwashikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah mkiwa kweli mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Na washuhudie adhabu yao kundi la waumini.”[3]

Adhabu ya mtumwa ni nusu ya adhabu ya aliye huru, nayo ni bakora khamsini. Hapigwi mawe hata kama ameshawahi kuingia katika ndoa sahihi. Hapati jengine zaidi ya nusu ya adhabu ya aliye huru, nayo ni bakora khamsini. Imaam Ahmad amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe na wale viongozi waongofu pia walipiga mawe.”

Haya tumeshayapitia.

[1] al-Bukhaariy (6830) na Muslim (1691).

[2] 24:13

[3] 24:02

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 434-435
  • Imechapishwa: 28/12/2017