52. Tafsiri inayoweka wazi maana ya Shahaadah II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu – kwamba tusiabudu isipokuwa Allaah pekee, wala tusimshirikishe na chochote, wala wasifanye baadhi yetu wengine kuwa waungu badala ya Allaah.” Wakikengeuka, basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.” (Aal ´Imraan 03 : 64)

MAELEZO

Sema – Hapa anazungumzishwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili ajadiliane na watu wa Kitabu, mayahudi na wakristo.

Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu – Neno hilo ni “kwamba tusiabudu isipokuwa Allaah pekee na wala tusimshirikishe na chochote na wala wasifanye baadhi yetu wengine kuwa waungu badala ya Allaah”. Tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah ndio maana ya “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”. Maana ya “neno lililo sawa baina yetu na baina yenu” ni kwamba sisi na nyinyi ni vivyo hivyo.

Kwamba tusiabudu isipokuwa Allaah pekee, wala tusimshirikishe na chochote… – Baadhi yetu wasiwafanye wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah kwa njia ya kwamba wakawatukuza kama anavyotukuzwa Allaah, wakawaabudu kama anavyoabudiwa Allaah na hukumu ikafanywa ni kwa ajili ya mwingine.

Wakikengeuka – Wakiyapa mgongo yale mliyowaita kwayo.

Shuhudieni, kwamba sisi ni waislamu – Watangazieni na washuhudisheni ya kwamba nyinyi ni wenye kujisalimisha kwa Allaah na mmejitenga mbali na yale waliyomo na kulirudisha kwao neno hili tukufu, ambalo ni “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 73
  • Imechapishwa: 30/05/2020