55- Kusimama kwa ajili ya majeneza ni jambo limefutwa. Zipo aina mbili:

1- Kusimama ambaye ameketi chini pindi linapopitishwa.

2- Wale wasindikizaji kuyasimamia pale wanapoishilia kulifikisha kaburini mpaka waliweka ndani ya ardhi.

Dalili ya hilo ni Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambayo ina matamshi mbalimbali:

La kwanza: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama kwa ajili ya jeneza nasi tukasimama. Kisha akakaa chini nasi tukakaa chini.”

Ameipokea Muslim (03/59), Ibn Maajah (01/468), at-Twayaalisiy (01/383), at-Twayaalisiy (150) na Ahmad nambari. (631, 1094, 1167).

Ya pili: “Alikuwa akisimama katika jeneza kisha baada ya hapo anakaa.”

Ameipokea Maalik (01/332), ash-Shaafi´iy amepokea kutoka kwake katika “al-Umm” (01/247), Abu Daawuud (02/64).

La tatu: Kupitia kwa Waaqid bin ´Amr bin Sa´d bin Mu´aadh ambaye amesema:

“Nilihudhuria jeneza katika Banuu Salamah ambapo nikasimama. Naafiy´ bin Jubayr akasema: “Keti chini! Hakika mimi nitakupasha khabari ya dhati kabisa. Mas´uud bin al-Hakam az-Zuraqiy amenihadithia  kwamba yeye amemsikia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) akiwa katika uwanja wa Kuufah akisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akituamrisha kuyasimamia majeneza kisha baada ya hapo akawa anakaa na akatuamrisha nasi kukaa.”

Ameipokea ash-Shaafi´iy na Ahmad (627), at-Twahaawiy (01/282), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake.

Pia ameipokea al-Haazimiy katika “al-I´tibaar”, uk. 91 kwa cheni ya wapokezi nzuri, vilevile ameipokea al-Bayhaqiy (04/27) kupitia sura kama hii kwa tamko lingine. Nalo ni:

La nne: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyasimamia majeneza mpaka yawekwe chini na watu walikuwa wakisimama pamoja naye. Kisha akikaa kitako baada ya hapo na akiwaamrisha kukaa kitako.”

La tano: Kupitia kwa Ismaa´iyl bin Mas´uud[1] az-Zuraqiy kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

“Nilihudhuria jeneza ´Iraaq na nikawaona watu wamesimama wakisubiri liwekwe ndani. Nikamuona ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) akiwaashiria waketi chini. Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituamrisha tuketi chini baada ya kusimama.”

Ameipokea at-Twayaalisiy (01/282) kwa cheni ya wapokezi nzuri.

Tamko hili na lililo kabla yake yako wazi kwamba kuyasimamia mpaka yawekwe ni jamlo linaloingia katika makatazo na kwamba limefutwa. Maneno ya Swiddiyq Hasan al-Khaan katika “ar-Rawdhwah” (01/176) baada ya kuthibitisha kwamba kuyasimamia ni jambo limefutwa pindi linapopitishwa:

“Kuhusu jambo la watu kulisimamia kwa nyuma yake mpaka liwekwe ardhini hukumu yake haikufutwa.”

Hili ni kosa la wazi. Kwa sababu linakwenda kinyume na yale tuliyotaja katika matamshi mawili. Kilicho dhahiri ni kwamba hakuyaona.

56- Imependekezwa kwa mwenye kulibeba atawadhe kwanza. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayemuosha maiti basi aoge na yule atakayembeba atawadhe.”

Hadiyth hii ni Swahiyh, kama ulivyotangulia ubainifu wake katika masuala ya 31.

[1] Katika kitabu cha asili imetokea Ismaa´iyl bin al-Hakam bin Mas´uud. Sahihi ni kama nilivyothibitisha. Kana kwamba hili liligeuzika wakati wa kuchapisha au baadhi ya nuskha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 101-102
  • Imechapishwa: 14/07/2020