55. Sifa ya Sujuud


Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitanguliza mikono yake ardhini kabla ya magoti[1]. Ameamrisha hilo na kusema:

“Ataposujudu mmoja wenu basi  asiiname kama anavyoinama ngamia. Atangulize mikono yake kabla ya magoti yake.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mikono inasujudu kama unavyosujudu uso. Pindi mmoja wenu anapoweka uso wake chini basi na aweke mikono yake chini na wakati anapoinyanyua basi na ainyanyue.”[3]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiviweka chini viganja vyake vya mikono, akivitanua[4], akibana vidole vyake pamoja[5] na akivielekeza Qiblah[6].

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiiweka mikono yake usawa wa mabega yake[7] na wakati mwingine usawa wa masikio yake[8].

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiiweka mikono yake na pua yake katika ardhi[9]. Alisema kumwambia yule mtu aliyeswali kimakosa:

“Unaposujudu basi makinika katika Sujuud yako.”[10]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Unapoenda katika Sujuud basi weka uso wako na mikono yako mpaka kila mfupa utulie mahala pake.”[11]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hana swalah yule asiyeweka pua yake ardhini kama anavyoweka paji la uso.”[12]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile akiweka magoti yake na ncha za vidole vyake vya miguuni ardhini[13].

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akivipindisha na kuelekeza ncha za vidole vya miguu yake Qiblah[14].

Akiweka (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) visigino vyake pamoja[15], akiinyanyua miguu yake[16], akiamrisha kufanya hivo[17] na akipindisha vidole vyake vya miguuni[18].

Hivi ndivyo viungo saba ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisujudu juu yake: vitanga viwili vya mikono, magoti, miguu, paji la uso na pua. Amefanya viungo viwili hivyo vya mwisho vilivyotajwa kuwa kiungo kimoja katika Sujuud pale aliposema:

“Nimeamrishwa (katika upokezi mwingine “Tumeamrishwa”) kusujudu juu ya viungo saba; juu ya paji la uso – na akaashiria kwa mkono wake kwenye pua yake – mikono (katika upokezi mwingine “vitanga vya mikono”), magoti na ncha za vidole vya miguu na wala tusikunje nguo[19] na nywele.”[20]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mja anaposujudu basi vinasujudu pamoja naye viungo saba: uso wake, vitanga vya vya mikono, magoti yake na miguu yake.”[21]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona mwanamume akiswali hali ya kuwa amefunga nywele kwa nyuma yake na akasema:

“Hakika mfano wa huyu ni kama mfano wa mwenye kuswali hali ya kuwa amefunga [mikono yake].”[22]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile:

“Haya ni makazi ya shaytwaan.”[23]

Bi maana mafundo yale yaliyofungwa.

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hailazi mikono yake ardhini[24]. Bali alikuwa akiinyanyua mbali na ardhi na akiiweka mbali na mbavu zake kiasi cha kwamba mtu alikuwa anaweza kuona weupe wa kwapa zake kwa nyuma[25] na pia kiasi cha kwamba endapo mtoto wa mbuzi angelitaka kupita chini ya mikono yake basi angeliweza kufanya hivo[26]. Alikuwa akipea kufanya hivo mpaka wakisema baadhi ya Maswahabah wake:

“Tulikuwa tukimuonea huruma Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa namna anavyoiweka mikono yake mbali na mbavu zake pindi anaposujudu.”[27]

Ameamrisha hilo na kusema:

“Unaposujudu weka viganja vyako chini na inua viwiko vyako.”[28]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyooka katika Sujuud. Asiilaze yeyote mikono yake kama mbwa.”[29]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Asiilaze yeyote mikono yake kama mbwa.”[30]

Katika tamko jingine amesema vilevile:

“Msiitandaze mikono yenu kama atandazavyo mbuai. Jitegemeze juu ya vitanga vyako na iweke mbali mikono yako. Kwani ukifanya hivo basi kila kiungo kitasujudu na wewe.”[31]

[1] Ibn Khuzaymah (1/76/1) na ad-Daaraqutwniy, al-Haakim ambaye ameisahihisha na na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Hadiyth zote zinazoipinga hii sio Swahiyh. Hayo ndio maoni alionayo Maalik na imenasibishwa vilevile kwa Ahmad, kama ilivyotajwa katika “at-Tahqiyq” (2/108) ya Ibn-ul-Jawziy. al-Marwaziy amepokea kwa mlolongo w wapokezi Swahiyh ya kwamba Imaam al-Awzaa´iy amesema:

“Nimewaona watu wakitanguliza mikono kabla ya magoti.”

