54. Baadhi ya fadhilah za wajukuze, wana na wakeze Mtume na Mu´aawiyah

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

وسبطي رسول الله وابني خديجة

21 – Vilevile wajukuze Mtume wa Allaah na wana wa Khadiyjah

وفاطمة ذات النقاء تبحبحوا

     na Faatwimah mwenye kusifiwa

وعائشـة أم المؤمنين وخالنـا

22 – Vilevile na ´Aaishah ambaye ni mama wa waumini, na mjomba wetu

معـاوية أكـرم به ثم امـنح

    ambaye si mwengine ni Mu´aawiyah muheshimiwa

MAELEZO

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Wajukuze Mtume wa Allaah.”

Bi maana al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa). al-Hasan na al-Husayn ni wajukuze wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bi maana ni watoto wa msichana wake Faatwimah. Wao ndio:

“Viongozi wa vijana wa Peponi.”[1]

kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… wana wa Khadiyjah.”

Watoto wote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanatokamana na Khadiyjah. Isipokuwa Ibraahiym peke yake. Yeye mama yake ni Maariyah Qibtwiyyah. Kuhusu watoto wengine wote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanatokamana na Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Alizaa nae wavulana wawili waliokufa katika uhai wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mji wa Makkah.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na Faatwimah.”

Faatwimah ambaye ni binti yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anampenda. Faatwimah alipokuwa anafika anasimama kwa ajili yake na kumbusu na kumkalisha pembezoni nae.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Vilevile na ´Aaishah ambaye ni mama wa waumini… “

Yeye ndiye mwanamke aliyekuwa akipendwa zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwanaume aliyekuwa akipendwa zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni baba yake ambaye ni Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh)[2].

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… mjomba wetu ambaye si mwengine ni Mu´aawiyah.”

Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhiya Allaahu ´anh). Huyu alikuwa ni Swahabah mtukufu. Alikuwa ni mwandishi wa Wahy. Alikuwa akimwandikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qur-aan. Alikuwa ni mjomba wa waumini kwa sababu dada yake, ambaye ni Umm Habiybah, ni mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo yeye anakuwa ni mjomba wa waumini. Bi maana yeye ni kaka wa mama wa waumini. Hizi ni katika fadhilah zake (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] Kuna idadi kubwa ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao wamepokea Hadiyth hii mpaka as-Suyuutwiy akasema: “Hili ni jambo limepokelewa kwa njia nyingi.” Faydhw-ul-Qadiyr (03/415)

[2] Ameyapokea haya al-Bukhaariy (4358) na (3662) na Muslim (08) na (2384)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 127-128
  • Imechapishwa: 10/01/2024