57. Hekima ilioko nyuma ya kheri na shari


Allaah amekadiria kila kitu, kizuri na kibaya, imani na ukafiri, uongofu na upotofu. Kwa upande wa Allaah kukiumba ni kizuri na sio shari, kwa sababu Allaah amekiumba kwa hekima. Hata hivyo ni kibaya kwa yule ambaye kimempata. Kifo, kujeruhika na mambo ya kuchosha huzingatiwa kuwa ni mabaya kwa yule ambaye yamempata. Lakini sio shari inapokuja kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni mambo yanayojulisha ukamilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa vile ameumba kizuri na kibaya. Kuyaumba yote mawili ni katika maajabu ya uumbaji Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuumba shari isipokuwa kwa hekima na sio burebure. Ameiumba ili apate kuwajaribu kwayo na kuwaadhibu kwayo. Adhabu ni kitu kibaya kwa yule ambaye ametumbukia ndani yake, lakini hata hivyo ni uadilifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa nisba ya Allaah ni kitu chenye kusifiwa kwa sababu kimewekwa mahali pake stahiki. Kama ambavo analimpa mtenda wema kadhalika anamuadhibu mtenda maovu kutokana na machumo yao. Haya yanajulisha uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo ni lazima kuamini Qadar, nzuri na shari yake. Mtu asiamini nzuri yake peke yake bali anapaswa kuamini zote mbili. Zote mbili ni zenye kutoka kwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Shari si yenye kutoka Kwako.”[1]

Qadar ni tamu na chungu kwa upande wa waja. Shari ni chungu na kheri ni tamu – zote mbili zinatokamana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah ameumba vinyume viwili kutokana na hekima Yake ili upate kutambulika uwezo, utashi na hekima Yake.

[1] Muslim (771).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 04/08/2021