58. al-Qummiy upotoshaji wake wa pili wa Aal ´Imraan

al-Qummiy amesema pindi alipokuwa akifasiri Aayah:

وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ النَّبِيِّينَ لَمَا آتَيْتُكُم مِّن كِتَابٍ وَحِكْمَةٍ ثُمَّ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مُّصَدِّقٌ لِّمَا مَعَكُمْ لَتُؤْمِنُنَّ بِهِ وَلَتَنصُرُنَّهُ

“[Kumbukeni pindi] Allaah alipochukua fungamano kwa Manabii [akawaambia:] “Nikisha kupeni Kitabu na hikmah, kisha [siku moja] akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mlionayo; ni juu yenu mumuamini na mumnusuru.”[1]

“Baba yangu amenieleza, kutoka kwa Abu ´Umayr, kutoka kwa Ibn Masaakin, kutoka kwa Abu ´Abdillaah aliyesema: “Allaah hakupatapo kutuma Nabii yeyote kuanzia Aadam kuendelea mbele isipokuwa alirudi duniani ili kumnusuru kiongozi wa waumini.” Neno:

لَتُؤْمِنُنَّ بِهِ

“… ni juu yenu mumuamini… “

bi maana Mtume wa Allaah na neno:

وَلَتَنصُرُنَّهُ

“… na mumnusuru.”

bi maana kiongozi wa waumini. Kisha Akasema:

أَأَقْرَرْتُمْ وَأَخَذْتُمْ عَلَىٰ ذَٰلِكُمْ إِصْرِي

“Je, mmekiri nammekubali fungamano langu juu ya hayo?”

Bi maana mkataba Wangu:

قَالُوا أَقْرَرْنَا

“Tumekiri.”

Ndipo Allaah akawaambia Malaika:

فَاشْهَدُوا وَأَنَا مَعَكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ

“Basi shuhudieni; Nami niko pamoja nanyi katika wenye kushuhudia.”[2]

Ni ujasiri mkubwa ulioje walionao Baatwiniyyah Raafidhwah kwa kumsemea uongo Allaah na Kitabu Chake. Ni mara ngapi wanajaribu kumuweka ´Aliy katika ngazi ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Wanaweza hata kumnyanyua ´Aliy ili wawapotoshe watu na sio kwa sababu eti wanampenda.

Allaah hakuwatuma Mitume wa hapo kabla kama Muusa, Daawuud na Sulaymaan kumnusuru Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), sembuse kumnusuru ´Aliy. Huoni namna ambavyo Baatwiniyyah wanamfadhilisha ´Aliy juu ya Mtume wa Allaah na Mitume wengine (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam)? Isitoshe watamnusuru ´Aliy dhidi ya nani? Dhidi ya Maswahabah. Ni kwa nini Allaah hakuwatuma Mitume kumnusuru ´Aliy katika vita vya Swiffiyn na dhidi ya Khawaarij? Hii ni dalili ya wazi kabisa juu ya kwamba imani ya kuamini Kurudia ni ukafiri na ni uongo mkubwa juu ya Allaah.

Maana ya Aayah ni kwamba Allaah alichukua fungamano kwa Mitume ya kwamba wasadikishane na wanusuriane wao kwa wao. Tafsiri nyingine ni ile inayonasibishwa kwa ´Aliy na Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambao wamesema:

“Allaah hakutuma Mtume yeyote isipokuwa alichukua fungamano kutoka kwake ya kwamba pindi atapotumwa Muhammad katika uhai wake, basi amuamini na kumnusuru. Aliamrisha vilevile kuchukua fungamano na Ummah wake ya kwamba Muhammad akitumwa ilihali wako hai, wamwamini na wamnusuru.”

Tazama Tafsiyr ya Qur-aan ya Ibn Kadhiyr[3]. Ibn Jariyr amechagua hiyo tafsiyr ya kwanza[4].

[1] 03:81

[2] Tafsiyr al-´Ayyaashiy (1/106).

[3] Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhiym (3/100)

[4] Jaami´-ul-Bayaan (3/332-333).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 03/04/2017