54. Yanayosemwa na Ahmad, at-Tirmidhiy na Ibn Khuzaymah

65- Hanbal amesema:

“Nilimuuliza Abu ´Abdillaah juu ya Hadiyth kama:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anashuka kwenye mbingu ya chini ya dunia.”

 “Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kwa macho yenu kama mnavyoona mwezi mwandamo na kwenye usiku usiokuwa na mawingu.”

“Mpaka pale Allaah atapoweka unyayo Wake juu yake ambapo utasema: “Inatosha, inatosha.”

Abu ´Abdillaah akasema: “Tunaziamini na tunazisadikisha bila kuzifanyia namna wala maana. Wala haturudishi chochote katika hayo ikiwa zina cheni ya wapokezi Swahiyh. Haturudishi sifa miongoni mwa sifa Zake kwa sababu ya matusi.”

66- at-Tirmidhiy amesema:

“Wanachuoni wengi wamesema kuhusu Hadiyth hii na mapokezi mfano wake zinazoongelea sifa za Allaah na Mola (Tabaarak wa Ta´ala) kushuka kwenye mbingu ya chini ya dunia kama ni Swahiyh. Mtu anatakiwa kuziamini zote bila ya kuzifanyia namna wala kuhoji. Haya yamepokelewa kutoka kwa Maalik bin Anas, Sufyaan bin ´Uyaynah na ´Abdullaah bin al-Mubaarak ambao wamesema:

“Zipitisheni Hadiyth hizi bila ya kuzifanyia namna.”

Haya yamesemwa na wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Ama kuhusu Jahmiyyah wameyapinga mapokezi haya na kusema kwamba huko ni kufananisha. Allaah mara nyingi ametaja mkono, uoni na usikivu kwenye Kitabu Chake. Hata hivyo Jahmiyyah wanazifasiri kwa njia nyingine ambayo haikufasiriwa na wanachuoni na wanasema:

“Allaah hakumuumba Aadam kwa mkono Wake. Maana ya mkono ni nguvu.”

Wanachuoni wamesema:

“Hizi ni sifa Zake. Kufananisha ni pale mtu ataposema usikizi kama usikizi, mkono kama mkono.”

67- Imamu wa maimamu Abu Bakr Muhammad bin Khuzaymah amesema:

“Khabari zilizopokelewa katika sifa ni zenye kuafikiana na Qur-aan. Vizazi vilivyokuja nyuma vimezipokea kutoka kwa vizazi vilivyotangulia, kutoka kwa Maswahabah na Taabi´uun katika wakati wetu, kwa njia ya kwamba ni sifa za Allaah (Ta´ala). Mtu anatakiwa kuwa na utambuzi Naye, kumuamini na kujisalimisha juu ya yale Aliyoeleza (Ta´ala) katika Wahy pamoja na yale yaliyoelezwa na Mtume na Nabii Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Shari´ah Yake. Mtu afanye hivo bila ya kupindisha maana na kukanusha, kutomfanyia namna na kumfananisha.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaat-ul-Yad li-Laah Swifatan min Swifwaatih, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 14/07/2019