55. al-Ash´ariy alikuwa na ´Aqiydah ya Ahl-ul-Hadiyth

68- Imaam Abul-Hasan ´Aliy bin Ismaa´iyl al-Ash´ariy amesema baada ya kutaja ´Aqiydah ya Khawaarij, Raafidhwah na Jahmiyyah:

“Huu ndio msemo wa ´Aqiydah ya Ahl-ul-Hadiyth na Ahl-us-Sunnah. Miongoni mwa jumla ya yale ambayo Ahl-ul-Hadiyth was-Sunnah wanaamini ni kumthibitisha Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kila kilichosemwa na Allaah na wapokezi waaminifu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawarudishi chochote katika hayo.

Mpaka aliposema:

“Wanathibitisha kuwa Allaah Yuko juu ya ´Arshi Yake, kama alivosema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa huruma amelingana juu ya ‘Arshi.”[1]

Na kwamba Ana mikono miwili isiyotakiwa kufanyiwa namna, kama alivosema:

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“Kipi kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa mikono Yangu?”[2]

na:

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali mikono Yake imefumbuliwa.”[3]

Na kwamba Ana macho mawili yasiyotakiwa kufanyiwa namna, kama alivosema:

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا

“Inatembea chini ya macho Yetu.”[4]

Na kwamba Ana uso, kama alivosema:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

“Kila aliyekuwa juu yake [ardhi] ni mwenye kutoweka na utabakia uso wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu.”[5]

Mpaka aliposema:

“Yote niliyotaja kuhusu wao ndio ´Aqiydah yangu ninayoonelea.”

Haya yametajwa na Abu Bakr bin Fawrak katika kitabu  ”al-Khilaaf bayn Ibn Kullaab wal-Ash´ariy”. Akasema pia mwishoni mwa maandishi:

“Haya yanakuthibitishia kwamba Abul-Hasan ´Aliy bin Ismaa´iyl al-Ash´ariy alikuwa ni mwenye kuitakidi misingi hii ambayo ndio kanuni za Ahl-ul-Hadiyth na misingi ya Tawhiyd yao.”

69- Imaam Abu Sulaymaan al-Khattwaabiy amesema:

“Madhehebu ya Salaf katika Aayah na Hadiyth zinazoongelea sifa ni kuzipitisha kwa udhahiri wake na kupinga namna na ufanano.”

70- Haafidhw Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy bin Thaabit al-Khatwiyb amesema:

“Kuhusu sifa zilizosihi kupokelewa katika Sunnah Swahiyh, madhehebu ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) ni kuzithibitisha na kuzipitisha kwa udhahiri wake na kupinga namna na ufanano. Mlango huu umejengwa juu ya kwamba kuzungumzia sifa ni kama kuzungumzia dhati.

Ni jambo linalotambulika kwamba kumthibitisha Mola (´Azza wa Jall) ni kuthibitisha juu ya uwepo Wake, sio kuthibitisha ukomo wala namna, vivyo hivyo kuthibitisha sifa Zake ni kuthibitisha uwepo wazo, sio kuthibitisha ukomo wala namna.

Tunaposema kuwa Allaah (Ta´ala) yuko na mkono, usikizi na uoni, hivyo tumemthibitishia Allaah sifa ambazo amejithibitishia Mwenyewe. Hatusemi kuwa maana ya mkono ni nguvu wala kusikia na kuona maana yake ni elimu.”

[1] 20:05

[2] 38:75

[3] 05:64

[4] 54:14

[5] 55:26-27 [5]

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaat-ul-Yad li-Laah Swifatan min Swifwaatih, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 18/07/2019