53. Mlango kuhusu msemo “Ee Allaah! Nisamehe Ukitaka”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiseme mmoja wenu: “Ee Allaah! Nisamehe Ukitaka! Ee Allaah! Nirehemu Ukitaka!” Akate azimio la maombi. Kwani Allaah hakuna amtenzaye nguvu.”[1]

2- Kwa Muslim imekuja kwa tamko lisemalo:

“Anatakiwa aifanye kubwa shauku yake. Kwani Allaah hakioni kikubwa kwa kile alichokitoa.”

MAELEZO

Mwandishi anachotaka hapa ni kubainisha kwamba katika ukamilifu wa Tawhiyd na imani ni kuomba kwa kukata na kutokuwa na mashaka. Pindi muumini anapomuomba Mola wake basi anaomba kwa kukata pasi na kuwa na mashaka. Kwani ukarimu wa Allaah ni mkubwa. Yeye ndiye Tajiri, Mwenye kuhimidiwa. Si sawa kwa muumini kuomba kwa kuvua. Kiumbe ndiye aombwaye kwa kubagua kwa sababu ima akawa si muweza au akawa si mwenye kutaka. Kuhusu Mola ni Tajiri na Muweza.

1- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiseme mmoja wenu: “Ee Allaah! Nisamehe Ukitaka! Ee Allaah! Nirehemu Ukitaka!” Akate azimio la maombi. Kwani Allaah hakuna amtenzaye nguvu.”

Haisilihi kwa mja kuomba kwa kubagua. Kwa sababu kuomba kwa kuvua ni kama kwamba si mwenye dhiki wala mwenye kuhitajia maombi haya. Kwa hivyo ni wajibu awe mwenye kukata. Kwani hakika Allaah hakuna awezaye kumtenza nguvu wala hakuna kimshindacho.

2- Kwa Muslim imekuja kwa tamko lisemalo:

“Anatakiwa aifanye kubwa shauku yake. Kwani Allaah hakioni kikubwa kwa kile alichokitoa.”

Allaah (Ta´ala) ni Mtukufu, Tajiri, Mwenye kuhimidiwa. Kila anachowapa waja Wake ni kidogo na ni chepesi Kwake japokuwa (Subhaanahu wa Ta´ala) atakuwa ni Mwenye kuwapa kitu kikubwa.

Muumini anapaswa awe ni mwenye shauku kubwa kwa vile vilivyoko kwa Allaah. Anatakiwa aufungamanishe moyo wake kwelikweli kwa Allaah, awe ni mwenye kurejea kwa Allaah kikwelikweli na asiwe ni mwenye kuvunjika moyo. Pindi anapomuomba basi amuombe hali ya kuwa ni mwenye shauku kubwa, muhitaji na asivue kitu. Kadhalika anapowaombea ndugu zake asiseme “Allaah akusamehe akitaka, Allaah akurehemu akitaka.” Bali anatakiwa awe ni mwenye kukata na asiseme “Allaah akitaka” hata kama anafanya hivo kwa ajili ya baraka. Asifanye kubagua. Wala hatakiwi vilevile kusema: “Ee Allaah! Nisamehe kwa kile unachokitaka.”

Faida:

Pete ya ndoa haina msingi wowote na ni miongoni mwa matendo ya manaswara.

Hadiyth zote zilizopokelewa kuhusu watu wa Pangoni ni dhaifu. Lakini kuna uwezekano zikawa zinapeana nguvu. Hata hivyo kuna matamshi yaliyosihi kutoka kwa Maswahabah, jambo ambalo linaweza kuzitia nguvu Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Haijuzu kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Lau ungeliiona hali ya Ummah wako basi ungeliuhuzunikia na kuuombea… “ Kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hasikii wala haoni. Kama ilivyokuja katika Hadiyth:

“Hakika wewe hujui waliyozusha baada yako.”[2]

[1] al-Bukhaariy (6339) na Muslim (2679).

[2] al-Bukhaariy (4625) na Muslim (247).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 152
  • Imechapishwa: 06/11/2018