53. Dalili ya kushuhudia kuwa Muhammad (صلى الله عليه وسلم) ni Mtume wa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, ni maneno Yake (Ta´ala):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Kwa hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe. Yanamuhuzunisha yale yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni. Ni mpole na mwenye huruma kwa waumini.” (at-Tawbah 09 : 128)

MAELEZO

Anayetokana na nyinyi wenyewe – Bi maana anayetokana na watu wenu, bali anayeto kati yenu. Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

“Yeye ndiye aliyepeleka Mtume kwa watu wasiojua kusoma wala kuandika miongoni mwao anawasomea Aayah Zake na anawatakasa na anawafunza Kitabu na hekima – na japo walikuwa kabla katika upotofu wa wazi.” (al-Jumu´ah 62 : 02)

Yanamuhuzunisha – Ni mazito juu yake yale yanayokutieni uzito.

Anakuhangaikieni – Kwa sababu ya manufaa yenu na kuwazuieni na madhara.

Ni mpole na mwenye huruma kwa waumini – Mwenye upole na huruma kwa waumini. Amelifanya maalum kwa waumini kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrishwa kupambana vita makafiri na wanafiki na kuwafanyia ushupavu. Sifa hizi ambazo amesifiwa nazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinafahamisha kwamba yeye ni Mtume wa Allaah kikweli, kama ambavo yamefahamisha juu ya hilo maneno Yake (Ta´ala):

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah.” (Muhammad 48 : 29)

Vilevile maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.” (al-A´raaf 07 : 158)

Aayah zilizokuja kwa maana kama hii zinazojulisha kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah wa haki ni nyingi sana.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 74
  • Imechapishwa: 30/05/2020