54. ´Aqiydah ya Ashaa´irah ina mizizi katika ´Aqiydah ya Jahmiyyah


Qur-aan Tukufu ni miongoni mwa maneno Yake, matamshi na maana yake.

Jahmiyyah wanasema kuwa matamshi na maana yake vyote viwili vimeumbwa.

Ashaa´irah wanasema kuwa matamshi yake yameumbwa lakini maana yake haikuumbwa. Wanaona kuwa maana imesimama ndani ya nafsi Yake na baadaye ikaabiriwa na Jibriyl. Hivyo Qur-aan ni ibara au simbulizi juu ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). ´Aqiydah hii pia ina mizizi katika ´Aqiydah ya Jahmiyyah. Tofauti pekee ni kwamba Ashaa´irah wanasema kuwa maana ya Qur-aan haikuumbwa. Lakini mapote yote mawili yanaamini kuwa matamshi yake yameumbwa.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah, ni mamoja matamshi na maana yake, kwa njia inayolingana na utukufu Wake (´Azza wa Jall). Maneno na sifa nyenginezo zote ni kamilifu. Kile kisichozungumza kina upungufu – Allaha ametakasika kutokamana na yale wanayoyasema!

Wakati wana wa israaiyl walipomwabudu ndama waliotengenezewa na Saamiriy, Allaah (Ta´ala) akasema:

أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا

“Je, hawakuona kwamba hawasemezi na wala hawaongozi njia?”[1]

Ni dalili inayojulisha kuwa Allaah huwazungumzisha waja Wake. Kitu kisichozungumza hakina uhai. Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alisema kumwambia baba yake:

يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا

“Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote?”[2]

Ni dalili inayofahamisha kwamba kile kisichosikia, kisichoona wala kuzungumza hakistahiki kuabudiwa. Kumthibitishia Allaah sifa hakupelekei kwamba eti sifa Zake zinafanana na sifa za viumbe. Majina na sifa za Allaah hazifanani na majina na sifa za viumbe Wake. Wala maneno ya Allaah hafanani na maneno ya viumbe. Sifa za viumbe ni zenye kulingana na wao na sifa za Allaah ni zenye kulingana Naye. Kuna tofauti kati ya sifa hizi na zile. Haya ndio yaliyoashiriwa na mtunzi (Rahimahu Allaah) pale aliposema:

“Qur-aan ni manneo ya Allaah. Haikuumbwa ili imalizike wala sio sifa ya kiumbe ili itokomee.”

Injiyl na Tawraat ni maneno ya Allaah. Maneno Yake ni zaidi kuliko haya. Qur-aan haikuumbwa tofauti na wanavosema Jahmiyyah. Viumbe humalizika na hutokomea. Katika hali hiyo ni kwamba Qur-aan itatokomea. Mambo sivyo kabisa. Hakuna chochote katika maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) ambacho hutokomea.

Wala Qur-aan sio sifa ya kiumbe. Hapa wanaraddiwa wale wanaosema kuwa Qur-aan imetamkwa na Jibriyl na pia ni Radd kwao kwa njia ya kwamba endapo mambo yangelikuwa hivo basi ingelikuwa ni sifa ilioumbwa. Sifa ya kiumbe inamalizika tofauti na maneno ya Allaah yasiyomalizika na kutokomea. Amesema (Ta´ala):

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا

“Sema: “Endapo bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandika] maneno ya Mola wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu ijapo tungelileta mfano wake kujaza tena.”[3]

Maneno ya Allaah hayamaliziki na kutokomea kama ambavyo zilivyo sifa Zake zingine zote.

[1] 7:148

[2] 19:42

[3] 18:109

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 03/08/2021