56. Fadhila za baadhi ya maimamu wa Ahl-us-Sunnah


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

24- Walioko baada yao ni Taabi´uun kwa uchukuliaji wao mzuri

     sawa kwa matendo na maneno yao na wakawa ni wenye kufaulu

 

25- Pia na Maalik, ath-Thawriy na halafu ndugu zao

     Abu ´Amr al-Awzaa´iy

 

26- Waliokuja baada yao ash-Shaafi´iy na Ahmad

     ni imamu wa uongofu mwenye kufuata haki na kunasihi

27- Hao ni watu waliosamehewa na Allaah

     hivyo wapende hakika utafurahi

MAELEZO

Walioko baada yao… – Wanaofuatia baada ya Maswahabah ni Taabi´uun. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“Na wale waliotangulia awali katika Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema.” (09:100)

Maneno Yake:

وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“… na wale waliowafuata kwa wema.”

yanajumuisha wale wote waliowafuata kwa wema hadi siku ya Qiyaamah. Lakini kunaposewa neno “Taabi´iy” kunakusudiwa yule ambaye alichukua elimu na akasoma kutoka kwa Swahabah. Vinginevyo neno “mfuataji” linajumuisha kila yule ambaye alichukua na akapita juu ya mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuanzia wale wa mwanzo, ambao walikuwa baada ya Maswahabah na wa mwisho. Kwa ajili hii amesema (Jalla wa ´Alaa) baada ya kuwataja Muhaajiruun na Answaar:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.” (59:10)

Katika Aayah hii kuna Radd kwa Raafidhwah ambao wanawachukia Maswahabah wa Mtume wa Allaah kwa mioyo yao na wanatamka kwa ndimi zao. Bali wanawalaani kabisa na kuwakufurisha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hii ndio maana Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwa na mioyo na ndimi safi kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[1]

Wana mioyo safi kutokana na maneno Yake:

وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا

“… na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki.”

Vilevile wana ndimi safi kutokana na maneno Yake:

يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ

“Wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani.””

Katika Aayah hii kuna mafunzo ya kwamba inatakiwa kwa mtu awe na moyo na ulimi mzuri kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huu ndio mfumo wa wale wenye kuwafuata kwa wema.

Kuhusu wale ambao wanajeruhi, kupekua kasoro, kutatiza juu ya fadhila za Maswahabah, kuwakufurisha na kuwalaani, haya ni mambo yanayoenda kinyume na mfumo wa Kiislamu, anaujengea uadui Uislamu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu akiwatukana Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile ameitukana Qur-aan inayowasifu na kuwatapa.

Pia na Maalik, ath-Thawriy na halafu ndugu… – Mwandishi (Rahimahu Allaah) anataja fadhila za maimamu. Miongoni mwao ni maimamu hawa:

Maalik mkusudiwa ni Maalik bin Anas ambaye ni Imaam wa al-Madiynah.

ath-Thawriy mkusudiwa ni Sufyaan ath-Thawriy.

al-Awzaa´iy mkusudiwa ni Imaam wa watu wa Shaam.

Waliokuja baada yao ash-Shaafi´iy na Ahmad – Ni Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy na Ahmad bin Hanbal.

hivyo wapende hakika utafurahi – Wapende as-Salaf as-Swaalih na maimamu wa Uislamu. Hakika kufanya hivo ni alama ya imani.

Hakumtaja Abu Haniyfah kwa kuwa imesemekana kuwa yeye ni katika Taabi´uun na kwamba alikutana na kundi la Maswahabah. Maoni sahihi ni kwamba yeye ni katika waliokuja baada ya Taabi´uun. Hakukutana na Maswahabah. Alikutana na Taabi´uun. Yeye ni mtu wa karne ya tatu ambayo ni moja ya zile karne bora (Rahimahu Allaah). Yeye ndiye imamu wa kwanza miongoni mwa wale maimamu wane inapokuja katika zama.

[1] ´Aqiydah al-Waasitwiyyah katika “Majmuu´-ul-Fataawaa” (03/152).