54. Inajuzu kuwapiga vita wezi na Khawaarij

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inafaa kuwapiga vita wezi na Khawaarij. Wakimshambulia mtu au mali yake basi inafaa kwake kupambana kwa ajili ya nafsi yake na mali yake. Ajitetee kwa yote ayawezayo. Hata hivyo haifai kwake kuwafuata au kuwatafuta wakimuacha.  Hakuna mwingine isipokuwa kiongozi au mtawala wa waislamu ndiye anayeweza kufanya kitu kama hicho. Ana haki tu ya kujitetea mahala hapo. Anuie kutomuua yeyote. Ikitokea wakati wa kuitetea nafsi yake akamuua yule mshambulizi, basi atajaza yule mshambulizi. Na ikitokea yeye ndiye akafa wakati yuko anaitetea nafsi yake na mali yake, kunatarajiwa kwake kufa shahidi. Hivyo ndivyo ilivyotajwa katika Hadiyth na mapokezi. Vinaamrisha tu kujitetea na wala haviamrishi yule mshambulizi kuuawa wala kufuatwa. Wala usimalize uhai wake endapo ataanguka chini au akapata majeraha. Hafai vilevile kwake kumuua wala kumsimamishia adhabu iwapo atamkamata. Badala yake anatakiwa kumpeleka mahakamani na awaache wamuhukumu.”

MAELEZO

Huu ni upambanuzi unaozungumzia namna ambavyo Khawaarij, majambazi na wafanya fujo wanavyotakiwa kupigwa vita. Yamejengwa juu ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna mtu alimuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Unaonaje lau atakuwepo mtu anayetaka kuchukua mali yangu?” Akasema: “Usimpe.” Akauliza: “Vipi ikiwa atanipiga vita?” Akasema: “Mpige vita.” Akauliza: “Vipi ikiwa ataniua?” Akasema: “Unakuwa shahidi.” Akauliza: “Vipi ikiwa mimi ndiye nitamuua?” Akasema: “Anaingia Motoni.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kuuawa kwa sababu ya mali yake ni shahidi. Mwenye kuuawa kwa sababu ya kuitetea heshima yake ni shahidi. Mwenye kuuawa kwa sababu ya dini yake ni shahidi.”[2]

Mtu akishambuliwa kwenye mali yake au kwa wanawake wake au kwenye nafsi yake mwenyewe, anatakiwa ajitetee kiasi na uwezo wake pasi na kunuia mauaji. Ikipelekea akatokea kumuua yule mshambulizi basi apuuzilie mbali. Akiuawa basi anakuwa shahidi. Shari´ah imemjuzishia yule mshambuliwaji kuitetea mali yake, heshima yake na nafsi yake. Bali baadhi ya wanachuoni wanasema kuwa ni wajibu kuwatetea wake zake na dada zake. Kwa hiyo ni wajibu kuwatetea dada zake. Ikiwa inatosha kwa makabiliano madogo yawezekanayo basi ni vizuri. Mambo yakipelekea katika kumuua hana dhambi na wakati huo huo yule muuliwaji anaingia Motoni. Mvamiwaji akiuawa basi ni shahidi – Allaah akitaka. Hata hivyo anatakiwa kufanya hivo kwa ajili ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na kushikamana na Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) na sio kuitetea nafsi yake peke yake. Kwani matendo yanalipwa kutegemea na nia.

Imaam Ahmad ameyajenga masuala haya juu ya Hadiyth hizi. Anakusudia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameruhusu kujitetea na sio kumuua. Amesunisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kujitetea na sio kuua. Pia na wewe usinuie kumuua. Unachotakiwa ni kunuia kujihami. Akikoma, ni sawa. Asipoacha isipokuwa baada ya kumuua basi hukumu ni yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huyu mshambulizi anaingia Motoni na yule mshambuliwaji akiuawa anakuwa shahidi.

Usimuue endapo utamkamata au akajeruhiwa. Huna haki yoyote ya kumaliza uhai wake. Akikimbilia huna haki ya kumkimbiza. Shari yake imeisha na hilo ndilo lengo. Ima aanguke hali ya kuumia au akimbie. Katika hali hiyo usimfuate. Akianguka hali ya kuumia usimmalizie. Haifai kwako kufanya hivo. Ukifanya hivo basi umevuka mpaka. Umeamrishwa kuitetea nafsi yako na sio kumuua. Ukimkamata basi usimuue na wala usimsimamishie adhabu ya Kishari´ah. Anatakiwa kupelekwa mahakamani ambapo atasimamishiwa hukumu ya Allaah au kile wanachoona kuwa ndio cha sawa. Mahakama ndio ina majukumu ya makosa watayofanya.

[1] Muslim (140).

[2] at-Tirmidhiy (1421) na Abu Daawuud (4772). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 429-430
  • Imechapishwa: 08/12/2017