52. Maamuma hawataki imamu asome “as-Sajdah” na “al-Insaan” katika Fajr ya ijumaa

Swali 52: Baadhi ya maamuma wanawapinga maimamu wa misikiti kusoma Suurah “as-Sajdah” na “al-Insaan” katika swalah ya Fajr siku ya ijumaa na wanawataka kuigawanya Suurah “as-Sajdah” katika Rak´ah mbili kwa hoja eti kutokuweza kusimama nyuma ya imamu kutokana na uzee wao. Wanajengea hoja kwamba baadhi ya maimamu wa misikiti wanaigawanya. Je, tuyasikie maneno yao katika jambo hilo au kuigawanya, baadhi ya nyakati tuache kuisoma au tuisome siku zote pasi na kuigawanya katika Rak´ah mbili pasi na kujali wanaopinga[1]?

Jibu: Sunnah kwa imamu ni yeye kusoma katika swalah ya Fajr siku ya ijumaa “as-Sajdah” katika Rak´ah ya kwanza na Suurah “al-Insaan” katika Rak´ah ya pili. Asijali maneno ya wale wanaopinga. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiisoma katika swalah ya Fajr siku ya ijumaa ilihali yeye ndiye mwenye kuwahurumia zaidi ya watu, mjuzi zaidi wa watu na mwenye kumuonea huruma zaidi mnyonge.

Akiacha kuisoma mara moja kwa mwezi au miezi miwili ili kuwafunza watu kwamba kule kuisoma sio jambo la lazima na kwamba inafaa kusoma nyingine, ni jambo lisilokuwa na neno.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/395-396).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 09/12/2021