57. Hukumu ya wanawake kupiga dufu kwa ajili ya kutangaza ndoa

Imependekezwa kwa wanawake kupiga dufu ili ndoa itangazike na ienee na hayo yanafanyika kati ya wanawake peke yao. Dufu hilo lisiambatane na muziki, ala za pumbao wala sauti nzuri za wanawake. Katika mnasaba huu hakuna neno kwa wanawake kuimba mashairi kwa njia ya kwamba wasisikiwe na wanaume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kipambanuzi kati ya halali na haramu ni dufu na sauti katika ndoa.”

Imaam ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Katika hayo kuna dalili inayoonyesha kuwa inafaa kwa wanawake kupiga dufu na kunyanyua sauti zao kwa kitu katika maneno kama mfano wa:

أتيناكم أتيناكم

“Tumekujieni, tumekujieni… “

na mfano wake. Si kwa nyimbo zenye kuamsha maovu, kusifu uzuri, madhambi na kunywa kwa pombe. Hayo ni haramu ndani ya ndoa kama ilivyo pia haramu kwenginepo. Vivyo hivyo pumbazo zengine zote zilizoharamu.”

Ee dada wa Kiislamu! Usifanye israfu katika kununua vitu vya kujipamba na nguo katika mnasaba wa ndoa. Matendo haya ni israfu ambayo imekatazwa na Allaah na akaeleza kwamba hawapendi wenye kufanya hivo. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ

“Wala msifanye israfu. Hakika Yeye hawapendi wafanyao israfu.”[1]

Fanya mambo kati na kati na achana na mambo ya kujifakharisha.

[1] 06:141

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 106
  • Imechapishwa: 20/11/2019