58. Kila kitu kinatokea kwa makadirio ya Allaah


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Alikijua kila kitu kabla ya kuwepo kwake na mambo yakapitika kwa mujibu wa makadirio Yake. Waja Wake hawasemi neno lolote wala kutenda kitendo chochote isipokuwa amekwishakikadiria na kutangulia kukijua:

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

“Kwani hajui Yule aliyeumba na hali Yeye ni Mwenye kuendesha mambo kwa upole, Mwenye khabari za ndani kabisa?”[1]

MAELEZO

Allaah alikijua kila kitu kwa ujuzi Wake wa milele anayosifika kwayo milele na siku zote. Baadaye yakatokea mambo kwa wakati wake. Waja hawasemi neno lolote wala hawafanyi kitendo chochote kizuri na kibaya, kuamini na kukufuru, kutoa ahadi, kutukana wala kuapiza, isipokuwa Allaah amekwishayakadiria na kuyapanga na baadaye akayaumba na kuyafanya yapatikane. Amesema (Ta´ala):

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

“Kwani hajui Yule aliyeumba na hali Yeye ni Mwenye kuendesha mambo kwa upole, Mwenye khabari za ndani kabisa?”

Hapa swali linaulizwa kwa njia ya kuthibitisha. Aayah inafahamisha kwamba hakuumba isipokuwa baada ya kuyajua. Aliyajua mambo, kisha baadaye akayaumba. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake na Yeye ni Mwenye khabari juu ya kila kitu.

[1] 67:14

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 47
  • Imechapishwa: 04/08/2021