[2] Abu Daawuud, Tammaam katika ”al-Fawaa-id” (1/108) na an-Nasaa’iy katika ”as-Sughraa” na ”al-Kubraa” (1/47) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. ´Abdul-Haq ameisahihisha katika “al-Ahkaam al-Kubraa” (1/54). Amesema:

“Ina mlolongo wa wapokezi bora kuliko ya nyuma yake.” (1/56)

Bi maana Hadiyth ya Waa-il inayopingana nayo. Pamoja na kuwa inapingana na Hadiyth hii Swahiyh na Hadiyth iliyo kabla yake si Swahiyh inapokuja katika mlolongo wa wapokezi wake. Inahusiana vilevile na Hadiyth nyenginezo zote zilizo na maana kama hiyo. Hayo nimeyabainisha katika “adh-Dhwa´iyfah” (929) na “al-Irwaa´” (357)

Kujitofautisha na ngamia kwa kutanguliza mikono kwanza kabla ya magoti ni kwa sababu ngamia hutanguliza magoti kwanza, kama ilivyotajwa katika “Lisaan-ul-´Arab” na vitabu vyengine vya kiarabu. Vivyo hivyo ndivyo alivyosema at-Twahaawiy katika “Mushkil-ul-Aathaar” na “Sharh Ma´aaniyl-Aathaar” na Imaam as-Saraqastwiy (Rahimahu Allaah). Amepokea kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh ya kwamba Abu Hurayrah amesema:

“Asipige magoti mtu kama anavyofanya ngamia anayekimbia.” (Ghariyb-ul-Hadiyth (2/70/1-2))

Imamu akasema:

“Hili linahusiana na Sujuud. Hatakiwi kujitupa kama anavyojitupa ngamia mwenye wasiwasi anayekimbia. Bali anatakiwa aende chini polepole na hali ya kutulia kwa kutanguliza mikono kabla ya magoti, kama ilivyopokelewa wazi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Halafu akataja Hadiyth iliyo juu. Ibn-ul-Qayyim amezungumza maneno ya ajabu aliposema:

“Maneno haya hayaeleweki na hayafahamiki kwa mabingwa wa lugha.”

Anaraddiwa na vile vyanzo tulivyovitaja na vyengine unavyoweza kuvirejelea. Nimelibainisha hilo kwa undani zaidi katika Radd yangu dhidi ya Shaykh at-Tuwayjiriy ambayo huenda ikachapishwa.

[3] Ibn Khuzaymah (2/79/1), Ahmad na as-Sarraaj. al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (313).

[4] Abu Daawuud na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[5] Ibn Khuzaymah, al-Bayhaqiy na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[6] al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Kwa Ibn Abiy Shaybah (2/82/1) na as-Sarraaj wamelenga kuelekeza vidole kupitia upokezi mwingine.

[7] Abu Daawuud na at-Tirmidhiy aliyeisahihisha pamoja na Ibn-ul-Mulaqqin (2/27). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (309).

[8] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[9] Abu Daawuud na at-Tirmidhiy aliyeisahihisha pamoja na Ibn-ul-Mulaqqin (2/27). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (309).

[10] Abu Daawuud na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[11] Ibn Khuzaymah (1/10/1) kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

[12] ad-Daaraqutwniy, at-Twabaraaniy (1/140/3) na Abu Nu´aym katika ”Akhbaar Aswbahaan”.

[13] al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Kwa Ibn Abiy Shaybah (2/82/1) na as-Sarraaj wamelenga kuelekeza ncha za vidole kupitia upokezi mwingine. al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[14] al-Bukhaariy na Abu Daawuud. Nyongeza imepokelewa na Ibn Raahuuyah katika ”al-Musnad” (2/129/4). Ibn Sa´d (4/157) amepokea ya kwamba Ibn ´Umar alipenda kukielekeza Qiblah kila kiungo chake cha mwili, hata vidole gumba, wakati anaposwali.

[15] at-Twahaawiy, Ibn Khuzaymah (654) na al-Haakim ambaye kaisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[16] al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[17] at-Tirmidhiy na as-Sarraaj. al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[18] Abu Daawuud, at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah.

[19] Bi maana nguo hazitakiwi kushikwa na mikono wakati wa Rukuu´ na Sujuud, amesema Ibn-ul-Athiyr katika “an-Nihaayah”.

[20] al-Bukhaariy na Muslim. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (310).

[21] Muslim, Abu ´Awaanah na Ibn Hibbaan.

[22] Muslim, Abu ´Awaanah na Ibn Hibbaan. Ibn-ul-Athiyr amesema:

“Maana ya Hadiyth ni kwamba iwapo nywele zake zingelikuwa zimeachwa basi zingelianguka ardhini katika Sujuud, jambo ambalo analipwa thawabu kwalo. Lakini zikifungwa inahesabika hazikusujudu. Amemfananisha na mtu ambaye mikono yake imefungwa kwa sababu haigusi ardhini katika Sujuud.”

Inaonekana hukumu hii inawahusu wanaume peke yao na sio wanawake, kama ash-Shawkaaniy alivyonukuu kutoka kwa Ibn-ul-´Arabiy.

[23] Abu Daawuud na at-Tirmidhiy aliyesema kuwa ni nzuri. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan wote wawili wameisahihisha. Imetajwa katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (653).

[24] al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[25] al-Bukhaariy na Muslim. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (359).

[26] Muslim, Abu ´Awaanah na Ibn Hibbaan.

[27] Abu Daawuud na Ibn Maajah kwa mlolongo wa wapokezi ulio mzuri.

[28] Muslim na Abu ´Awaanah.

[29] al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na Ahmad.

[30] Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha.

[31] Ibn Khuzaymah (2/80/1), al-Maqdisiy katika ”al-Mukhtaarah” na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 122-126
  • Imechapishwa: 04/08/2017