53. Uwajibu wa kutulizana baada ya Rukuu´


Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anafanya kusimama kwake huku kunakuwa kurefu kunakokaribia na urefu wa Rukuu´ yake. Alikuwa wakati mwingine anaweza kukirefusha mpaka wanasema:

“Amesahau.”[1]

Ameamrisha kutulizana ndani yake na alisema kumwambia yule mtu aliyeswali kimakosa:

“Halafu kiinue kichwa chako mpaka uti wa mgongo unyooke sawasawa na kila mfupa urudi mahala pake.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Unapoinuka unyooshe mgongo wako na kiinue kichwa chako mpaka mifupa irudi mahala pake.”[2]

Akamweleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba hakuna swalah ya yeyote inayotimia mpaka afanye hivo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) haitazami swalah ya mja ambaye hanyooshi uti wa mgongo wake baina ya Rukuu´ na Sujuud yake.”[3]

[1] al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad. Imetajwa katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (307).

[2] Sentesi ya kwanza pekee imepokelewa kwa al-Bukhaariy na Muslim. Iliyobaki inapatikana kwa ad-Daarimiy, al-Haakim, ash-Shaafi´iy na Ahmad.

Uzinduzi

Maana ya Hadiyth hii iko bayana na wazi; nayo ni kutulizana katika kisimamo hichi. Baadhi ya ndugu zetu Saudi Arabia na kwenginepo wanatumia hoja kwa Hadiyth hii ya kwamba ni jambo limewekwa katika Shari´ah kuweka/kurudisha mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika kisimamo hichi. Ni jambo liko mbali kabisa kutokana na ujumla wa mkusanyiko wa mapokezi na matamshi ya Hadiyth hii kuhusiana na mtu yule aliyekuwa anaswali vibaya. Bali ni jambo batili. Hadiyth kwa mapokezi na matamshi yake mbalimbali haizungumzii kabisa kuweka/kurudisha mikono katika kisimamo hichi. Ni vipi itafaa kuitumia ili kuthibitisha kuwa mkono wa kulia unatakiwa kuwekwa/kurudishwa juu ya mkono wa kushoto baada ya Rukuu´? Hapa ni pale ambapo hayo matamshi yote yatachangia maoni katika hilo. Mtu asemeje ilihali kwa uwazi kabisa zinathibitisha kinyume chake?

Isitoshe uwekaji uliyotajwa mara ya kwanza sio ambao unafahamika kunapotajwa Hadiyht. Mifupa inayokusudiwa katika Hadiyth iliyotajwa ni uti wa mgongo, linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pindi alipokuwa akiinua kichwa chache anasimama na kunyooka sawasawa mpaka kila pingili ya uti imerudi mahala pake.”

Zingatia na kuwa mwenye inswafu.

Mimi binafsi sina shaka ya kwamba kuweka/kurudisha mikono juu ya kifua katika kisimamo hichi ni Bid´ah inayopotoa. Kwa kuwa kitendo hicho hakikuthibiti kabisa katika Hadiyth zinazohusiana na hukumu za swalah pamoja na wingi wake. Lau kingelikuwa na msingi basi kingelitufikia japo kwa njia moja. Kutokana na ninavyojua hakuna yeyote katika Salaf aliyefanya hivo na wala hakuna imamu yeyote katika maimamu wa Hadiyth aliyelitaja.

Haya hayaendi kinyume nay ale aliyonukuu Shaykh at-Tuwayjiriy katika kijitabu chake, uk. 18-19, kuhusu kwamba Imaam Ahmad amesema:

“Akitaka aiwache baada ya Rukuu´ na akitaka aiweke [juu ya kifua].”

Hivo ndivyo alivyotaja Swaalih bin Imaam Ahmad katika “al-Masaail-ul-Imaam Ahmad”, uk. 90, kutoka kwa baba yake. Hakusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kasema hivo, bali alisema hivo kwa Ijtihaad na maoni yake mwenyewe. Mtu anayetoa maoni anaweza kukosea. Kukisimama dalili sahihi juu ya kwamba kitendo fulani ni Bid´ah – kama hichi ambacho tunakizungumzia sasa – haina maana ya kwamba kitendo kitasita kuwa ni Bid´ah kwa sababu tu maimamu wana maoni hayo, kama alivyothibitisha Shaykh-ul-Islaam katika baadhi ya vitabu vyake. Bali mimi naona katika maneno ya Imaam Ahmad namna ambavyo yeye mwenyewe anaona kuwa kitendo hicho hakikuthibiti katika Sunnah kwa sababu amemwacha kila mmoja aamue na afanye vile anavyotaka. Je, hivi Shaykh muheshimiwa anadhani kuwa Imaam Ahmad vivyo hivyo amempa khiyari [kila mmoja] kuhusu kitendo hicho kabla ya Rukuu´? Hivyo imethibiti kuwa kitendo hicho sio Sunnah, kama yalivyo makusudio.

[3] Ahmad na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 120-121
  • Imechapishwa: 18/02/2017