Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا

Wanasema: “Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa.” (Aal ´Imraan 03:154)

2-

الَّذِينَ قَالُواْ لإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُواْ لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا

“Wale ambao waliwaambia ndugu zao nao wakakaa [hawakwenda vitani]: “Lau wangelitutii basi wasingeliuawa.” (Aal ´Imraan 03:168)

3- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi  wa sallam) amesema:

“Pupia juu ya yale yanayokunufaisha na mtake msaada Allaah na wala usivunjike moyo. Utapofikwa na jambo usiseme ´Lau ningelifanya hivi basi ingelikuwa kadhaa na kadhaa´. Lakini badala yake sema:

قَدَر الله و ما شاء فعل

“Hivi ndivyo alivyokadiria Allaah na hufanya atakavyo.”

Kwani hakika ya ´lau` hufungua matendo ya shaytwaan.”[1]

MAELEZO

Mlango huu unazungumzia kuhusu neno ´lau` na kama linafaa au halifai. Kinachokusudiwa ni kwamba haitakikani kulitumia kwa sababu linapingana na Qadar. Ni wajibu kujisalimisha na kusubiri. Pindi ndugu anapofariki, anapokuwa mgonjwa au anapopatwa na msiba basi haitakikani kupingana na kusema ´lau`.

 1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا

Wanasema: “Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa.”

Hapa wanasemwa vibaya na kukosolewa.

2-

الَّذِينَ قَالُواْ لإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُواْ لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا

“Wale ambao waliwaambia ndugu zao nao wakakaa [hawakwenda vitani]: “Lau wangelitutii basi wasingeliuawa.”

Ni dalili inayoonyesha kuwa haijuzu kutumia neno hilo kwa ajili ya kupingana na Qadar wakati wa ugonjwa, maangamivu na mfano wake. Hivi ndivo walivyo  wanafiki. Makadirio na mipango ya Allaah ni jambo ambalo halina budi kutokea. Ameweka katika Shari´ah kufanya sababu kwa sababu ya hekima kubwa. Ni wajibu kwa muislamu kufanya yale anayotakiwa kufanya na pindi Qadar itatokea basi haimpasi yeye kupingana na makadirio hayo.

 3- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi  wa sallam) amesema:

“Pupia juu ya yale yanayokunufaisha na mtake msaada Allaah na wala usivunjike moyo. Utapofikwa na jambo usiseme ´Lau ningelifanya hivi basi ingelikuwa kadhaa na kadhaa´. Lakini badala yake sema:

قَدَر الله و ما شاء فعل

“Hivi ndivyo alivyokadiria Allaah na hufanya atakavyo.”

Kwani hakika ya ´lau` hufungua matendo ya shaytwaan.”

Kuna baadhi wameiandika namna hii:

قَدَّر الله و ما شاء فعل

“Hivi ndivyo alivyokadiria Allaah na hufanya atakavyo.”

Hata hivyo hiyo ya kwanza ndio sahihi zaidi na maana yake ni kwamba haya kweli ni makadirio ya Allaah. Makadirio ya Allaah na hufanya atakavyo.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi  wa sallam):

“Kwani hakika ya ´lau` hufungua matendo ya shaytwaan.”

Inamfungulia mja matendo ya shaytwaan, bi maana wasiwasi na kumtia mashaka. Ni wajibu kwa muumini kuliepuka ili asije kutumbukia katika mtego wa shaytwaan. Mambo yote haya yamepangwa na Allaah. Kwa ajili hii amesema (Ta´ala):

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao [katika kazi zenu]. Wabashirie wale wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.” (al-Baqarah 02:155-157)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi  wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayepatwa na msiba na akasema ´Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na Unipe badala yake kheri kuliko´ isipokuwa humlipa kwa msiba wake na humpa badala ilio bora kuliko.”[2]

Kwa mfano mgonjwa ameenda kwa daktari kutafuta matibabu na akafa, wale wengine hawatakiwi kusema ´Lau angelienda kutibiwa kwa daktari mwingine na akasafiri nje  ya nchi`. Wanachotakiwa kusema ni:

قَدَر الله و ما شاء فعل إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعونَ

“Hivi ndivyo alivyokadiria Allaah na hufanya atakavyo. Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

 Asipingane kwa neno ´lau`.

Ama ´lau` ikitumiwa kubainisha kitu kilichotakikana kufanyika, haihesabiki ni kupingana. Ni ubainifu wa kitu ambacho ni bora zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Hivi sasa ningefanya kitu nilichokiacha basi ninge… “[3]

Kuzungumza namna hiyo ili kubainisha ambacho kingekuwa bora zaidi haina neno. Mfano wa hilo ni:

“Ningelijua kuwa ni mgonjwa basi ningelimtembelea.”

Hapa mtu anabainisha juu ya kitendo bora zaidi kilichompita. Huku sio kwa njia ya kukinzana na ni jambo halihusiani na mlango huu. Kilichokatazwa ni kukinzana na Qadar.

[1] Muslim (2664).

[2] Muslim (918).

[3] al-Bukhaariy (1651) na Muslim (1216).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 159-160
  • Imechapishwa: 07/11/2018