54. Baadhi ya fadhila za wajukuze, wana na wakeze Mtume na Mu´aawiyah


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

21- Vilevile wajukuze Mtume wa Allaah na wana wa Khadiyjah

     na Faatwimah ambaye alikuwa mtakasifu

22- Vilevile na ´Aaishah ambaye ni mama wa waumini na mjomba wetu

    ambaye si mwengine ni Mu´aawiyah muheshimiwa

MAELEZO

Wajukuze Mtume wa Allaah – Bi maana al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa). al-Hasan na al-Husayn ni wajukuze wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bi maana ni watoto wa msichana wake Faatwimah. Wao ndio:

“Viongozi wa vijana wa Peponi.”[1]

kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

… wana wa Khadiyjah – Watoto wote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanatokamana na Khadiyjah. Isipokuwa Ibraahiym peke yake. Yeye mama yake ni Maariyah Qibtwiyyah. Kuhusu watoto wengine wote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanatokamana na Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Alizaa nae wavulana wawili waliokufa katika uhai wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mji wa Makkah.

na Faatwimah – Faatwimah ambaye ni binti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anampenda. Faatwimah alipokuwa anafika anamsimamia na kumbusu na kumkalisha pembezoni nae.

Vilevile na ´Aaishah ambaye ni mama wa waumini… – Yeye ndiye mwanamke aliyekuwa akipendwa zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwanaume aliyekuwa akipendwa zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni baba yake ambaye ni Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh)[2].

… mjomba wetu ambaye si mwengine ni Mu´aawiyah – Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhiya Allaahu ´anh). Huyu alikuwa ni Swahabah mtukufu. Alikuwa ni mwandishi wa Wahy. Alikuwa akimwandikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qur-aan. Alikuwa ni mjomba wa waumini kwa sababu dada yake ambaye ni Umm Habiybah ni mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo yeye anakuwa ni mjomba wa waumini. Bi maana yeye ni kaka wa mama wa waumini. Hizi ni katika fadhila zake (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] Kuna idadi kubwa ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao wamepokea Hadiyth hii mpaka as-Suyuutwiy akasema: “Hili ni jambo limepokelewa kwa njia nyingi.” Faydhw al-Qadiyr (03/415)

[2] Ameyapokea haya al-Bukhaariy (4358) na (3662) na Muslim (08) na (2384)