Mawalii ni waja wema walio na hadhi na sisi tunawaheshimu, tunawapenda na tunawaiga katika matendo mema. Lakini hata hivyo wao sio washirika pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Wao ni kama sisi ni wenye kumuhitaji na ni mafukara kwa Allaah (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ

“Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah!” (35:15)

Aayah hii ni yenye kuenea.

وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

“Allaah ndiye mkwasi, anayestahiki kuhimidiwa.” (35:15)

Viumbe wote ni mafukara kwa Allaah (´Azza wa Jall) wakiwemo Manabii na Mitume, Malaika (´alayhimus-Swalaatu was-Sallaam). Wote hawa ni mafukara kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Haya yanaondoa utatizi. Watu hawa wanachukua sehemu ya Qur-aan na kuitumia kama dalili na wakati huo huo wanaacha sehemu nyingine. Wanachukua Aayah zinazowatapa na kuwasifu mawalii na wanaacha Aayah nyenginezo zinazobainisha kuwa hawaabudiwi badala ya Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba yule mwenye kutafuta kutoka kwao kitu ilihali ni maiti ni kafiri mshirikina. Wanaziacha Aayah hizi. Huu ni katika upotevu uliyotajwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Hebu chukua kanuni hii: mtu vovyote atavyofikia katika wema, karama na nafasi mbele ya Allaah hana lolote kuhusiana na uola na kwamba haifai kumuomba pamoja na Allaah na kwamba hafanyiwi kitu katika ´ibaadah na kwamba Allaah haridhii hilo.

Mawalii na waja wema wakweli hawaridhii hayo. Kinyume chake wanayakataza kwa ukali kabisa. Wanaoridhia hayo ni wale mashaytwaan ambao wanawaita watu kuwaabudu. Kuhusu mawalii wa Allaah wametakasika kutokamana na hayo. Hawayaridhii. Wanaoyaridhia ni wale mawalii wa shaytwaan. Hii ndio maana ya maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah):

“… lakini nina uhakika kabisa ya kwamba maneno ya Allaah hayagongani, na kwamba maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayaendi kinyume na maneno ya Allaah.”

Ni wajibu kuyarudisha maandiko baadhi yake kwa mengine na baadhi yake kuyafasiri mengine mpaka kile kinachotakikana kiwe wazi. Kitendo hichi, ni kama alivyosema Shaykh, ni jibu zuri linalotakiwa kutiliwa umuhimu kwa kuwa limejengwa juu ya Qur-aan. Mwenye kuliafiki anakuwa amejipatia fungu kubwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 73
  • Imechapishwa: 04/01/2017