54. Maana ya kwamba Muhammad (صلى الله عليه وسلم) ni Mtume wa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah maana yake ni kumtii katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha kwa yale aliyoeleza, kujiepusha yale aliyokataza na kuyakemea na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale Aliyoyawekea Shari´ah.

MAELEZO

Maana ya kushuhudia kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ni kukiri kwa mdomo na kuamini kwa moyo ya kwamba Muhammad bin ´Abdillaah al-Qurashiy al-Haashimiy ni Mtume wa Allaah (´Azza wa Jall) kwa viumbe vyote, kati ya majini na watu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (adh-Dhaariyaat 51 : 56)

Hata hivyo ´ibaadah haiwi sahihi kwa Allaah (Ta´ala) ikiwa haiafikiani na Wahy uliyokuja na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَىٰ عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.” (al-Furqaan 25 : 01)

Ushuhudiaji huu unapelekea kumsadikisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoyaeleza, kutekeleza amri zake kwa yale aliyoamrisha, kujiepusha na yale aliyokataza na kuyakemea na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale aliyoyawekea Shari´ah. Kitu kingine kinachopelekea katika shahaadah hii, ni mtu kutoamini kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  ana haki yoyote katika uola, kuendesha ulimwengu au haki yoyote katika ´ibaadah. Bali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mja asiyeabudiwa na ni Mtume asiyekadhibishwa. Hamiliki chochote, katika manufaa wala madhara, juu ya nafsi yake yeye wala nafsi ya mtu mwengine isipokuwa kwa yale anayotaka Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ

“Sema: “Sikuambieni kuwa mimi nina hazina ya Allaah; na kwamba najua ghaibu na wala sikuambieni kuwa mimi ni Malaika. Si vyenginevyo sifuati isipokuwa yale niloletewa Wahy.”” (al-An´aam 06 : 50)

Kwa haya inapata kufahamika kwamba hakuna yeyote anayestahiki kuabudiwa. Ni mamoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengineo aliye chini yake katika viumbe na kwamba ´ibaadah hafanyiwi isipokuwa Allaah pekee:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu. Hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza [kujisalimisha].” (al-An´aam 06 : 162-163)

na kwamba haki yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kumuweka ile daraja aliyowekwa na Allaah (Ta´ala); nayo ni kwamba yeye ni mja na Mtume wa Allaah – swalah na amani ziwe juu yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 75
  • Imechapishwa: 30/05/2020