57. Adhabu iliyowekwa katika Shari´ah ni kafara

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule mwenye kukutana Naye baada ya kutekelezewa adhabu ya dhambi yake hapa duniani, basi hiyo ndio kafara yake. Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atakayekutana Naye hali ya kuwa ni mwenye kuendelea juu ya madhambi yake pasi na kutubia madhambi yanayopelekea kuadhibiwa, jambo lake liko kwa Allaah; akitaka kumuadhibu Atamuadhibu na akitaka kumsamehe Atamsamehe. Hata hivyo yule atakayekutana Naye akiwa ni kafiri atamuadhibu na wala hatomsamehe.”

MAELEZO

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum):

“Nipeni kiapo ya kwamba hamtomshirikisha Allaah na chochote, hamtoiba, hamtozini, hamtowaua watoto wenu, wala hamtoleta usingiziaji wa kashfa mlioizua baina ya mikono yenu na miguu yenu na wala kwamba hamtoniasi katika mema. Yule atakayeyahakikisha hayo basi ujira wake uko kwa Allaah. Yule atakayefanya kitu katika hayo na akaadhibiwa duniani  basi hiyo ndio kafara yake. Yule atakayepatwa na kitu katika hayo na Allaah akawa amemsitiri, basi jambo lake liko kwa Allaah; akitaka Atamuadhibu na akitaka Atamsamehe.”[1]

Mtenda dhambi yuko chini ya matakwa ya Allaah. Amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah, basi hakika amezua dhambi kuu.”[2]

Allaah ana khiyari akitaka atamsamehe na akitaka atamuadhibu. Yeye anaghufuria, anahurumia na ni mpole. Inawezekana hata Allaah akamsamehe mtenda dhambi ambaye yuko na madhambi kama mlima. Mtu yule wa madhambi atayaona madhambi yake yameandikwa kwenye madaftari tisini na tisa, kila daftari litakuwa na madhambi kwa upeo wa umbali wa macho yanapoweza kufika. Pamoja na hayo Allaah atamsamehe kwa sababu ya shahaadah ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah´. Mpwekeshaji atayekutana na Allaah pasi na kumshirikisha atasamehewa na kutolewa Motoni kabla au baada. Imaam Ahmad amesema:

“Hata hivyo yule atakayekutana Naye akiwa ni kafiri atamuadhibu na wala hatomsamehe.”

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah, basi hakika amezua dhambi kuu.”

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[3]

[1] al-Bukhaariy (3892) na Muslim (1709).

[2] 04:48

[3] 05:72

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 432
  • Imechapishwa: 10/12/2017