55. Hatumshuhudilii muislamu yeyote kuwa ataingia Peponi wala Motoni


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatumshuhudii muislamu yeyote kwa kitendo alichofanya kuingia Peponi wala Motoni. Tunatarajia kwake mema na tunachelea kwake. Tunachelea kwa mtenda dhambi na tunatarajia kwake huruma ya Allaah.”

MAELEZO

Amesema:

“Hatumshuhudii muislamu yeyote kwa kitendo alichofanya kuingia Peponi wala Motoni.”

Bi maana midhali dhambi sio kufuru. Ikiwa dhambi ni kufuru au shirki, ina hukumu yake. Ama dhambi ikiwa ni maasi tu, hatumshuhudilii Pepo wala Moto. Akifanya matendo mema tunatarajia kwake Pepo. Akifanya matendo yanayopelekea katika Moto, tunachelea kwake. Tunatarajia kwa yule mwenye kutii na tunachelea kwa mtenda maasi. Hatumkatii yeyote Pepo wala Moto. Hakuna mwenye haki ya kufanya hivo isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) peke yake. Isipokuwa tu kufuru ya wazi. Myahudi au mnaswara ni makafiri, ni jambo liko wazi. Mtu kama huyu ataingia Motoni. Tunashuhudia ya kwamba kafiri ataingia Motoni. Ni muumini, ambaye ni mtenda maasi au mwenye kutii, ndiye ambaye hatumshuhudilii si Pepo wala Moto. Jambo lake liko kwa Allaah (´Azza wa Jall). Tunamtarajia yule mwenye kutii na tunachelea kwa yule mwenye kuasi. Tunatarajia kwa yule mwema na wakati huohuo tunachelea juu yake. Kwa sababu kuna uwezekano anafanya matendo mema kwa uinje na kwa undani ni kinyume kabisa na hivo. Ni jambo limetokea hapo kabla. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu mwanamume aliyewaua maadui:

“Yuko Motoni.”[1]

Uinje wake alikuwa mpambanaji, lakini nia ilikuwa kitu kingine.

Vivyo hivyo inahusiana na yule mtu aliyepigwa mshale. Maswahabah wakasema kuwa ni shahidi ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Kamwe! Kishuka cha juu alichochukua katika mateka bila ya idhini kinamuunguza Motoni.”[2]

Umm-ul-´Alaa´ alikuwa akimtunza ´Uthmaan bin Madh´uun. Alipofariki akasema:

“Allaah akukirimu, ee Abuul-Saaib! Nashuhudia ya kwamba amekukirimu.” Ndipo Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unajuaje kuwa Allaah amemkirimu? Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mimi ni Mtume wa Allaah lakini sijui ni kipi kitanipitikia.” Akasema: “Baada ya hapo sikumtakasa yeyote zaidi.” Kisha akaota namna alivyo na chemchem inayopita. Mwanamke huyo akamueleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Hayo ni matendo yake.”[3]

Tunachotaka kusema ni kwamba usimshuhudilii yeyote Pepo wala Moto.”

[1] al-Bukhaariy (4203) na Muslim (111).

[2] al-Bukhaariy (4234) na Muslim (115).

[3] al-Bukhaariy (2687).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 431-432
  • Imechapishwa: 10/12/2017