2- Yote haya ni katika matendo ya ki-Shaytwaan yaliyoharamishwa yanayoitia kasoro ´Aqiydah au kuivunja kabisa. Kwa sababu hayafikiwi isipokuwa kwa kufanya mambo ya kishirikina.

Uchawi  ni ibara ya kilichojificha na ikakosekana sababu yake. Umeitwa ´uchawi` kwa sababu unafanyika kwa mambo yenye kujificha yasiyoonekana kwa macho. Uchawi ni hirizi, visomo, maneno anayosema, madawa na kufukiza. Upo uchawi wa kikweli na ambao unaathiri mioyo, miili, kumfanya mtu mgonjwa, kuua na kuachanisha kati ya mtu na mke wake. Kuathirika kwake ni kutokana na idhini ya Allaah ya kilimwengu. Uchawi ni matendo ya kishaytwaan. Uchawi aina nyingi haufikiwi isipokuwa kwa kufanya kwanza shirki, kujikurubisha kwa roho chafu kwa yale wanayoyapenda na kuwatumia kwa kuwashirikisha. Kwa sababu hiyo Shari´ah imeuambatanisha na shirki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na mambo saba yenye kuangamiza.” Wakasema: “Ni yepi?” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, uchawi… “[1]

 Kwa hivyo uchawi unaingia ndani ya shirki kwa njia mbili:

Ya kwanza: Ndani yake kuna kuwatumia mashaytwaan, kuwategemea na kujikurubisha kwao kwa yale wanayoyapenda ili waweze kumsaidia huyo mchawi. Kwa hiyo uchawi ni katika mafunzo ya mashaytwaan. Amesema (Ta´ala):

وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ

“Lakini mashaytwaan ndio waliokufuru: wanafundisha watu uchawi.”[2]

Ya pili: Ndani yake kuna kudai elimu ya mambo yaliyofichikana na kudai kushirikiana na Allaah katika hayo, mambo ambayo ni kufuru na upotevu. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ

“Hakika walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote.”[3]

Bi maana fungu.

Mambo yakishakuwa ni hivo basi hapana shaka kwamba ni kufuru na shirki inayoivunja ´Aqiydah. Ni lazima kumuua yule mwenye kuyafanya, kama walivofanya wakubwa katika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Wakati mwingine watu wanaweza kuchukulia wepesi jambo la mchawi na uchawi. Pengine hata wakafanya hiyo ni sanaa miongoni mwa sanaa wanazojigamba kwazo, wakawapa wenye nazo majizawadi, wakafanya vilabu, matamasha na mashindano kwa ajili ya uchawi na yakahudhuriwa na maelfu ya watazamaji na mashabiki au uchawi huo wakauita kuwa ni ´sarakasi`. Huku ni kuwa na ujinga juu ya dini, kuchukulia wepesi suala la ´Aqiydah na kuwamakinisha wenye wazimu.

[1] al-Bukhaariy (2766) na Muslim (258).

[2] 02:102

[3] 02:102

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 23/03/2020