56. Sura ya kwanza: Kudai elimu iliyofichikana kwa kusoma kiganja cha mkono, kikombe, unajimu na mengineyo

1- Makusudio ya elimu iliyofichikana ni yale yaliyofichikana kwa watu katika mambo yatayokuja huko mbele, yaliyopita na yale wasiyoyaona. Allaah ameifanya elimu hii ni maalum Kwake. Amesema (Ta´ala)

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Sema: “Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye ghaibu isipokuwa Allaah.”[1]

Hakuna ajuaye elimu iliyofichikana isipokuwa Allaah pekee. Lakini hata hivyo Allaah anaweza kumfunulia mjumbe Wake kutoka katika ghaibu Yake kutokana na hekima na maslahi fulani. Amesema (Ta´ala):

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ

“Mjuzi wa ghaibu na wala hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake; isipokuwa yule aliyemridhia miongoni mwa Mitume.”[2]

Bi maana hafunuliwi kitu katika ghaibu Yake isipokuwa yule aliyemteua kwa ajili ya ujumbe Wake na hivyo anamdhihirishia akitakacho katika yaliyofichikana. Kwa sababu itatumiwa kama dalili juu ya utume wake kwa hiyo miujiza ambayo moja wapo ni kuelezea mambo yaliyofichikana ambayo Allaah amemfunulia. Hapa anaingia mjumbe wa ki-Malaika na wa kibinaadamu. Hawafunuliwi wengine wasiokuwa hao kutokana na dalili ya ukomekaji.

Kwa hivyo yule mwenye kudai elimu iliyofichikana, kwa njia yoyote, mbali na wale waliovuliwa katika wajumbe Wake, basi huyo ni mwongo na ni kafiri. Ni mamoja atadai hivo kwa kusoma kiganja cha mkono au kikombe, ukuhani, uchawi, unajimu au mengineyo. Haya ndio yanayofanywa na baadhi ya wachawi na waongo ambapo wanaelezea sehemu kilipo kitu kilichopotea, vitu vilivyofichikana na sababu za baadhi ya magonjwa. Utawaona ni wenye kusema kwamba fulani ndiye kakufanyia kitu fulani na fulani na hivyo ukapatwa na maradhi kwa sababu hiyo. Haya yanafanyika kwa kuwatumia majini na mashaytwaan. Lakini wao huwaonyesha watu kuwa wameweza kufanya hivo kupitia vitendo vya mambo hayo kwa ajili ya kutaka kukudanganya na kubabaisha. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Makuhani mmoja wao huwa na rafiki katika mashaytwaan ambaye anampa khabari mambo mengi yaliyofichikana kutokana na yale aliyosikia kwa kuiba. Huwa wakichanganya ukweli kwa uongo.” Mpaka aliposema: “Miongoni mwa watu hawa wako ambao mashaytwaan huwaletea vyakula, matunda, vitu tamtam na vyenginevyo ambavyo havipatikani sehemu hiyo. Miongoni mwao wako ambao majini yanawarusha kwenda Makkah, Yerusalemu au kwenginepo.”[3]

Wakati mwingine pengine khabari zao zikawa kwa njia ya unajimu ambapo kupitia hali za nyota wakatoa dalili juu ya yanayozuka ulimwenguni kama mfano wa nyakati za upepo, kunyesha kwa mvua, kubadilika kwa bei za bidhaa na vitu vyenginevyo ambavyo wakadai kwamba vinaweza kujulikana kwa kusoma zile nyota, namna vinavyotembea, kukusanyika kwake, kuachana kwake na wakasema kwamba mtu ambaye ataoa nyota fulani na fulani basi atapata kitu fulani na fulani, mwenye kusafiri kwa nyota fulani basi atapata kitu fulani, ambaye atazaa kwa nyota fulani na fulani basi atapata kitu fulani katika furaha au mkosi. Hayo ni kama baadhi ya magazeti duni yanavotangaza upuuzi kuhusiana na nyota na bahati ambazo mtu atapata. Pengine baadhi ya wajinga na watu wenye imani dhaifu wakawaendea wanajimu hawa na wakawauliza juu ya mustakabali wa maisha yao, watapitikiwa na nini, kuhusu kuoa kwao na mengineyo.

Mwenye kudai elimu iliyofichikana au akamsadikisha mwenye kudai elimu iliyofichikana, basi huyo ni mshirikina na kafiri. Kwa sababu amedai Allaah kushirikiana katika sifa ambazo ni maalum Kwake. Nyota zimedhalilishwa na zimeumbwa. Hazina chochote cha kujiamulia, hazifahamishi mkosi, furaha, kifo wala uhai. Yote haya ni miongoni mwa matendo ya mashaytwaan wenye kuiba usikizi.

[1] 27:65

[2] 72:26-27

[3]  Majmuu´-ut-Tawhiyd, uk. 797-801.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 19/03/2020